Jifunze namna ya Kuandika Mkataba Kisheria Unapouza au Kununua Kitu

Jifunze namna ya Kuandika Mkataba Kisheria Unapouza au Kununua Kitu

figganigga

JF-Expert Member
Joined
Oct 17, 2010
Posts
25,724
Reaction score
55,906
Katika shughuli zetu za kuuza na kununua ambazo tunazifanya kila siku mikataba ya maandishi ni jambo ambalo wengi tunakutana nalo. Mikataba hii iwe rasmi au isiwe rasmi suala la msingi ni kuwa huwa tunaifanya. Aidha wakati mwingine si wote wenye kuhusisha suala la mikataba ya maandishi katika makubaliano yao mbalimbali na hii hutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kuaminiana. Kuhusu kuaminiana niseme jambo moja tu kuwa suala la mikataba ni muhimu sana hata kana mwenzako unamuamini kwa kiwango cha juu kabisa( highest degree of trust).

Nathubutu kusema kuwa hata awe mzazi wako kama kuna jambo la msingi mmelifanya ni vema kukawapo mkataba wa maandishi. Nasema hivi kwakuwa kwa uzoefu wangu wa mambo haya mara nyingi mgogoro hautokani na waliouziana au kukubaliana isipokuwa mgogoro unakuja kuanzishwa na walio nyuma ya hao.

Kwa mfano baba anaweza kumpa mwanae kiwanja na wasifanye mkataba wowote wa maandishi kwa kuwa wanaaminiana. Hiyo ikaenda kwa miaka kadhaa ambapo baba akawa amefariki. Baaada ya hapo anaibuka mtu anasema mimi ni mtoto wa marehemu kwa hiyo nahitaji kiasi kadhaa kutoka mali hii.

Hapa mgogoro si kati ya baba na mwana tena isipokuwa ni kati ya mwana na mtu mwingine. Kama huna mkataba wowote wa maandishi mpaka kesi hii kuisha waweza kuwa umepoteza kila kitu. Huu ni mfano tu katika kusisitiza kuwa mtu asiseme mi na fulani tunaaminiana. Mgogoro sio lazima utokane na nyie wawili isipokuwa walio nyuma yenu waweza kuanzisha mgogoro.

MADHARA YA KUTOFANYA MKATABA WA KISHERIA
Ni vema sana kujihadhari kwakuwa ukisikia neno mgogoro ujue kuna mambo makubwa mawili. Kwanza gharama kubwa ni uwezekano wa kupoteza kabisa ile mali na haijalishi iwe uliinunua au ulipewa isipokuwa tu ukishakuwa na mgogoro upo katika hatari hiyo. Pia gharama ya pesa kama kuwalipa wanasheria, gharama za uendeshaji kesi, nauli na matumizi mengineyo ambayo hujitokeza bila hata kutarajia. Pili kuna gharama ya muda .

Hii huhusisha kushinda mahakamani kila siku na wote mwajua mahakama zetu zilivyo, kushinda vituo vya polisi huku shughuli zako za msingi za kila siku zikisimama. Pia hapa kuna muda wa kusubiri hukumu ambapo kesi yaweza kukaa mahakamani hata miaka sita . Hakika unakuwa umesurubika(suffer) na umepoteza mambo mengi katika kushughulikia jambo hili.

USHAURI
Ushauri wa kawaida tu kwa hili ni kuwa na utamaduni wa kuweka katika maandishi kila makubaliano na hii iwe kwa watu wote mnayeaminiana sana au msiyeaminiana. Fanya hili kuwa utamaduni wako kwa kuweka kila muamala wako katika maandishi suala la kuaminiani lisiwe hoja tena kwakuwa mgogoro hautakuwa kati yako na yeye isipokuwa unaweza kuwa kati ya mtu wa nyuma yake na wewe au mtu wa nyuma yako na yeye. Nitatoa mfano mwingine halisi ambapo mfano huu ni kesi ipo mahakamani hadi leo.
Mwaka 2010 mwezi wa saba mtu mmoja alimuuzia rafiki yake gari aina ya land cruiser akiwa anatafuta fedha kwa ajili ya safari yake ya uingereza baada ya kupata kazi huko. Wakauziana na kwakuwa waliaminiana sana hawakuandikishana popote.

