Katika hatua nyingine, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imesema haipokei msaada wa kibajeti kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo.
Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais (Fedha na Uchumi), Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini, Ali Abdallah Ali katika kikao cha Baraza la Wawakilishi.
Waziri Mwinyihaji alisema kwamba, fedha ambazo Zanzibar imekuwa ikipokea kama msaada wa kibajeti, ni zile zinazotolewa na wahisani kupitia Serikali ya Muungano na Zanzibar kupewa gawio lake kupitia mfumo wa asilimia 4.5.
"Mheshimiwa Spika, si kweli kwamba Serikali ya Muungano husaidia bajeti ya SMZ, isipokuwa husaidia katika upatikanaji wa fedha zinazotolewa na washirika wa maendeleo, kama misaada ya kibajeti," alisema Waziri Mwinyihaji.
Mapema, mwakilishi huyo alitaka kujua iwapo ni kweli Serikali ya Jamhuri ya Muungano huipatia Zanzibar misaada kwa ajili ya bajeti yake. Waziri Mwinyihaji alisema katika kipindi cha 2001 hadi 2009, jumla ya sh 2,530,889, zilitolewa na wahisani kusaidia bajeti, ambapo Zanzibar ilinufaika na sh milioni 115,599.
Hata hivyo, alisema tume ya pamoja, tayari imekwishapitia vyanzo mbalimbali vya mapato na kutayarisha ripoti yake itakayosaidia kuwepo mfumo bora wa mgawo baina ya pande mbili za Muungano, kwa vile kiwango inachopata Zanzibar ni cha muda mrefu.
Wakati huo huo, Dk. Mwinyihaji alisema kuwa, Zanzibar imekuwa haipati gawio la kodi kutoka kwa mabenki yanayotoa huduma zake Zanzibar, kwa vile kodi hizo hulipwa makao makuu ya benki hizo Tanzania Bara.
Aliyasema hayo wakati akijibu swali la Mwakilishi, Ali Abdallah Ali wa Jimbo la Mfenesini katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea mjini Zanzibar.
Alisema kwamba benki nyingi zinazotoa huduma Zanzibar ni matawi ukiondoa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ambayo makao makuu yake yapo Zanzibar.
Aliyataja matawi ya benki yanayotoa huduma Zanzibar kuwa ni NBC, NMB, CRDB, Barclays, TPB, PBZ, KBC, Exim, FBME na Diamond Trust Bank, ambapo hulipa kodi serikalini pale zinapopata faida katika uendeshaji wake.
Hata hivyo, alisema ni vigumu kuweza kufahamu takwimu sahihi za viwango vya kodi vinavyolipwa na benki zinazofanya shughuli zake Zanzibar kwa vile zinaendeshwa kama matawi.
Waziri Mwinyihaji alisema mbali na Zanzibar kupoteza mapato, vile vile inakosa mapato yatokanayo na faida ya uwekezaji ambayo hupaswa kulipa mwekezaji kwa wateja wao na kodi ya ushuru wa dhamana kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa kutoka nje.
Aidha, alisema Zanzibar hupoteza kodi itokanayo na kipato cha mishahara ambayo hukata wafanyakazi wa mabenki yaliyopo Zanzibar kwa vile kodi hiyo huingizwa katika Hazina ya Muungano.
Awali, Mwakilishi Ali Abdallah Ali, alitaka kujua Zanzibar inanufaika na kiasi gani cha fedha kufuatia uwekezaji wa mabenki yanayotoa huduma zake Zanzibar.