BARAZA Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) limetoa siku saba kwa mahakama kutoa ufafanuzi wa hukumu ya kifungo cha miezi sita jela, aliyopewa mshitakiwa Ally Sururu na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam baada ya kukaidi amri ya kuvua kofia ya Kiislamu (baraghashia) akiwa kizimbani.
Kwa mujibu wa Bakwata, hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Wilberforce Luhwago baada ya mshitakiwa huyo kukaidi agizo hilo alilompa akiwa kizimbani na kusababisha majibizano yaliyofuatiwa na hukumu hiyo.
Waislamu tunaamini kuwa Hakimu Luhwago ni kirusi cha udini kinachofanya katika chombo cha kusimamia sheria, tunaiomba mamlaka husika kufuatilia jambo hili kwa haraka na kumwajibisha mhusika ili Waislamu wa Tanzania waendelee kuwa na imani na chombo hiki
, alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Umoja wa Vijana wa Kiislamu ya Bakwata, Dk Seif Sulle.
Sulle ambaye alikuwa akitoa tamko kwa niaba ya Mufti Mkuu wa Tanzania, Shehe Issa Shabaan Simba, katika Ofisi za Makao Makuu ya Bakwata jana kuwa Dar es Salaam wamelisikia Septemba mosi kupitia vyombo vya habari na limedhalilisha mavazi ya ibada ya Kiislamu na kuingilia uhuru wa kuabudu.
Baadhi ya wanasheria waliozungumza na gazeti hili kwa kigezo cha kutotajwa majina yao gazetini, walisema hakuna sheria ya moja kwa moja inayozuia mtu kuvaa kofia mahakamani ila kuna utaratibu wa kimahakama ambao unahitaji kuheshimiwa na kufuatwa na kila anayepaswa kufanya hivyo.