MZEE SALUM ZAHORO NA KIKO KIDS
Mzee Salum Zahoro alizaliwa 1937 mkoani Tabora. Alisoma katika shule ya msingi ya White Fathers ya Tabora kuanzia 1944 hadi 1948 alipokatishwa masomo na kupelekwa kusoma kuraani.
Alianza muziki tangu 1953 akiwa Kiko Kids, ambayo baadaye alikuwa kiongozi wake mkuu. Awali alikuwa akipiga tumba, lakini baadaye alijifunza kupiga gita la solo na kuimba.
jina la Salum Zahoro linawakumbusha watu enzi za miaka ya 1960 na 1970 wakati bendi ya Kiko Kids iliyokuwa na maskani yake Tabora ilipokuwa ikitingisha nchi.
Vibao kama vile Wamtetea bure, Sili Sishibi, Umeniasi mpenzi, Mpenzi wangu wanionea, Tanganyika na Uhuru na Bahati ni miongoni mwa vilivyoipatia sifa kubwa bendi hiyo, vikiwa ni utunzi wake Zahoro.
Alirekodi nyimbo zake nyingi katika studio za Asanandi iliyokuwepo Mombasa, Phillips na Daudia zilizokuwepo Nairobi nchini Kenya, lakini fedha alizopata hazikulingana na jasho lake.
Kiko Kids ilikufa kifo cha kawaida 1972 baada ya wanamuziki kadhaa kuondoka. Zahoro alijitahidi kuifufua kwa kuwapa mafunzo wanamuziki wapya, lakini ilipofika 1984, alipatwa na matatizo ya kifamilia yaliyomfanya aachane kabisa na muziki.
Aliamua kurejea tena katika muziki mwanzoni mwa 1990 baada ya kuundwa kwa bendi ya Shikamoo Jazz na hadi umauti , alikuwa mmoja wa wanamuziki wa bendi hiyo, akiwa kiongozi, mwimbaji na mpiga gita la solo.
Zahoro aliwahi sema kutokuwepo hata kuisikia sheria ya hatimiliki ni sababu kubwa iliyowafanya wanamuziki wa enzi zake kutonufaika lolote kutokana na muziki.
"Kungekuwepo na sheria hiyo tangu enzi zetu, bila shaka hivi sasa ningekuwa na maisha mazuri, ningemiliki nyumba na gari. Lakini maisha yetu sisi wanamuziki wa zamani wa Tanzania ni duni na hata hatima zetu ni za wasiwasi,"
Zahoro ........Kufa kwa bendi nyingi za zamani kulichangiwa na uchakavu wa vyombo kwa vile nyingi zilikuwa zikimilikiwa na watu binafsi, ambao hawakuwa na uwezo wa kununua vyombo vipya.
Mzee Zahoro siku za mwishoni alikuwa kiongozi wa Shikamoo jazz, Bendi hii ilianzishwa na taasisi ya Helpage International, iliyokuwa na makao makuu yake nchini Uingereza, ambayo ilikuwa ni maalumu kwa ajili ya kuwasaidia wazee. Taasisi hii ndiyo iliyoipeleka bendi hii kufanya maonyesho mara kadhaa katika nchi mbalimbali za Ulaya, ikiwemo Uingereza.
“Mwaka 1994 alikuja mzungu kutoka London aitwaye Rony Graham aliyekuwa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Help Age International, akaniomba nikusanye wakongwee kadhaa ili tutumbuize kwenye sikukuu ya Kampuni yao,”
Zahoro anasema kuwa, akawachukua Kassim Mponda, Ally Rashid, Athuman Manicho, Kassim Mapili, Suleiman Majengo, Mohammed Tungwa, John Simon, Ally Adinani ‘Jimmy’ na Juma Mrisho.
Alisema kuwa, kazi walioifanya vijana hao wa zamani katika Sikukuu hiyo ya Help Age ilimsisimua muingereza huyo kiasi akaamua kumshawishi Zahoro kuanzisha bendi, ambapo alipokubali akanunulia vyombo na kukabidhi.
Zahoro alifariki mwanzoni mwa mwezi February 2021
View attachment 2643872
Sent using
Jamii Forums mobile app