TUHUMA za ufisadi ambazo zimesambazwa katika mtandao wa intaneti zikihusu utendaji kazi wa viongozi wakuu ndani ya Benki ya Posta (TPB) na wale wa Wizara ya Fedha, zimeanza kuivuruga benki hiyo.
Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka ndani ya benki hiyo zinaonyesha kuwa, tayari bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo kwa kushirikiana na menejimenti, imeunda kamati maalumu ya kuwasaka watu wanaoaminika kusambaza taarifa hizo.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, tayari maofisa wapatao watano wa benki hiyo wamepewa likizo ya lazima ili kupisha uchunguzi ambao umeanza kufanywa.
Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka ndani ya bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo, zilibainisha kuwa, miongoni mwa watu waliopewa likizo hiyo ya lazima ni pamoja na Ofisa Uajiri na Utawala, Danny Maganga, Mkuu wa Huduma za Bodi, Rita Akena na Mkuu wa Maridhiano, Joseph Salala.
Vyanzo hivyo vya uhakika vililidokeza gazeti hili kuwa katika likizo hiyo ya lazima, maofisa hao walitakiwa kubakia katika maeneo yao ya kazi pasipo kusafiri bila ruhusa ya mwenyekiti wa bodi wa benki hiyo.
Kwa mujibu wa barua za kusimamishwa kazi kwa maofisa hao wa juu wa TPB, uamuzi huo umeleezwa waziwazi kuhusishwa na taarifa hizo katika mtandao wa intaneti zilizochapwa katika webu maarufu ya Jambo Forum.
Barua hizo za kusimamishwa kazi zilizosainiwa na Mtendaji Mkuu wake Alphonce Kihwele, ambazo gazeti hili limeziona, zinaeleza kuwa, taarifa ambazo zimewekwa katika mtandao huo ni nyeti na ambazo kimsingi zinapaswa kujulikana kwa mameneja peke yake na hivyo kusababisha ionekane dhahiri kuwa, watu waliozituma kwenye mtandao huo wanatoka ndani ya menejimenti ya TPB na si vinginevyo.
Kama unavyojua, kuvujisha taarifa za siri kwa watu wasiohusika pasipo kibali cha mamlaka ni kosa la kimaadili, ambalo adhabu zake ziko chini ya taratibu za Sheria ya Maadili ya Kazi Kifungu cha 48 (1) cha Sheria inayohusu benki na taasisi za fedha ya mwaka 2006, na kifungu cha 13 (c) ya Sheria ya Benki ya Posta ya mwaka 1991, inasomeka moja kati ya barua ya watu waliopewa likizo ya lazima.
Tanzania Daima ilipozungumza na Kihwele ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa TPB, kwanza alianza kwa kueleza kuwa taarifa zilizowekwa katika mtandao huo wa intaneti anazifahamu zilikuwa ni za kupotosha.
Mambo yanayotokea kwenye mtandao si ya kweli, na sasa tunafanya uchunguzi kubaini ni nani aliyesambaza tuhuma hizo, alisema.
Mbali ya hilo, Kihwele pia alikanusha tuhuma zinazomhusisha yeye kula njama za kujiongezea mkataba wa kazi katika benki hiyo hata baada ya muda wake kumalizika.
Suala la mimi kuteuliwa na kuongezwa muda lipo chini ya bodi, mimi sina uwezo wa kujiteua, mimi nateuliwa na bodi, nitakaa saa ngapi na bodi? alihoji Kihwele akionyesha dhahiri kutokubaliana na tuhuma hizo.
Hata hivyo, mtendaji mkuu huyo aliahidi kuzungumza na gazeti hili siku ya Ijumaa ya wiki hii ili aweze kutoa ufafanuzi kwa madai kuwa, siku ambayo alifuatwa alikuwa na kazi nyingi.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma kwamba kumekuwa na kuchezewa kwa mahesabu ya benki hiyo kwa lengo la kuonyesha kuwa kuna faida kubwa inayopatikana katika operesheni zake, Kihwele alihamaki na ghafla akasimama kutoka katika kiti chake.
Wewe kama unalipwa kwa kuandika habari hiyo proceed (endelea). Inawezekana umetumwa. Kuna mtu ambaye amekutuma. Nani kakutuma? alisema kwa ukali na kisha akatoka nje ya chumba maalumu cha mahojiano, akibamiza mlango na kumuacha mwandishi wa habari hizi ndani.
Taarifa zilizosambazwa kwenye mtandao, zinamtuhumu Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta, kwa kughushi barua ya Bodi ya TPB ili aongezewe mkataba mwingine wa miaka mitatu, baada ya kipindi chake cha tatu cha mkataba kuishia Novemba 25 mwaka 2006.
Katika hili inadaiwa kuwa, Novemba 20, 2006 kilipofanyika kikao cha bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo, kikao kilidai kutaarifiwa juu ya mtendaji huyo kuongezewa mkataba mwingine wa miaka mitatu na Wizara ya Fedha iliyodai kupokea pendekezo kutoka kwenye bodi, kitu ambacho bodi inadai kuwa hakuna kikao kilichokutana kumpendekeza.
Aidha, waraka huo unadai kuwa, uchunguzi uliofanyika ulionyesha kuwa, uhalifu huo ulifanywa na viongozi wa juu wa bodi, lengo likiwa ni kumbakisha Kihwele katika mamlaka yake kwa sababu ambazo hazijawekwa bayana.
Mbali na tuhuma hizo, pia imeelezwa kuwa, ufisadi mwingine uliofanyika ni ule wa mtendaji huyo kuwalazimisha watengeneza mahesabu, idara ya fedha kuhakikisha wanatoa hesabu zinazoonyesha faida, kinyume cha ukweli.
Katika hili, ambalo ndilo lililomfanya ahamaki hata kukataa kuendelea na mahojiano, inaelezwa katika tuhuma hizo kwamba, makosa hayo ya kukusudia katika mahesabu ya TPB yalishtukiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Aidha, tuhuma nyingine zilizomo kwenye waraka huo ni zile zinazoeleza kuwa Kihwele ameandaa timu yake ya mtandao inayowahusisha baadhi ya wafanyakazi ndani ya benki hiyo, ili kuweza kufanikisha vitendo visivyozingatia misingi ya utendaji unaofaa wa kazi.
Alisema katika kufanikisha hilo, baadhi ya watu walio katika mtandao huo wamekuwa wakipewa zawadi ya kupandishwa vyeo.
Moja kati ya tuhuma nzito zinazodaiwa kuendeshwa na kundi la mtandao huo ndani ya benki hiyo inayomilikiwa na serikali, ni pamoja na ile ya kuiingiza benki katika mikataba mibovu, ikiwemo ule wa uwekaji na uendeshaji wa mashine za kutolea fedha ATMs, ambazo zinadaiwa kuigharimu benki hiyo mamilioni ya fedha yasiyostahili.
Mkataba huo ambao TPB imeingia na benki nyingine nchini (jina tunalo) unaelezwa katika waraka huo kuwa ni kielelezo tosha cha mikataba ya kifisadi yenye nia ya kuliangamiza shirika, ambapo benki imekuwa ikilipa mamilioni ya pesa bila kupata faida yoyote.
Inadaiwa kuwa moja kati ya makubaliano ya mkataba huo, TPB itailipa taasisi hiyo fedha na kampuni inayosambaza ATM ya TANPAY kiasi cha sh 12,000 kwa kila kadi inayotolewa kwa mwaka wa kwanza na kwa mwaka wa pili zitalipwa sh 8,800 na mwaka watatu zitalipwa sh 8,600 kwa kadi hiyo ambayo uhai wake unadaiwa kuwa ni wa miaka mitatu.
Waraka huo umezidi kufafanua kuwa, kadi ya Uhuru inauzwa kwa jumla ya sh 29,400, hivyo TPB huwatoza wateja wake sh 15,000 wanapojiunga na Uhuru kadi, ambako sh 12,000 zinapelekwa kwa taasisi mbili inazoshirikiana nazo katika biashara hiyo.
Aidha, inadaiwa kuwa mteja anayetumia kadi hiyo hutozwa sh 350 kila anapoitumia kuchukua fedha, ambapo kati ya pesa hizo sh 300 hupelekwa FBME/TANPAY, utata unaibuka juu ya chanzo cha mapato ya TPB kulipa gharama za mwaka wa pili ambazo ni sh 8,800 na mwaka wa tatu sh 8,600, ambapo TPB inadai haina chanzo cha kupata fedha hizo, hali iliyosababisha wabia wa TPB kufanikiwa kujipatia sh milioni 200 kutoka katika benki hiyo.
Katika waraka huo wenye kurasa tisa, pia ufisadi mwingine uliolalamikiwa ni ule wa kuwepo utaratibu wa kulipa watu binafsi au makampuni ya wanaodaiwa kuwa ni ya marafiki, pasipo kufuata taratibu zozote za fedha.
Waraka huo pia unahusisha madai kwamba kampuni yenye uhusiano ama wa kifamilia au kirafiki na mmoja wa watendaji wa juu wa benki hiyo ilipewa zabuni ya kukarabati kaunta za benki ya TPB, tawi la Ubungo, ambapo inadaiwa kuwa sh milioni 800 zilitumika kwa ajili ya ukarabati huo pamoja na malipo mengine kwa Kampuni ya Patty Plan inayodaiwa kumilikiwa na mtoto wa rafiki wa mkuu mmoja wa benki hiyo.
Utata mwingine umeibuka katika kesi inayodaiwa kuwa ni ya kupanga ikimhusisha ofisa mstaafu wa jeshi aliyeishitaki TPB, ambako katika kesi hiyo, walitumiwa mawakili wa nje kuitetea benki hiyo huku mlalamikaji akitetewa na kampuni ya uwakili inayomilikiwa na mmoja wa watendaji wa benki hiyo.
Aidha, imedaiwa kuwa, kuna baadhi ya kampuni ambazo zimekuwa zikitumiwa kuchota mamilioni ya fedha ndani ya benki hiyo kwa njia ya kukopeshwa, ambazo zilikopa kiasi cha sh bilioni 1.6.
Na kabla hazijalipa deni hilo, zikaomba kuongezewa sh bil. 2 ili ziweze kufufua kampuni zao, lakini pia waweze kulipa mikopo.
Aidha, inadaiwa kuwa baadhi ya watendaji walipinga pendekezo hilo, ikiwa ni juhudi za kuwafanya warejeshe mkopo wa awali baada ya kugundua kuwa hakuna juhudi zinazofanywa ili mkopo huo urejeshwe.