View attachment 1882821
[emoji2398]
Wikipedia
Hivi karibuni kulikuwa na tukio lililotikisa ulimwengu wa uwekezaji haswa kwenye mawasiliano: Ethiopia ilikuwa inafungua soko lake la watu milioni 112 hivi, lililokuwa limeshikiliwa na kampuni moja ya umma,
Ethio Telecom—ifananishe na TTCL kwa Tanzania. Utoaji wa leseni ulifanyika kwa njia ya mnada, kukawa na makundi mawili: kundi la
MTN lililoahidi dola (Marekani) milioni 600 na lingine la
Vodafone (wakiongozwa na
Safaricom ya Kenya) lililoahidi dola (Marekani) milioni 850.
Kundi la
MTN lilikuwa na uungwaji mkono na China kupitia
Belt and Road Fund. Mfuko huu ulipanga kuipatia fedha
MTN ili iweze kuwekeza Ethiopia. China ina mkakati maridhawa sana wa kujitanua kiuchumi, kisiasa, na kijamii kupitia mradi wake wa
Belt and Road ambao umekuwa ukipigwa vita sana na mataifa ya magharibi, yakiuona kama hatua ya kuondoa ushawishi wao huku China isiyofuata demokrasia na haki za binadamu ikisambaza ujumbe “hatari” kwa nchi maskini. Ni kweli kwa kiasi fulani, China haijali kinachotokea kwenye nchi itakayowekeza; huwa inasema “haiingilii masuala ya ndani”; inachotaka ni biashara tu. Ethiopia ni moja ya nchi zilizo kwenye mpango wa
Belt and Road, pamoja na Kenya (tumeona ujenzi wa reli ghali sana), Tanzania (hapa kuna reli na bandari ya Bagamoyo), na nchi nyingine karibu 130 duniani. Kuwekeza kwenye mawasiliano Ethiopia ilikuwa ni hatua muhimu sana ya mpango huo kwani ingeipatia kampuni ya
Huawei nafasi ya kusambaza teknolojia ya
5G ambayo imekuwa gumzo ulimwenguni hivi karibuni.
Kundi la Vodafone, ambalo linajulikana kwa jina la
Global Partnership for Ethiopia, linajumuisha kampuni za
Vodafone, Safaricom, Vodacom Group, Sumitomo Corporation, CDC Group (inamilikiwa na serikali ya Uingereza), na
US Development Finance Corporation (inamilikiwa na serikali ya Marekani). Kundi hili likashinda mapema kabisa hata kabla ya siku ya mnada kwa kuwa lilikadiriwa kuwa na dau la juu zaidi ambalo
MTN isingeweza kupiku. Wachambuzi wa mambo wanasema ilikuwa si kuhusu uwekezaji, ilikuwa kuizuia China. Zaidi ya hapo, huenda Ethiopia inachagiza ushawishi wa Marekani kwenye usuluishi wa mgogoro wake na Misri kuhusu mto Nile. Muungano wa
Global Partnership for Ethiopia unategemea kutengeneza ajira milioni 1.5 huku ukiwekeza dola (Marekani) bilioni 8.5 kwa kipindi cha miaka 10.
Pamoja na nafasi kuwa wazi tena, ambapo Ethiopia itauza leseni nyingine, huenda
MTN wasirudi huku wakisingizia vita ya Ethiopia kaskazini na mgogoro wa mto Nile. Zaidi, serikali ya Ethiopia itauza 40% ya hisa kwenye kampuni ya kitaifa ya
Ethio Telecom sambamba na utoaji wa leseni mpya na huenda ikaondoa “utamu” wa soko kama ilivyotarajiwa. Kampuni nyingine zinazoangaliwa kwenye uombaji wa leseni ya pili ni
Orange na
Etisalat. Marekani na washirika wake walifanikiwa kuigusa China katika harakati za kujitanua. Lakini China ina nafasi kubwa ya kufanikisha mpango wake ambapo miradi ya mabilioni ya dola inaendelea kote duniani wakati pesa zikitoka China kwa upande mmoja huku ikizikopesha nchi washirika kwa upande mwingine.
Global Partnership for Ethiopia welcomes licence award to operate telecom services in Ethiopia
Kenya's Safaricom, partners aim to start Ethiopia operations in 2022
Nawajibika kwa makosa ya kiuandishi.