Mwaka mmoja na nusu baadae gari hiyo ikakamatwa maeneo ya Sinza na polisi kwasababu kuwa mwaka 2009 Disemba iliwagonga watu wawili na kuuwa mmoja maeneo ya tabata na kukimbia. Mnunuzi alijitetea kwa urahisi tu kuwa gari amelipata 2010 July kwa hiyo hawezi kuwa anahusika na lolote kabla ya muda huo.

Utetezi wake ulikubaliwa isipokuwa tu alitakiwa atihibitishe kwa kuonesha mkataba halali wa mauziano ambao utaonesha kuwa ameanza kumiliki gari hilo baada ya ajali. Ilikuwa vigumu kwake na hilo likamwingiza moja kwa moja katika kesi hiyo na mpaka naandika makala haya amesota na kesi hiyo kwa miaka minne sasa na haijajulikana inaisha lini ambapo kwa mtazamo wa kitaalam kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana na hatia na kwenda jela.Kwa hiyo utaona hapa kuwa kufanya maandiko ya kisheria katika kila muamala si muhimu tu katika kudhulumiana bali pia hata mambo mengine kama haya ambayo yanaweza kujitokeza bila kutarajia.

JE, KILA MAANDISHI NI MKATABA?
Aidha uandishi mzuri wa mkataba wa kisheria hupelekea mkataba wenye hadhi na mkataba wenye hadhi ndio mkataba halali ambao hukubalika kisheria na pia huweza kutumika kama ushahidi endapo kuna tatizo. Yawezekana unao mkataba lakini hauna hadhi kisheria na likijitokeza jambo mkataba wako hautakubalika. Si kila maandishi ni mkataba isipokuwa mkataba huwa na vitu maalum vya kisheria ambavyo huufanya kukubalika na kutambuliwa. Haya hapa ndio mambo ya msingi ambayo hutakiwa kuwa ndani ya mkataba.

MKATABA MZURI HUWA NA HAYA:
( a ) Lazima uwe na majina ya wahusika ambayo yatakuwa yameandikwa kwa urefu na kwa kueleweka.Mfano jina liwe Paschal Mayenge Archard. Epuka kuandika vifupi mfano P.M. Archard. Jina linatakiwa liwe katika ukamilifu wake na hasa pawe na majina matatu kamili. Pia majina ya pande zote mbili yaani muuzaji na mnunuzi yatokee hivyohiyvo si tu majina ya upande mmoja. Yawezekana mkataba mwingine unahusisha watu wengi zaidi pia ni muhimu majina matatu ya kila mmoja yaonekane hata kama wako ishirini.

( b ) Katika majina hayo hadhi ya kila mmoja iainishwe mbele ya jina lake. Mfano kama ni muuzaji au mnunuzi mbele iandikwe kuwa huyu ni muuzaji na huyu ni mnunuzi. Halikadhalika kama ni mkopaji, mkopeshwaji, mtoa zawadi mpokea zawadi viainishwe.

( c ) Bei au gharama halisi ya mauziano ioneshwe. Iandikwe kwa tarakimu yaani namba mfano 1,000,000/= na kwa maneno katika mabano ( Milioni moja tu).Ni muhimu yote mawili yaonekane , hii huondoa utata.Tarehe ya mkataba ioneshwe sambamba na maelezo kama fedha imelipwa yote au kiasi.

( d ) Kama kuna kiasi kilichobaki kianishwe kwa tarakimu na pia kwa maneno kama nilivyoonesha hapo juu. Muda wa kulipa kilichobaki nao uainishwe ikiwa ni pamoja na hatua za kuchukua ikiwa muda uliowekwa utapita. Mkataba lazima uoneshe muda ukipita nini kifanyike mfano ikifika tarehe 7. 12. 2015 saa kumi jioni kiasi cha pesa iliyobaki hakijalipwa basi mali itamrudia mwenye nayo na mnunuzi hatakuwa na deni lolote dhidi ya muuzaji, au itahesabika kuwa mkataba umevunjika na mnunuzi atatakiwa kumlipa fidia ya kiasi fulani muuzaji kwa kuvunja mkataba.

