Viongozi wa CHADEMA wakamatwa Geita
na Edward Kinabo, Geita
[Source: Tanzania Daima]
VIONGOZI wawili wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wilayani hapa, juzi jioni walikamatwa na polisi jirani na kituo kikuu cha mabasi mjini hapa, wakituhumiwa kumshambulia muuza magazeti, Abbas Omari.
Viongozi hao ni Katibu Mkuu wa chama hicho wilayani Geita, Rogers Ruhega (34) na Katibu wa Kata, Paul Vincent (33), ambao walikamatwa wakidaiwa kumshambulia muuza magazeti huyo katika eneo lake la biashara.
Muuzaji huyo wa magazeiti alifungua RB namba GE/IR/1055/2009 katika kituo kikuu cha polisi wilayani Geita, akielezea kushambuliwa na viongozi hao.
Viongozi hao wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, jana asubuhi, walisema chanzo cha tukio hilo ni kunyofolewa kwa habari zinazohusu wasifu wa mgombea ubunge wa CHADEMA, Jimbo la Busanda katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili.