Mimi natatizika mpaka Kichwa kinaniuma Kwa nini Sokoine apewe sifa Sana wakati wake mambo yalienda harijojo??
Ukitaka kujua na kuondokewa na huko "kutatizwa" kwako kwa nini "Mambo yalikwenda harijojo," kama usemavyo; na bado Sokoine aliendelea/anaendelea "kupewa sifa sana yeye," ni lazima ujue sababu za hayo mambo kwenda harijojo, na juhudi zilizokuwa zinafanyika kurekebisha.
Wananchi walielezwa na walijua kwa nini mambo yalikwenda yalivyokwenda wakati huo, na walijua kwamba sio Sokoine wala serikali aliyokuwa akiiongoza iliyosababisha 'harijojo'.
Uchumi sehemu zote duniani wakati huo ulikwama, ukianzia kwenye matatizo yaliyotokana na vurugu za wakubwa wa Magharibi na Mashariki,.
Vita vya Israel na waarabu na bei za mafuta kupanda sana. Na kama hayo hayakutosha, nasi tukapata mgogoro wetu hapahapa kwenye ukanda wetu, wa vita na Uganda. Hili lilitudidimiza sana; lakini hatukuwa na njia ya kuiepuka vita hiyo. Ilikuwa ni lazima tuipigane.
Na licha ya yote hayo - fahamu uchumi wetu ulikuwa unategemea nini - mazao yetu makuu yaliyokuwa yanatuingizia pesa za kigeni yalikuwa Kahawa, katani, pamba, Chai.
Bei za mazao yote haya wakati huo ilishuka sana. Brazil alichukua soko lote la kahawa, na mkonge, ukapata mshindani wa nguvu kweli kweli, 'synthetic fibres', nylon. Kamba za mkonge hazikuwa na wanunuzi tena, na magunia ya nylon ndio kila nchi iliyategemea. Mkonge ukafa kifo cha kibudu!
Chakula pia ikawa shida, kwa sababu ya ukame, kwa hiyo ikabidi kuangukia "yanga" wakati fulani. Lakini hakuna mTanzania aliyekufa kwa njaa. Pasingekuwa na juhudi nzuri na mipango mizuri iliyotumika, pengine historia yetu hadi sasa ingekuwa inaonyesha aibu ya waTanzania kufaa kwa sababu ya kukosa chakula. Hili pia inabidi ulielewe wakati unapojaribu kuelewa kwa nini waTanzania walienzi uongozi wao wakati huo.
Ukisikiliza kwa makini sauti za wanaolaumu, utadhani kuwa ni Tanzania pekee iliyokumbwa na matatizo ya kiuchumi wakati huo. Kenya walikula "Yanga", pamoja na kwamba wao ndio hutumiwa kama mfano wa mafanikio katika eneo hili letu kila tunapolinganishwa. Lakini unafuu waliokuwa nao Kenya pia unaelezeka sababu zake.
Sasa, kama kweli uliuliza swali kwa nia ya kutaka kujua, nadhani unaweza kuanzia hapo, na kuendelea kujijengea uelewa mwenyewe kwa kuchambua mbivu na mbichi kila unapokutana na mijadala ya aina hii.
Nitashukuru kupata 'feed back'.