Habari zimekwishaandikwa katika magazeti ya Kenya kuhusu kuingia kwa wanajeshi wa Uganda nchini Kenya, kwenye mwambao wa ziwa Victoria. Hata picha za video zimekwishachukuliwa. Inaaminika wapo nchini kwa baraka za serikali ya Kibaki.
jana magazeti ya kenya yalitoa ..leo..
MWANANCHI: Posted Date::1/14/2008
http://mwananchi.co.tz/newsre.asp?id=3942
Museven adaiwa kupeleka wanajeshi 3,000 Kenya *Ni kumsaidia Rais Kibaki
*Wakenya wamshangaa
*Mawaziri EAC kukutana
*Viogozi wa kimataifa wazidi kuhaha kutafuta amaniTausi Mbowe na Mashirika ya Habari,
ZAIDI ya wanajeshi 3,000 kutoka nchini Uganda wanadaiwa kuingia nchini Kenya katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo kwa lengo la kuongeza ulinzi nchini humo.
Mkazi wa Busia aliliambia gazeti la Jumapili la Kenya 'The Sunday Standard' kuwa wanajeshi hao kutoka Uganda walionekana katika miji kadhaa huku wengine wakiwa katika eneo la fukwe za ziwa Victoria karibu na mto Suo.
"Wanajeshi kutoka Uganda wapo kwenye sehemu zote za mipaka huku wengi wakifanya doria karibu na ziwa Victoria,"alisema mwalimu wa mmoja wa shule ya sekondari kutoka la Wilaya ya Budalang?i, nchini Kenya.
Mbunge wa Nambale, Chris Okemo alisema baadhi ya wanajeshi hao wameripotiwa kuingia nchini humo lakini wengi wao walionekana katika mji wa Busia.
"Tumepokea taarifa kuwa kuna idadi kubwa ya watu wasiofahamika ambao haijulikani wamekuja kufanya nini Kenya. Wengi wa watu hao ni wanajeshi kutoka Uganda," alisema Mbunge huyo na kuongeza kuwa wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Mbunge mwengine kutoka Bondo, Dk Oburu Oginga naye alisema wanajeshi hao kutoka nchini Uganda waliingia nchini humo usiku kupitia eneo la Mageta wakiwa kwenye makundi makundi.
"Kundi la kwanza lilikuwana askari 12 ambao walikuwa wanaongea lugha ya Kiswahili liliingia eneo la Mageta saa 11 jioni na kuwauliza wenyeji njia ya kufika eneo lengine la Usenge na ufukwe la Uhanya katika ziwa Victoria," alisema Dk Oburu
Kwa mujibu wa Dk Oburu, baada ya saa mbili wanajeshi zaidi waliwasili katika eneo hilo hivyo kulazimika kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Bondo.
"Huu ni ujinga hakuna mtu yoyote anayeruhusiwa kuingia nchini kwetu kwa kisingizo cha machafuko yanayoendelea, Kenya haina vita hivyo Uganda hawapaswi kuleta wanajeshi wao.
"Tunasheria zetu zinazotulinda, wananchi lazima wawakatae wanajeshi hao kutoka Uganda kwani wanatumia hali ya sasa ya nchi yetu kuingia nchini kwetu kwa lengo la kujinufaisha," alisema Dk Oburu.
Kwa mujibu wa The Standard, wanajeshi wengi waliripotiwa kuingia nchini humo na kuonekana kartika maeneo ya Bugoma na wakazi wa maeneo hayo wanasema kuwa waliona mabasi sita yakiwasusha askari hao.
Mpaka sasa Rais Yoweri Museveni wa Uganda ndiye rais pekee aliyetoa pongezi kwa Rais Mwai Kibaki kufuatia ushindi tata alioupata baada ya kutangazwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo (ECK) kuongoza kiti hicho katika kipindi kingine cha miaka mitano ijayo. Rasi Museveni pia alikaririwa akisema kuwa yuko tayari kutoa msaada ulinzi kwa Raisi Kibkai endapo atahitaji msaada huo.
Hata hivyo, Uganda imekanusha tuhuma hizo. Mshauri wa Masuala ya Habari wa Raisi Museveni, John Nagenda alisema tuhuma hizo hazina ukweli wowote na kumnwa hakuna askari wa Uganda waliopelekwa nchini Kenya.
Naye Msemaji wa Jeshi la Uganda, Kapteni Paddy Ankunda, alisema tuhuma hizo si za kweli na kwamba zinalengo la kuichafua Serikali ya Museveni na kuongeza kuwa wanajeshi pekee waliopo nchini humo ni wale walio katika mafunzo maalumu katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Karen kilichopo jijini Nairobi.