( e ) Mashahidi ni muhimu kila upande. Kila upande hata ukiwa na shahidi mmoja wala si mbaya. Shahidi awe mtu wa kuaminika , mtu mzima na mwenye akili timamu. Wataandika majina yao matatu kwa urefu kama yalivyo ya wahusika na pia wataweka sahihi zao huku ikioneshwa shahidi yupi wa upande upi na yupi wa upande upi. Wakili ni mtu muhimu sana kwa wakati huu kwani wakili anaweza kuwa shahidi pekee bila kuwapo shahidi mwingine yeyote.
Wakili anakuwa shahidi wa wote wawili na panakuwa hapahitajiki mwingine yeyote.Pia wakili ni shahidi wa kuaminika zaidi na anaaminiwa na kila mamlaka ikiwemo mahakama na hivyo uwepo wake katika mkataba ni ulinzi tosha kwa mkataba wako.

( f ) Mali inayouzwa au iliyohusishwa kwenye mkataba ichambuliwe vyema. Kama ni kiwanja au nyumba ielezwe mtaa, kata, tarafa kitongoji,mkoa,plot namba kama ipo, urefu, upana, ikiwezekana jirani wa kushoto na kulia.au magharibi, mashariki, na kama ni gari, pikipiki maelezo yote yaliyo kwenye kadi yaingie katika mkataba ili kutambua kwa undani mali yenyewe.

( g ) Anuani za muuzaji au mnunuzi ziwepo ikiwa ni pamoja na namba ya simu. Hili la namba ya simu ni muhimu sana kwasasa kutokana na msaada mkubwa wa mawasiliano haya endapo mtu atahitajika.

( h ) Picha ndogo yenye kuonesha taswira ya mtu kwa ukamilifu (passport size) ni muhimu sana na ibandikwe mbele ya jina la mtu. Si muhimu sana kwa mashahidi lakini kwa wahusika wenyewe ni muhimu sana.

( I ) Alama ya dole gumba mbele ya jina nayo ni muhimu sana. Hii ni kutokama na alama hii kutoweza kwa namna yoyote kuingiliwa au kughushiwa.Tia dole kwenye kablasha ya muhuri na weka dole gumba mbele ya kila jina. Hii pia si lazima kwa mashahidi.

( j ) Kama ni kiwanja au nyumba ni muhimu mkataba uoneshe kama kimelipiwa kodi ya ardhi ( Land rent) na kama hakijalipiwa mkataba ueleze nani atalipa kodi hiyo kati ya anayenunua au anayeuza.

( k ) Pia ni muhimu sana mkataba uoneshe iwapo mgogoro wowote utatokea kuhusiana na mkataba huo nini wahusika wafanye, mfano endapo mgogoro utatokea kuhusiana na mkataba huu mahakama ya Tanzania yenye mamlaka ndio itahusika na utatuzi wa mgogoro. Sambamba na hilo mkataba uweke wajibu kwa muuzaji kuwa tayari kumpa ushirikiano mnunuzi iwapo mali aliyomuuzia itaonekana kuwa na mgogoro mbeleni mfano muuzaji atampa ushirikiano mnunuzi endapo kutatokea mgogoro wowote kuhusiana na mauziano haya.

Kwa ufupi hayo ni baadhi tu ya mambo ya msingi katika kukufanya kuwa salama katika mikataba. Nirudie tu kusema kuwa si kila maandishi uliyoandika na kuhifadhi nyumbani kwako ni mkataba jitahidi kuwa na mkataba wa kisheria.

Mwandishi wa makala haya ni Mwanasheria na Mshauri wa sheria kupitia gazeti la serikali Habari Leo kila jumanne, gazeti Jamhuri kila jumanne na Nipashe jumatano.

bashiryakub@ymail.com
 
Mauziano ya viwanja/mashamba yanayothibitishwa na mjumbe wa Tawi wa CCM au Serikali ya Mtaa ni mkataba unaokubalika kisheria.
 
Mimi nina swali, nimenunua kiwanja karibia hayo yote nimefanya isipokuwa hapakuwa na mwanasheria na alama ya dole gumba je vp mkataba wangu utatambuliwa mbele ya sheria?
 
Mada nzuri sana hii. Nimeisoma katika wakati mwafaka kuwa wiki ijayo ninanunua nyumba kwa mtu.
 
