Kumeibuka picha inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, hususan Facebook na Instagram, ikionesha kinachodaiwa kuwa cheti cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kikitumika kama kifungashio cha maandazi.
Baada ya kufanyika kwa ufuatiliaji, imebainika kuwa cheti hicho si halisi na hakijatolewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, bali kimetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya akili unde.
Chapisho hilo limezua mjadala mkubwa mtandaoni, huku likiambatana na uvumi kwamba katika baadhi ya maeneo nchini Tanzania, vyeti au nyaraka muhimu zimekuwa zikitumika kufungashia bidhaa mbalimbali kama maandazi, samaki na vitu vingine.
Akichangia kuhusu picha hiyo kupitia mtandao wa Instagram, mmoja wa watumiaji wa mitandao ya kijamii alibainisha dosari zinazoonesha kuwa cheti hicho si cha kweli. Alisema:
“Cheti hiki si halisi. Fonti iliyotumika kwenye kichwa cha cheti ni tofauti na ile inayotumika kwenye vyeti rasmi vya UDSM. Pia, nembo ya UDSM haipo katika muonekano huo; nembo halisi huwa na mkono unaoshika mwenge pamoja na kitabu kilichopo pembeni kwa muundo tofauti. Aidha, maandishi ya daraja la ufaulu (Grade/Class) yametumia fonti tofauti na ile ya kawaida inayotumika kwenye vyeti halisi, ambayo mara nyingi hufanana na Bickham Script Pro.”
Aidha mpangilio wa sahihi katika haufanani na vyeti rasmi vya UDSM, kadhalika hazifanani na sahihi za wahusika waliotakiwa kuweka sahihi hizo mwaka 2022 mfano ni makamu mkuu wa chuo hicho Profesa William Annangisye.
Licha ya uvumi huo kuenea ukurasa wa chuo kupitia mtandao wa
instagram umekanushana taarifa kwa kusema kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kinapenda kuufahamisha umma kuwa picha ya cheti inayosambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikidaiwa kuwa ni cheti halisi cha chuo hicho si ya kweli. Chuo kimebaini kuwa picha hiyo imetengenezwa kwa njia ya kidijitali kwa lengo la kupotosha wananchi na kuharibu taswira ya taasisi hiyo ya elimu ya juu.
Hivyo, UDSM inapenda kusisitiza kuwa hakijahusika kwa namna yoyote katika utoaji wa cheti hicho kinachosambazwa.
Aidha, UDSM imeeleza kuwa vyeti vyake halisi vina alama maalum za usalama, muundo rasmi uliothibitishwa pamoja na mpangilio maalum wa saini za viongozi wa chuo ambao hutumika kuthibitisha uhalali wa cheti husika. Chuo kimefafanua kuwa baadhi ya taarifa zinazoonekana katika picha hiyo ya kugushi, ikiwemo matumizi ya saini ya “Registrar”, haziendani na utaratibu rasmi wa utoaji wa vyeti vya UDSM.
Aidha kupitia Google reverse Image Search imebainika
picha ambayo inayoelekeana na hiyo ikidaiwa kuwa ni cheti kilichotolewa na moja ya chuo kikuu kutoka nchini Nigeria ambayo pia inaonekana kutengenezwa kwa Akili Unde.