SoC02 Jinsi nilivyoepuka kukeketwa

SoC02 Jinsi nilivyoepuka kukeketwa

Stories of Change - 2022 Competition

hanayna

Member
Joined
Jul 29, 2022
Posts
5
Reaction score
1
Habari zenu wote natumai mpo salama.
Mimi ni binti nileyenusurika kupata tohara (kukeketwa), katika kijiji chetu au kabila letu kuna utamaduni wa mtoto wa kike(msichana) kukeketwa, wao wanamtazamo kuwa mtoto wa kike(msichana) akishapata tohara anakuwa ni msafi , analeta hadhi katika ukoo, anahifadhi utamaduni na anakubalika katika jamii.

Hivyo basi katika kijiji chetu binti anapofikisha umri wa miaka 12 hadi 14 analazimika kupata tohara(kukeketwa) ,nilipofikia umri wa miaka 7 mimi na familia yangu tulilazimika kuhamia mjini kulingana na pesa tukiyokuwa nayo baada ya kuuza mifugo,

Wazazi wakaamua wakafanye biashara mjini ,baba alinishika mkono na kuniambia mwanangu wewe na mama yako sasa tunaenda mjini tukaanze kufanya biashara ya nafaka maana nasikia inalipa sana huko na pindi utakapofikisha umri wa miaka 12 utarudi kijijini kufanyiwa tohara , basi nilivyosikia tunaenda mjini nilifurahi sana na kumuambia baba sawa nitarudi kufanyiwa tohara

Tulivyofika mjini niliona watoto wa kike wakienda shule na sisi kijijini kwetu watoto wa kiume pekee ndio wanaoenda shule nikatamani na mimi siku moja niende shule , nikaweza kumwambia baba na mimi naomba unipeleke shule kama hawa mabinti wa mjini wanavyoenda baba alitabasamu kisha akasema sawa mwanangu nitakupeleka , nilifurahi sana kusikia hivyo basi siku ya kwenda shule ikafika nikapelekwa katika shule ya msingi ili kupata elimu ya msingi


Nilivyofika darasa la 3 siku moja katika shule yetu tukabahatika kutembelewa na taasisi moja inayopinga ukeketaji na unyanyasaji kwa wanawake basi tukakalishwa ndani ya jengo moja kubwa wanafunzi wote wa kike kuanzia darasa la awali mpaka darasa la 7 tukapewa mafunzo mbalimbali yanayohusu utu wa binadamu pia wakaeleza madhara juu ya ukeketaji kwa mwanamke

Tukaambiwa tusiweze kukubali kufanyiwa vitendo vya ukeketaji ni hatari sana kwetu kwani wanatumia vifaa visivyokuwa na usalama katika afya ya mwanadamu hivyi vifaa hivyo kuchangiwa na zaidi ya watu wawili na kupata magonjwa mbalimbali ya kudumu kama matatizo ya kibofu cha mkojo au kutokwa na hedhi zisizokuwa za kawaida
81754AE5-5A49-4D14-A7C6-5BE060FC8623.jpeg

Picha hii kwa udhamini wa UNICEF.

Pia husababisha umwagaji mwingi wa damu ambao unaweza kufanya kupoteza maisha na wao wanasema ukeketaji ni moja ya mahitaji ya kila msichana, mimi nilikuwa ninamtazamo kuwa kufanyiwa tohara kwa mwanamke ni jambo la kawaida sana sababu nilishazoea kuona ukifanyiwa tohara unapewa mifugo kama mbuzi ,ng’ombe au kondoo alafu hamna madhara yoyote yatakayoweza kutokea, basi hiyo ndio siku yangu ya kwanza kupata elimu hiyo,

Hivyo nilivyofika nyumbani nikaweza kuwaelezea wazazi kila kitu kuhusiana na elimu niliyoipata shuleni juu ya madhara ya ukeketaji kwa mtoto wa kike, wazazi waliweza kunielewa kisha baba akasema hata mimi mara nyingi nikiwa kwenye shughuli zangu nasikia kwenye redio wakitangaza juu ya upingaji wa ndoa za utotoni na ukeketaji eti kuna madhara makubwa sana hutokea pindi mtoto anapofanyiwa hivyo ,basi nilivyosikia hivyo nilifurahi na kusema kumbe wazazi wangu pia wanajua juu ya madhara ya ukeketaji mimi tu ndio nilikuwa sijui
0FC1083E-B6A2-4CB8-B345-F6B3E1E37C71.jpeg
picha hii kwa udhamini wa unicef.