Mada nzuri sana hii. Nimeisoma katika wakati mwafaka kuwa wiki ijayo ninanunua nyumba kwa mtu
Mimi nimesha bugi. Nilimuuzia dada yangu kiwanja pesa ajamalizia yapata mwaka sasa. Atuja andikishana popote nawaza kumrudishi pesa yake ya awali .yaaan mali bila daftari.
 
mada nzuri sana mkuu tumejifunza sana .
 
Kwenu figganigga na wanasheria wengine,

Kwanza tunashukuru kwa elimu nzuri mnayotoa khs mambo ya kisheria.
Naomba kuuliza mambo yafuatayo:

1. Mikataba ya mauziano ya viwanja visivyopimwa iliyofanyika kwenye ofisi za serikali za mitaa bila kuwepo mwanasheria ina thamani gani kwenye ushahidi (evidential value) mahakamani kwenye utatuzi wa migogoro ya ardhi na kudai fidia?

2. Je, kwa kawaida mahakama ina-enforce ulipwaji wa kiasi chochote cha fidia ya kuvunja mkataba kilichokubaliwa kwenye mkataba wa mauziano?
Mfano, katika mkataba wa mauziano ya kiwanja muuzaji na mnunuzi wamekubaliana hv:

A). KWAMBA, Muuzaji ana nia ya kuuza kiwanja hicho na Mnunuzi ana nia ya kununua kiwanja hicho kwa TZS 10,000,000/= (Shilingi za Kitanzania Milioni Kumi tu).

B). KWAMBA, Mnunuzi atamlipa Muuzaji fedha za manunuzi ya kiwanja hicho kwa awamu mbili; yaani awamu ya kwanza leo tarehe 15 Mwezi Januari 2015 mnunuzi amelipa na muuzaji amepokea TZS 5,000,000/= (Shilingi za Kitanzania Milioni Tano tu) na awamu ya pili kabla ya tarehe 15 Mwezi Machi 2015 mnunuzi atalipa kiasi kilichobaki cha TZS 5,000,000/= (Shilingi za Kitanzania Milioni Tano tu).


C). KWAMBA, kabla ya tarehe 15 Mwezi Machi 2015, muuzaji hatakuwa na haki wala mamlaka ya kuuza kiwanja hicho kwa mtu mwingine yeyote.

D). KWAMBA, iwapo muuzaji atavunja kifungu "C" hapo juu, muuzaji atatakiwa kumrejeshea mnunuzi fedha zote ambazo mnunuzi amemlipa muuzaji kwenye awamu ya kwanza, yaani TZS 5,000,000/= (Shilingi za Kitanzania Milioni Tano tu) na pia muuzaji atatakiwa kumlipa mnunuzi fidia ya kuvunja mkataba ambayo itakuwa ni MARA 10 (KUMI) ya fedha iliyolipwa kwenye awamu ya kwanza, yaani TZS 50,000,000/= (Shilingi za Kitanzania Milioni Hamsini tu). Muuzaji atatakiwa kurejesha fedha hizo na kulipa fidia hiyo kwa mnunuzi katika kipindi cha siku 7 (saba) tangia alipovunja kifungu hicho "C".

Natanguliza shukrani
 
huo mkataba sio mzuri ni wa kukomoana, tafuta mwanasheria.ushauri kama hakuna mwanasheria wakati wa mauziano toa pesa yote muachane
 
Mauziano ya viwanja/mashamba yanayothibitishwa na mjumbe wa Tawi wa CCM au Serikali ya Mtaa ni mkataba unaokubalika kisheria.
Hawa Watendaji wa Kata au Mwenyekiti serikali za Mitaa etc, hawakubaliki kuthibitisha mauziano ya mashamba/viwanja kwani wamekuwa sehemu ya tatizo. Hawaangalii uhalali wa vitu vinavyouzwa; wao uangalia zaidi kupata mpunga basi.
Kesi nyingi zimewahusisha hawa watu. Mbaya zaidi ni kwamba hawajui sheria zinazohusu mauziano.
Maswala ya kuuziana viwanja na mashamba ni bora zaidi kutumia wakili.
 
Back
Top Bottom