Utekaji, utesaji na mauaji wakati wa utawala wa Idd Amin ni suala ambalo liko kwenye kumbukumbu (living memory) ya Watanzania wengi.
Afisa wa Idd Amin aliyeongoza kikosi cha utekaji, utesaji na mauaji wakati huo alikuwa Brigadier Isaac Malyamungu.
Waliolengwa zaidi kushughulikiwa na Malyamungu walikuwa maofisa wa jeshi, wanasiasa, maafisa wa serikali pamoja na viongozi wa dini walioshukiwa au kutuhumiwa kuupinga utawala wa Amin.
Tofauti na utesajii unaodaiwa kufanyika hapa nchini, huko Uganda mara nyingi utesaji na mauaji vilikuwa unafanyika hadharani ili iwe "funzo" kwa wengine. Pia udhalilishaji ulikuwa ni wa kutisha. Wanaume walikuwa wanakatwa sehemu za siri na kulazimishwa kutembea barabarani wakizipepea!
Mauaji yalikuwa yanafanyika kwa kuwalaza watuhumiwa barabarani na kifaru cha kijeshi kupitishwa juu yao. Na mara nyingi hii kazi alikuwa anaifanya Malyamungu mwenyewe.
Tofauti na hapa nchini ni kwamba wakati huo Uganda ilikuwa inaendeshwa kijeshi; bila kufuata katiba wala sheria. Hivyo, watu kutekwa, kuteswa na "kupotezwa" hapa nchini kwenye mazingira ya kuwepo kwa katiba (tena inayozinatiai haki za binadamu) na sheria ni jambo ambalo halipaswi hata kufikirika.
Historia ni mwalimu mahiri. Hakuna utawala wowote katika historia ya dunia uliofanikiwa kwa kutumia njia hizi chafu.