Basi miaka ikaenda nikahitimu darasa la saba nikiwa nina miaka 14, Sisi kama familia tukaenda kuwasalimia babu, bibi na ndugu zetu wengine kijijini vile tulivyofika wakaanza kutushangaa sana kisha wakaanza kuwaambia wazazi wangu kwa ukali ni kwanini binti yenu mmemchelewesha kumleta kufanyiwa tohara ( ukeketaji) hadi ameaanza kukua

Hivyo basi niliweza kuwaangalia wale wazee kwa hasira kisha baba yangu akawaambia wale wazee tutaongea baadae kuhusu hilo swala kisha wakaweza kuingia ndani na kusalimia watu wengine , bibi na babu walifurahi sana walivyotuona kisha wakasema Oh! mjukuu wetu umekuwa sana sasa unatakiwa ufanyiwe tohara na utafutiwe mume akuoe nilimtizama bibi kisha nikacheka nikamwambia tutaongea hili swala baadae vizuri

Basi nikaenda kuwasalimia mabinti wenzangu niliyokuwa naishi nao jirani ila baadhi yao walikuwa wameshaolewa, wakaanza kunishangaa huku wakisema ndio umekuja kufanyiwa tohara na umeshapata mchumba huko mjini , nikawajibu hapana mimi na wazazi wangu tumekuja huku kijijini kuwajulieni hali na kutoa elimu juu ya mambo mbalimbali yanayohusu jamii, basi wakafurahi kuniona tukacheza na kufurahi kwa pamoja basi siku ikapita,

Asubuhi na mapema baba akawahi kwa mwenyekiti wa kijiji kumuomba kuitisha mkutano kwa wanakijiji wote, hivyo baba alikuwa kashamweleza mwenyekiti juu ya dhumuni la mkutano huo basi majira ya saa 7 adhuhuri mwenyekiti aliweza kupiga ngoma ya kijiji na kuwajulisha wanakijiji wote juu ya mkutano saa 10 alasiri , wanakijiji waliweza kuitikia kwa wingi kwa minajili ya kuudhuria mkutano,

Baba yangu aliweza kufika pale na kuongea na wanakijiji juu ya madhara mbalimbali ya ndoa za utotoni, haki ya mwanamke, athari za ukeketaji kwa mtoto wa kike na kuwapeleka shule watoto wote wa kike na kiume baba hakuweza kuwa mshauri pekee katika kikao kile bali aliweza kuwasiliana na taasisi zinazopinga ukeketaji na ukatiri kwa wanawake huko mjini pia waliweza kuja kutoa ushauri kwenye mkutano huo , ila kuna baadhi ya watu waliweza kuingiwa na elimu hiyo iliyotolewa na wengine walisema hao watu wa mjini wanataka kutuondolea mila na desturi zetu haiwezekani , pia mimi na mama yangu tuliweza kukaa na kina mama na watoto wa kike ili kuwapa elimu juu ya madhara ya ukeketaji,
4F85C4B3-8A63-4EA6-B397-389734F0C8EA.jpeg
picha hii ni kwa udhamini wa startv.co.tz.

Ndoa za utotoni na umuhimu wa elimu kwa mtoto , kwa upande wetu wengi waliweza kuelewa juu ya elimu hiyo ila wengi wao walikuwa na hofu waume zao na watoto wa kike wanahofu kwa baba zao, tukawaeleza waume zenu na baba zenu wako pia wanapata elimu hii hii kama tunayowapa ninyi basi wakafurahi , pindi kikao cha kijiji kilivyoisha kuna baadhi ya watu waliweza kusema hao ni wapotoshaji wanataka mabinti zetu wasipate zawadi wakati wakufanyiwa tohara(kukeketwa) na wasiweze kuwa wasafi maana usipofanyiwa tohara wewe ni mchafu,

