Kila nikipota mtaani nakutana na Mabango ya mama hana deni. Nikipita mitandaoni nakutana hashtags kwamba "Mama hana deni", "Mama ametenda" au Mama yuko kazini".
Wabunge tuliowatuma kwenda bungeni nao wanaimba wimbo ule ule Mama hana deni. Tufafakari pamoja, ni kweli hana deni au sisi hatumjui mdeni wetu?
Kwa nchi yoyote ile ili ipate maendeleo lazima serikali iwekeze kwenye shughuli ambazo zinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja. Watanzania waliowengi wapo kwenye haya makundi matatu, aidha ni wakulima, wafugaji au wafanya biashara. Je maisha ya makundi haya matatu yana yali gani kiuchumi?
Kilimo ndio shughuli inayoongoza kwa mchango mkubwa kwenye pato la taifa. Serikali imeyagusa vipi maisha ya wakulima juu ya masoko na bei ya mazao yao? Kodi na ushuru wa mazao?
Uchakataji na uongezaji wa thamani ya mazao ya kilimo? Mbolea na pembejeo za kilimo, upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ? Ni wazi kwamba bado Kuna changamoto kubwa kwenye kila aspect ya kilimo kuanzia kwenye masoko, uchakataji, Pembejeo za kilimo, ushuru wa mazao, uhaba wa maji kwa ajili ya umwagiliaji nk. Bado Kuna kazi kubwa sana ya kuhakikisha maisha ya wakulima.
Moja ya jambo muhimu kuliko yote kwenye kuongeza tija ya kilimo ni upatikanaji wa maji kwa ajili ya umwagiliaji. Ni wazi kwamba wakulima wengi wanalima kwa kutegemea mvua. Wastani wa miezi ya mvua ni Kati ya miezi 4 hadi 5 Kati ya miezi 12. Miezi 7 au 8 hakuna uzalishaji wa kilimo. Maeneo mengine mvua haitoshi. Kwa mikoa ya Kanda ya Kati kama vile Dodoma na singida, Vile vile mikoa ya jirani kama Tabora, Shinyanga na simiyu hupokea kiasi kidogo cha mvua chini ya mm 500.
Ni kweli kwamba maana ya ukame inamaanisha uchache wa mvua ila haimaanishi maeneo haya hayana maji. Kuna billions za Lita za maji ardhini ambazo kama serikali ikiwekeza vizuri kwenye uchimbaji wa visima inaweza kufuta kabisa utamaduni wa wakulima kulima kwa kutegemea mvua. Najua Kuna watu wanadhani haiwezekani. Majimbo yote ya marekani yaliyopo upande wa magharibi Kati ya mwaka 1910 hadi 1940 yalikuwa na ukame mkubwa sana.
Serikali ya marekani iliamua kuwekeza kwenye uchimbaji wa mabwawa na visima. Hadi kufikia mwaka 1950, hekta milioni 21 zilikuwa chini ya kilimo cha umwagiliaji. Baada ya tija kuongezeka, serikali ya marekani iliongeza uwekezaji hadi mwaka 1978, hekta 43 zilikuwa chini ya kilimo cha umwagiliaji katika majimbo ya Neva, Florida, New Mexico, Texas nk. Hivyo hivyo imefanyika China na Singapore. Sisi pia Inawezekana.
Hali kadhalika kwenye ufugaji, Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2023, Tanzania ni nchi ya pili kwa idadi kubwa ya mifugo barani Africa baada ya Sudani kusini ikiwa na mifugo milioni 88. Je, maisha ya wafugaji yakoje? Serikali imegusa vipi maisha ya wafugaji juu ya masoko ya bidhaa ya mifugo? Malisho ya mifugo? Uchakataji na uongezaji thamani wa bidhaa za mifigo?nk.
Eneo hili pia Lina changamoto kubwa sana. Ukisoma mpango wa mageuzi ya sekta ya mifugo wa miaka mitano 2021/22 -2025/26, wamebanisha kwama kwa idadi ya mifugo tuliyonayo, wafugaji wanahitaji hekta milioni 103 za maeneo ya malisho ukilinganisha na hekta milioni 3.6 tu ambazo zimetengwa tayari kwa ajili ya malisho. Hekta milioni 99 na zaidi bado zinahitajika kulisha mifugo. Je Mama hana deni?
Ukirudi kwenye sekta ya biashara, haihitaji kujieleza sana, tumeona yaliyotokea kariakoo Kati ya mwaka huu na mwaka jana na miaka yote. Serikali bado inahitaji kuwagusa wafanyabishara kwa unafuu wa kodi na mazingira wezeshi. Matatizo ni mengi sana.
Nimalizie kwa kusema kwamba kila ninapoona Kauli au mabango ya mama hana deni, nashawishika kufikiri kwamba watanzania bado hamjui mdeni wetu.
Wasalaaam