Kumekuwapo na
video inayosambazwa mtandaoni kuwa wanaigeria washikwa na mshangao baada ya mawingu kuripotiwa kuanguka kutoka angani.
Je, upi uhalisia wa madai hayo?
Ukurasa unaoitwa
Tochi celebrity gist coner ulichapisha
picha zinazoonesha hali sawa na inayoonekana kwenye video na kuambatanisha maelezo yanayosema, "Kitu kisicho cha kawaida kinachofanana na mawingu kilichoonekana kando ya Barabara ya Abuja-Kaduna kimezua mjadala mtandaoni, huku baadhi ya watu wakiamini kuwa ni “mawingu yaliyoanguka. Hata hivyo, wengine wanakisia kuwa huenda ni mabaki ya taka za viwandani badala ya tukio la asili."
Akijibu chapisho la
mdau kutoka mtandao wa X kuhusu video hiyo,
Dkt. Ayobola Adebowale anasema hali hii
siyo mawingu.
"Nilishuhudia jambo kama hili kila siku nikiwa mtoto, kwa sababu tuliishi karibu na kiwanda cha kutengeneza sabuni (Global). Ilisababishwa na mabaki ya taka za kiwandani yaliyokuwa yakimwagwa kwenye chanzo cha maji kilichokuwa karibu." Ameandika Dkt. Adebowale.
Aidha
chapisho lingine Instagram linaloeleza kuhusu video hiyo, katika sehemu ya maoni mtu mmoja anasema hali hiyo ilisababishwa na kemikali kugusana na maji na kuleta mwitikio wa kikemikali.
"Nilipita eneo hilo jioni hii nilipokuwa nikirudi kutoka Kaduna, na kila mtu ndani ya gari alisisitiza tusimame ili kuona kilichotokea.
Inaonekana lori lililokuwa limebeba kemikali lilianguka karibu na eneo hilo, na kemikali hizo zikagusana na mto au maji yanayotiririka, jambo lililosababisha mwitikio huo."
Tukio kama hili mkoani Morogoro, Tanzania.
Mwaka 2024 ilisambazwa video mtandaoni kutoka mkoani Morogoro ambapo ilidaiwa mawingu yalidondoka kutokana na mvua kubwa zilizonyesha lakini uhalisia ilikuwa ni mapovu yaliyotengenezwa baada ya kudondoka kwa gari iliyobeba kemikali zinazotumika kutengenezea sabuni kwenye
Kata ya Tungi, Manispaa ya Morogoro.
Kupitia
Gazeti la Mwananchi, Januari 21, 2024, Ofisa Afya Manispaa ya Morogoro, Ndimile Kilatu alisema maofisa wa idara hiyo walifika eneo la tukio (Tubuyu B) kufutilia chanzo cha mapovu katika korongo linalopitisha maji wakati wa mvua na kuyapeleka Mto Ngerengere na kubaini chanzo ni malighafi ya kutengenezea sabuni iliyomwagika Januari 17, mwaka huu kwenye maegesho ya malori ya Dar kuelekea DRC Congo au Zambia katika eneo la Nane Nane.