- Tunachokijua
- Mtangazaji na mshereheshaji mkongwe nchini, Taji Liundi kupitia ukurasa wake wa Mtandao wa Facebook, Taji Liundi, Aprili 14, 2026 alichapisha video yake akieleza kuhusu mwenendo wa hoja za wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kuonekana kulenga kuwashusha hadhi wananchi.
Madai
Kumekuwapo na chapisho linalosambazwa mtandaoni likiwa na nukuu inayodaiwa kutolewa na Liundi kuwa amesema 'bunge la Tanzania lina wabunge vilaza, hawafai'
Je, nukuu hiyo ilitolewa na Liundi?
Ufuatiliaji uliofanywa na JamiiCheck umejiridhisha kuwa nukuu hiyo si ya kweli kwani haikuttolewa na Taji Liundi. Katika video yake aliyoichapisha Aprili 14, 2026 hakutoa kabisa kauli hiyo.
Aidha kupitia Ukurasa wake wa Facebook Taji ameikanusha nukuu hiyo huku akisema "Nawafahamu. Sipo upande wenu na sina mapambano dhidi ya serikali, bunge mahakama wala viongozi wa nchi yangu. Taji liundi hamumjui!! Mmekosa agenda. Mnadandia punje zozote kuhalalisha mapambano yenu babaifu. Hapa mmefeli!! Na sio tu kufeli hii channel yenu ya mchongo mmeiua."
Rejea hapa nukuu halisi kutoka kwenye video ya Liundi.
"Yaani kusema kweli naogopa kurekodi hii video kwa sababu nina hasira sana. Na unapokuwa na hasira mtu bora tu uahirishe unachotaka kukifanya, lakini ningependa tu kusema, waheshimiwa wabunge, wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, acheni kutufanya Watanzania mazu-zu.
Kwa sauti yangu na sauti nyingine ambazo ningependa zipaze sauti kama umechukizwa, hii ni notice, notice kwenu waheshimiwa wabunge. Notice ya wananchi wa Tanzania kuwaambia kuweni serious ama achieni madaraka.
Sisi ni watu ambao tuna matatizo lukuki, tuna sonona kuu, tunapambana na hatuungi. Acheni mzaha. Ngoja nisizungumze zaidi nina hasira kweli. Nisije nikazungumza kitu ambacho kitaleta tafrani katikati ya taifa.
Huwa tunakaa kimya, tunakaa kimya tunaogopa. Tunakaa kimya hatusemi ukweli. Tunakaa kimya watu wenye uwezo. Lakini inafika hatua ninyi ambao mnasema sasa hivi hamkai kimya mnatudharau. Leo ninapost hii video. Naacha kuogopa sasa hivi.
Wabunge, wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hii ni notice kwenu. Mheshimiwa spika, nakufahamu vizuri na wewe pia ukiniangalia unanifahamu vizuri sana. Leo nazungumza na wewe. Msiruhusu mazungumzo ya kipumbavu ndani ya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tafadhalini sana."