Wakati hayo yakitokea wasuluhishi kutoka Jumuia mbalimbali za kimataifa ukiwamo Umoja wa Afrika (AU) wamezitaka pande zote zinazovutana zinazoongozwa na Rais Kibaki na Raila Odinga kutoendelea na hatua zozote ziatakazosababisha kuvunjika kwa hali ya amani nchini humo
Katika taarifa yake iliyosomwa jijini Nairobi jana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon alizitaka pande hizo kuhakikisha kuwa wanapata suluhu ya mgogoro huo ambao mpaka sasa unasadikiwa kusababisha jumla ya watu 500 kupoteza maisha huku zaidi ya Wakenya 300,000 wakikosa mahali pa kuishi kufuatia kubomolewa na kuchomewa makazi yao.
Ki-Moon alizitaka pande hizo kusahau yaliyopita na kuhakikisha amani inapatikana kwa lengo la kuijenga nchi hiyo.
Naye Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja Mataifa, Koffi Annan ambaye awali ilitarajiwa kuwasili nchini Kenya ili kuzikutanisha pande zote zinazovutana alizitaka pande hizo kutotafuta sababu zilizojificha ambazo zitachangiia kutopatikana kwa hali ya amani na kuwataka kushirikiana ili kupatika kwa suluhu.
Naye mshindi wa Tuzo ya Nobel, Askofu Mkuu Desmond Tutu kutoka Afrika Kusini, akizungumza na serikali ya Marekani kwa mara nyingine allisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mazungumzo ya ana kwa ana baina ya raisi Kibaki na Odinga.
Awali Askofu Tutu alifanikiwa kumshawishi Rais Kibaki kukubali kuunda serikali ya mseto na wapinzani wake kwa masharti kwamba kwanza Odinga atambue uwepo wa mamlaka ya serikali, akiimanisha kumtambua kuwa yeye ni Rais halali wa Jamhuri ya Kenya.
Hata hivyo, msimamo wa Rais Kibaki uligonga mwamba kutokana na msimamo wa Odinga ambaye alipendekeza serikali ya mpito ambayo itaanda uchaguzi mpya wa Rais ndani ya miezi mitatu. Tayari Odinga alishatamka wazi kwamba hamtambui Rais Kibaki kwa madai kuwa anaamini kwamba aliiba ushindi.
"Kwa mtazamo wetu ni vizuri kwa Rais Kibaki kukaa pamoja na Odinga bila kuwekeana vikwazo ili kujadili jinsi ya kumaliza mvutano unaoendelea kwa maslahi ya Wakenya, alisisitiza Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshighulikia masuala ya Afrika, Dk Jendayi Frazer.
Kauli hizo kutoka kwa viongozi mbali mbali wa Jumuiya za Kimataifa zilitolewa siku chache baada ya chama cha Orange for Democratic Movement (ODM) cha Odinga kutangaza maandamano makubwa yatakayofanyika kwa siku tatu mfululizo katika miji mbalimbali kuanzia Januari 16.
Annan, ambaye anatarajia kuwasili nchini humo mapema wiki hii kuendeleza sehemu aliyoacha Mwenyekiti wa Afrika, Rais John Kufuor wa Ghana aliitka serikaliya Rais Kibaki na upande wa upinzani kuangalia zaidi wakenya wanataka nini kwa lengo la kuonyesha uongozi bora.
Rais Mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa na Mke wa Rais Mtaafu wa Afrika Kusini, Graca Mandela wanatarajiwa kushirikiana na Annan katika mazungumzo hayo ya kutafuta amani nchini Kenya.
Shirika la Habari la Uingereza (Reuters) limesema kuwa Annan atakuwa na muda mwingi wa kukaa nchini Kenya ikilinganisha na Rais Kufuor, ambaye alikaa nchini humo kwa siku mbili pekee. Hata hivyo Rais Kufour alishindwa kuzipatanisha pande hizo mbili.
Awali marasi wanne wastaafu za Afrika walitembelea nchini humo kwa lengo la kuwafariji wananchi wa kenya. Marasi hao ni Rais Mkapa (Tanzania), Joachim Chisano (Msumbiji), Dk Kenneth Kaunda (Zambia) na Sir Ketumile Masire (Botwana) .
Wakati huo huo viongozi wa makanisa wamewataka Rais Kibaki na Odinga kurejesha hali ya amani nchini humo.
Viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali wamepinga vikali kufanyika kwa maandanao makubwa yaliyopangwa kufanywa na chama hca ODM siku ya Jumatano na kutaka viongozi hao kutumia njia ya mazungumzo badala ya kutumia nguvu.
Kiongozi wa Kanisa la Katoliki John Cardinal Njue alisema kufuatia vifo vingi vya wananchi huku wengine wakipoteza mali zao ni vizuri pande hizo kutumia njia ya maziungumzo badala ya nguvu.
"Nchi inaelekea katika hali mbaya kuita tena maandamano mengine wiki hii ni sawa na kuongeza matatizo yatakayosababisha ghasia tena zitakazosababisha kupoteza maisha ya watu wasio na hatia, "alisistiza Njue.
Jijini Nairobi maaskofu 33 wa Kanisa la Anglikana walimtaka Rasi Kibaki na Odinga kuwa tayari kwa mazungumzo yenye lengo la kuleta suluhu.
Naye Ramadhan Semtawa, anaripoti kuwa kufuatia ghasia zinazoendelea nchini Kenya, Baraza la Mawaziri la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) linatarajiwa kukutana katika mkutano wa dharura kujadili hali ya maafa ya kibinadamu nchini humo.
Mkutano huo wa dharura wa baraza hilo la mawaziri wa nchi wanachama wa EAC, utakuwa chini ya Uenyekiti wa Eriya Kategaya ambaye ni Naibu Waziri Mkuu wa kwanza wa Uganda na Waziri wa Afrika Mashariki wa nchi hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Waziri wa Afrika Mashariki wa Tanzania Dk Ibrahim Msabaha, alisema mkutano huo unatarajiwa kufanyika wakati wowote kutegemea mwenyekiti atakavyopanga kwa kuzingatia ratiba za mawaziri wa kila nchi.
Dk Msabaha alifafanua kwamba, mawaziri wa EAC wanajishughulisha na kuangalia athari za kibinadamu kwani jukumu la usuluhishi liko kwa wakuu wa jumuiya hiyo na wasuluhishi wengine wa kimataifa.
Alisema katika mkutano wao, moja ya jambo wanaloangalia katika athari hizo za kibinadamu ni kuona jinsi ya kufikisha misaada na njia za kuikusanya.
Hata hivyo, alisema mawaziri hao tayari wametoa azimio la kuzitaka pande zote zinazopingana nchini Kenya kukaa katika meza moja ya mazungumzo.
"Baraza la mawaziri litakutana kwa dharura ili kujadili namna ya kupata na kufikisha misaada ya kibinadamu. Sisi tumeangalia zaidi athari za kibinadamu, tunajua juhudu za kusuluhisha zipo chini ya wakuu wetu na jumuiya ya kimataifa," alisema na kuongeza:
"Rais Jakaya Kikwete, Yoweri Museveni wamekuwa wakijitahidi kusuhulisha, pamoja na Askofu Desmond Tutu na mwenyekiti wa AU John Kufuor. Hawa wote tunatambua mchango wao katika usuluhishi".
Dk Msabaha aliongeza kuwa uamuzi huo wa kufanya mkutano huo wa dharura umetokana na kauli moja ya mawaziri wote wa nchi za EAC ambayo ilitolewa Januari 11.
Kuhusu raia wa Kenya kuingia nchini kama wakimbizi, alisema hadi jana hakuna Wakenya waliokuwa wameingia nchini kama wakimbizi.
Dk Msabaha alisema Wakenya wote wanaoingia nchini wamekuwa wakija kwa ndugu na jamaa zao na kuongeza kwamba, hakuna mtu aliyeingia na kuhitaji msaada wa kibidanadamu kutoka Serikali ya Tanzania.
Alisema mpaka wa Tanzania uko wazi na kuongeza kwamba, kazi kubwa iliyopo sasa ni kusaidia kutatua matatizo katika nchi wanachama wa EAC ambazo hazina bandari ambazo awali zilikuwa zikitegemea bidhaa zao kutoka Kenya.
Msabaha alisema kwa sasa kunafanyika taratibu ndani ya serikali ya namna ya kusaidia kupeleka mafuta nchini Uganda.
Matokeo tata ya kura za urasi wa Kenya kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika Desemba 27, yameifanya nchi hiyo kuingia katika machafuko makubwa ambayo yamesababisha athari kubwa za kibinadamu na uchumi wa nchi wanachama wa EAC ambazo hazina bandari.