Emmanuel Nkayamba
New Member
- Sep 15, 2021
- 1
- 0
EMMANUEL STANSLAUS NKAYAMBA
Hili ni pendekezo langu kwa viongozi wa Taifa letu la Tanzania kuunda Jeshi la vijana wenye ujuzi na maarifa ya uzalishaji wa kilimo na ufugaji wa kisasa, na kisha kuwawezesha vijana hao kuingia moja kwa moja katika uzalishaji wa kilimo na ufugaji badala ya kusubiria ajira za serikali.
Ninaamini kuwa tunahitaji kutengeneza mbegu ya wakulima wenye utaalamu na maarifa ya kisasa, ambao wataenda kupandwa katika miji na vijiji mbalimbali ili kuambukizana na wakulima wengine maarifa na uzoefu baina yao. Ninapendekeza kuwa kazi kuu ya Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo na Mifugo iwe ni kuandaa wakulima na wafugaji wa kisasa, pamoja na watafiti ambao maabara zao za kiutafiti ni mashamba halisi wanayoyalima wao.
Mkakati huu wa kuyaweka mafunzo ya kilimo katika vitendo vya ukulima na ufugaji wa kisasa utakuwa ni sehemu ya alama za ufaulu wao kwa njia ya vitendo. Pindi kijana anapohitimu katika moja ya vyuo vinavyotoa mafunzo ya kilimo, mifugo au uvuvi, kijana huyo hatahesabika kuwa tayari amefaulu masomo yake, bali atapewa eneo na zana stahiki ili ashiriki katika mwaka mmoja wa masomo kwa njia ya uzalishaji. Katika uzalishaji wake, mwanafunzi huyo atakuwa chini ya usimamizi wa wataalamu kutoka chuo alichosomea, na chini ya Mkuu wa Wilaya wa mahali anapofanyia mazoezi ya uzalishaji wake.
Lengo ni kutengeneza wataalamu wa kilimo ambao watakuwa mfano hai wa kuonyesha na kufundisha wakulima kwa njia ya vitendo, kwa wao wenyewe kujihusisha na uzalishaji utakaomvutia mkulima wa eneo husika. Hatupaswi kuendelea kuzalisha wataalamu ambao wanaishia kuwa wakaguzi wa mashamba na mifugo ya wakulima, bali tunahitaji wataalamu watakaoenda kuwa wakulima wa mfano katika jamii zao. Tunapaswa tutoke katika dhana ya kutengeneza wataalamu wa kilimo na tuanze kutengeneza wakulima na wafugaji wenye utaalamu unaohitajika.
Wakulima wetu wanahitaji kujifunza kwa vitendo kutoka kwa wale waliohitimu katika vyuo vya mafunzo ya kilimo na mifugo, badala
ya kufundishwa kwa maneno ya wataalamu wa kilimo na mifugo. Wakulima wataamini kwa kuona matunda ya kazi nzuri zinazofanywa na vijana waliohitimu kutoka katika vyuo vyetu vya kilimo na mifugo. Darasa bora la kilimo ni shamba lenye matokeo mazuri, na mwalimu bora wa kilimo ni mkulima wa kisasa mwenye matokeo mazuri ya kazi yake, kwa kutumia mbinu na zana za kisasa katika kuzalisha mazao au mifugo yenye ubora.
Pindi mhitimu wa vyuo vya mafunzo atakapofanikiwa kuthibitisha kwa wataalamu na jamii yake, kuwa alichojifunza chuoni kina faida ya kuigwa na jamii husika, hapo mhitimu huyo atapata alama za mwisho zitakazomuwezesha kupata cheti kinachothibitisha kuwa yeye ni mkulima wa kisasa, mwenye utaalamu wa kilimo, mifugo au uvuvi.
FAIDA ZA MKAKATI HUU KWA JAMII NA KWA WAHITIMU WENYEWE
Mapinduzi ya aina yeyote yanahitaji wanajeshi au wapambanaji wa kuyaleta matokeo ya hayo mapinduzi. Lakini wanamapinduzi hao wanahitaji kuandaliwa kimtazamo, kimaarifa, kiujuzi na kivifaa, ili wawe tayari kutimiza wajibu wao na matarajio yetu kwao.
WAHITIMU WA KILIMO WATANUFAIKA KAMA IFUATAVYO
- Watapewa maeneo na nyenzo za kuwasaidia kuimarisha mbinu walizojifunza, kwa kuzitumia katika uzalishaji kwa njia ya vikundi vidogo vidogo.
