MUZIKI HALISI USO KWA USO NA HAMZA KALALA
Hamza Kalala :“Muziki wetu ulikuwa na kila sababu za kuishi, kwani ulitengenezwa kwa ustadi wa hali ya juu. Kulikuwa kuna hatua nyingi za kupitia hadi kufanikiwa kurekodi muziki na kupigwa redioni,”
“ Baada ya mtunzi kutunga muziki, ulienda kufanyiwa mazoezi katika maeneo maalumu. Mara nyingi maeneo hayo yalikuwa ni yale yenye watu, kama vile baa au hata maeneo ambayo kuna muingiliano wa watu”.
Lengo hasa ilikuwa ni kuangalia muitikio wao. Ikiwa watu wataonekana kuvutiwa zaidi na tungo za wimbo husika basi hiyo huonekana kuwa ni dalili nzuri.
“Lakini ikitoka hatua hiyo, hatua inayofuata huwa ni kwenda kuujaribu wimbo huo kwenye steji, ndani ya kumbi zetu tulizokuwa tukitumia kufanya maonyesho yetu. Pale tulikuwa tukisoma muitikio wa mashabiki wetu” anaongeza “ Wimbo mkali hukubalika kutoka kwenye hatua za awali kabisa”.
Baada ya kuupiga kwenye kumbi za muziki kwa majaribio, hatua inayofuata huwa ni kuuwasilisha wimbo huo kwa wataalamu kwa ajili ya kupitiwa.
Wataalamu kama Suleiman Hegga walihusika na jambo hili.
Hapa mashairi ya wimbo yalipitiwa neno kwa neno, na kisha maudhui yalihakikiwa, kabla ya wanamuziki kusikilizwa ikiwa wametamka kwa usahihi maneno yaliyomo ndani ya tungo husika. Matatizo ya lafudhi yalisahihishwa katika hatua hii.
“Ikitokea mwimbaji akatamka Lamazani, badala ya Ramadhani, wimbo utarudiwa, hadi pale neno hilo litakapotamkwa kwa usahihi” anaongeza “ Si hivyo tu hata ikitokea kuwa wimbo unamzungumzia mtu mmoja, kwa mfano mwanaume anamlalamikia mke wake hadi mwisho, watalaamu hawa hushauri kuwako kwa majibu ya malalamiko yanayotolewa hivyo kuingizwa kwa sauti ya mwanamke ndani yake”.
Na hii ndiyo sababu nyimbo nyingi za zamani zilikuwa na sehemu mbili sehemu ya kwanza inakuwa na malalamiko huku ya pili inakuwa na majibu au wakati mwingine muziki huo ulikuwa ukija na kisa, kilichosimuliwa kwa umahiri kama kisa hicho kinahusisha watu wawili basi wote walikuwa wakihusishwa kila mhusika kwa nafasi yake.
Kwa mfano kwenye wimbo wa Nachelewa stendi ya basi ulioimbwa na bendi ya Toma Toma kukiwa na sauti za wanamuziki mahiri kama Marehemu Adam Bakari (Sauti ya Zege). Mume anauliza “Kila siku mke wangu unarudi saa za usiku, ufikapo nyumbani macho yau yau. Nimevumilia sasa nimechoka. Leo nataka unieleze ukweli wapi unapochelewa...?” Mke anajibu “ Nachelewa stendi ya basi bwana eee, tabu ya mabasi waijua mume wangu, nihurumie bwana...”
Unaposikiliza muziki kama huu, unaweza ukagundua kazi kubwa iliyofanyika hadi kufikia hatua ya kurekodiwa kwake.
Kwa mantiki hiyo muziki wa wakati ule ulikuwa na kila sababu ya kuwa na uhai, kwani ulifanyiwa kazi kwa umahiri na weledi mkubwa anafafanua.
Kinachofurahisha zaidi ni kwamba, kulikuwa na watu wengi waliohusishwa kwenye utengenezaji wa muziki.
Kwa mfano, prodyuza alikuwa mwingine, mtaalamu wa sauti mwingine na pia vyombo vyote vya muziki kama vile tarumbeta, gitaa na ala nyingine vilipigwa na mtu mmoja mmoja tofauti na sasa.
Mambo kama haya yalichangia kwa kiasi kikubwa kuufanya muziki wa wakati ule kuishi muda mrefu.