Kama umefika Mwanza, utaona changamoto kubwa ya uchafu, hasa kutokana na wingi wa taka za plastiki na taka nyingine zinazotapakaa katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Mamlaka ya Jiji imeonekana kushindwa kuweka idadi ya kutosha ya mapipa ya taka katika maeneo muhimu, ikiwemo katikati ya jiji na maeneo ya vituo vya daladala, jambo linalochangia wananchi kutupa taka hovyo.
Utaratibu wa kufanya usafi kila mwisho wa mwezi ambao ulikuwa ukisaidia kuboresha mazingira umeishia wapi? Ni kwa nini mamlaka husika imeshindwa kuweka mfumo madhubuti wa ukusanyaji taka, kusimamia sheria za usafi na kuhakikisha mazingira yanatunzwa?
Tunaiomba serikali na viongozi wa Jiji la Mwanza kuchukua hatua za haraka kudhibiti tatizo hili, kulinda mandhari ya jiji na kuhifadhi mazingira ya Ziwa Victoria.