- Watapata vipaumbele vya soko la mazao yao ya ukulima au ufugaji pindi watakapokuwa wametoa matokeo bora. Serikali na jamii itatoa kipaumbele kwa mazao yao na kisha kuwapa 80% ya mapato kama sehemu ya mtaji wao wa kujiendeleza katika uzalishaji binafsi.
- Kwa wale watakaofanya vizuri katika hatua hii ya zalishaji watapata kipaumbele cha mkopo wa vifaa vya kisasa kutoka katika Benki ya Maendeleo ya kilimo (Tanzania Agricultural Develomennt Bank)
- Jamii itapata fursa ya kujifunza kwa vitendo faida za matumizi ya mbinu na nyenzo bora za kilimo katika kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao na mifugo. Kwa kuwachanganya wataalamu hawa na jamii walizotokea, jamii itapata fursa ya kuona hatua kwa hatua jinsi ya kufanya mambo kisasa na faida zake.
- Jamii pia itapata ongezeko la mazao ya biashara na chakula kwani kila mwaka serikali itakuwa inaongeza wakulima wa kisasa waliondaliwa katika vyuo vya mafunzo ya kilimo.
- MAHITAJI YA KUANZISHA NA KUFANIKISHA MKAKATI HUU
- Maboresho ya vyuo vya kati vya kilimo na mifugo, ili viwe na nyenzo za kisasa zinazoendana na mahitaji ya kutengeneza wakulima wa kisasa wenye utaalamu wa kuleta mapinduzi ya kilimo nchini. Maboresho haya yaguse katika uwezo wa vyuo hivi katika vifaa vya kutolea mafunzo na uwezo wa kupokea idadi kubwa ya watu watakaopata hayo mafunzo.
- Mapinduzi ya kilimo nchini yanahitaji mapinduzi ya kiitikadi. Tunahitaji namna mpya ya kukiona kilimo na ufugaji. Huu ni mkakati unaotakiwa kumilikiwa na wadau wote husika wa kilimo. Malengo na mipango-kazi vinaweza kubuniwa na wataalau wachache, ila utekelezaji unahusisha wadau wote. Pa, kuna umuhimu wa kuanzisha redio maalumu kwa ajili ya uenezi wa taarifa kuhusu mbinu mbalimbali za kilimo, yenye uwezo wa kusikiwa nchi nzima.
- Pia nyongeza ya progamu maalumu za luninga ambazo zitajikita kutoa mafundisho zaidi, ya utaalamu wa kilimo. Vyombo vya habari kama hivi vina umuhimu mkubwa sana katika kubadili uelewa na namna ya kufikiri kwa wadau wa kilimo.
- MAKUNDI YA WADAU WA MKAKATI HUU
- Wakulima
- Wagani,
- Watafiti
- Wakufunzi wa vyuo vya mafunzo ya kilimo na mifugo
- Wanafunzi wa vyuo vya kilimo na mifugo
- Wafanya biashara wa mazao ya kilimo na mifugo
- Watumiaji wa mazao na bidhaa za kilimo na mifugo
- VIKOSI MAALUMU KWA KAZI MAALUMU
- Huu ni utekelezaji wa wazo la Jeshi la Mapinduzi ya Kijani kwa kuunda vikosi maalumu vya vijana wakulima ambao; watapata mafunzo maalumu kuhusu uzalishaji wa mazao maalumu ambayo yana umuhimu mkubwa katika kuinua uchumi wa nchi.
- Kwa kuanzia mkakati huu, mazao tunayotakiwa kuyapa kipaumbele katika katika mkakati huu ni yale yenye umuhimu mkubwa kiuchumi nchini, ambayo ni:
- Kilimo cha zo la miwa ili kuongeza kiwango cha sukari kama moja ya bidhaa muhimu nchini
- Kilimo cha alizeti kama zao muhimu katika kutengeneza mafuta ya kupikia
- Kilimo cha pamba kama zao muhimu katika maendeleo ya viwanda
- Kilimo cha mpunga kama zao la muhimu katika usalama wa chakula nchini na biashara
Ili mkakati huu uwe na matunda ni muhimu kuwepo na soko imara na la moja kwa moja la mazao ya vikosi hivi, na kuwepo na viwanda vyenye uwezo wa kuchakata mazao haya kuwa bidhaa zilizotayari kwa matumizi. Ni muhimu viwanda hivi viwe ni sehemu ya serikali katika umiliki, usimamizi na uendeshaji wake.
EMMANUEL STANSLAUS NKAYAMBA
0764100586
Upvote
1