Pia wengine waliweza kujua ukeketaji ni uzalilishaji na kumnyima mwanamke haki zake , basi mwezi ulivyoisha tukarudi mjini niliweza kufaulu mtihani wa darasa la saba na kuweza kujiunga na elimu ya sekondari , nilipokuwa sekondari nilipenda sana kuudhulia semina zinazotoa elimu mbalimbali ili nipate kujifunza zaidi na mimi niweze kuwaelimisha watu wengine zaidi, nilipo maliza elimu ya sekondari ya juu nilijiunga na elimu ya chuo kikuu na kuchukua fani ya uhandisi wa kompyuta japo watu wengi waliweza kusema fani kama hii haiwezwi kusomwa na mtoto wa kike ,ila sikuweza kusikiliza maneno ya watu niliendelea na fani yangu ,siku moja nikiwa bado niko chuo nilikuwa nimejitunzia hela kidogo nikapata wazo la kwenda kijijini kuweza kuwapa elimu zaidi juu ya upotofu mbalimbali waliokuwa nao

Basi nikaenda hadi kijijini peke yangu kwa mara ya kwanza nikakuta ile elimu tulioitoa inafanya kazi kwa kiasi japo kulikuwa na baadhi ya watu walikuwa wanaendelea na tohara kwa wanawake, basi niliwapa wakubwa heshima zao nikawa nawaita vikundi kwa vikundi

Kwa kutumia hekima na busara niliweza kuwaelimisha wazee mbalimbali katika kile kijiji sababu wao ndio wanaosikilizwa sana kwenye familia zao niliweza kuwaambia wapelekeni watoto wenu mashuleni wakapate elimu kwani inamanufaa sana na nimkombozi kwao watoto hawapaswi kukaa tu nyumbani na kwenda kuchunga mifugo pekee au watoto wa kike kuozeshwa wakiwa na umri mdogo nao pia wanapaswa kusikilizwa kama ninyi mnavyo mnavyosikilizwa na wao , au kama wao hawapendi kwenda shule basi wapeni fursa ya kujifunza vitu mbalimbali ili nao waweze pata angalau ujuzi kama kufuma vitambaa, kushona nguo na kutengeneza vitu mbalimbali
A0091232-B242-45C8-B10A-04477922F0D6.jpeg
picha hii ni kwa udhamini wa mtezamedia.wordpress.com.

Basi nikakaa kama siku mbili alafu nikarudi chuoni kwa ajili ya kumalizia mwaka wangu wa mwisho wa masomo ,hatimaye niliweza kuhitimu elimu yangu ya chuo kikuu .Hapo mimi na familia yangu tuliweza kwenda tena kijijini kwa mara nyingine tulivyofika tulikuta kuna mabadiliko makubwa ,wazazi wengi sasa hawafanyi tohara(ukeketaji)kwa mabinti zao na wameweza kuuza baadhi ya mifugo na mali zao baadhi ili kuwasomesha watoto wao, hakika nilipatwa na furaha isiyo na kifani kuona elimu tuliyoitoa mimi na familia yangu inafanya kazi na kufanya watoto kutimiza ndoto zao
4B82B731-01C5-41FA-9750-3DB84552B5CD.jpeg

Picha hii ni kwa hisani ya IPP media

Watu wengi wanaoishi vijijini hawana elimu ya kutosha juu ya madhara ya ukeketaji kwa msichana/mwanamke hawajui kwamba ukeketaji unaadhiri afya ya kimwili na kiakili kwa msichana/mwanamke.
TAFAKALI: Je nisingeweza kwenda mjini ningefanyiwa tohara (ukeketaji)?

RAI YANGU;
watu binafsi, taasisi mbalimbali na serikali wanapaswa kuweza kusambaza elimu sehemu mbalimbali elimu juu ya madhara ya ukeketaji kwa mwanamke au kupitia vyombo vya habari, vipeperushi au kuweza kuwatembelea kuweza kuwaelisha.
HAKIKA NAJIVUNIA KUWA MSICHANA.
 

Attachments

  • 272F940D-69CD-46D0-875D-0BC832A8D48B.jpeg
    272F940D-69CD-46D0-875D-0BC832A8D48B.jpeg
    11 KB · Views: 6
  • 1EDB96B6-C2C4-406B-AC9F-F6113D3193DB.jpeg
    1EDB96B6-C2C4-406B-AC9F-F6113D3193DB.jpeg
    11 KB · Views: 5
Upvote 0
Back
Top Bottom