Hii ni namna moja ya kuboresha barua hiyo. Inaweza isiwe njia bora kabisa, lakini si imeboreka?
Bwana Edward Vermylen
KK A. Zerega’s sons, Inc.
28 Front St.
Brookyln, N.Y. 11201
Bwana Vermylen:
Kampuni yako imekuwa mteja wetu mzuri kwa miaka kumi na nne. Tunafurahia sana biashara yako na tunatamani kukupatia huduma ya haraka na kwa ufanisi kama unavyostahili. Lakini nasikitika kusema kuwa hilo haliwezekani kwa sababu magari yako ya mizigo hutuletea mizigo mikubwa kwa kuchelewa, kama ilivyotokea tarehe 10 mwezi wa kumi na moja. Kwa nini? Kwa sababu wateja wengine huchelewa kuleta mizigo pia. Hilo linasababisha msongamano. Hilo linasababisha magari yako yachelewe kutoka na wakati mwingine mzigo unachelewa kutumwa.
Hilo ni tatizo, lakini linaweza tatuliwa. Iwapo utaleta mzigo asubuhi, magari yako yatakuwa huru kuendelea na kazi, mzigo wako utahudumiwa kwa haraka, na wafanyakazi wetu watarudi nyumbani mapema kufurahia mlo mzuri wa tambi na macaroni mnaotengeneza
Haijalishi mzigo wenu umefika muda gani, tutafanya kila tuwezalo kuuhudumia kwa haraka.
Umetingwa hivyo tafadhali usijihangaishe kujibu ujumbe huu.
Wako muaminifu.
J—B
Meneja,
Barbara Anderson aliyefanya kazi katika benki huko New York, alitaka kuhamia Phoenix, Arizona sababu ya afya ya mwana wake. Kwa kutumia kanuni alizojifunza kwenye kozi yetu, aliandika barua kwa benki kumi na mbili za Phoenix.
Mpendwa:
Uzoefu wangu wa miaka kumi wa kazi ya benki unaweza kuwa na manufaa kwa benki inayokuwa kwa kasi kama yako.
Nimefanya kazi kadhaa za benki na Bankers Trust Company ya New York, na sasa ni meneja wa tawi. Nimepata ujuzi juu ya nyanja zote za benki, uhusiano na wateja, mikopo na uongozi.
Mwezi wa tano nitahamia Phoenix, nina hakika ninaweza kuwa na mchango kwenye faida na ukuaji wako. Nitakuwepo Phoenix juma la kuanzia tarehe tatu mwezi wa nne, nitathamini kupata nafasi ya kukuonyesha jinsi ninavyoweza kuisaidia benki yako kutimiza malengo yake.
Wako muaminifu,
Barbara L. Anderson
Unadhani bibi Anderson alipata majibu yoyote ya barua yake? Benki kumi na moja kati ya kumi na mbili zilimuita kwenye usaili, na ilikuwa uchaguzi wake ni benki gani aende. Kwa nini? Bibi Anderson hakuongelea kile anachotaka bali aliandika ni namna gani atakuwa msaada kwao. Alikazia matakwa yao na si yake.
Maelfu ya maafisa mauzo hutembea wakizunguka leo, wakiwa wamechoka na kukatishwa tama na malipo duni. Kwa nini? Kwa sababu mara zote wanafikiria kile wanachotaka. Hawatambui kuwa mimi na wewe hatuhitaji kununua chochote. Kama tungetaka tungeenda wanakouza kununua. Badala yake, sote, siku zote tunatamani kutatua matatizo yetu. Na kama wauzaji hao wangetuonyesha jinsi gani huduma zao au bidhaa zao zitatusaidia kutatua matatizo yetu, wasingehangaika kutushawishi kununua. Tungenunua wenyewe. Na mteja anapenda kuhisi amenunua mwenyewe kwa kutaka na si kwa kushawishiwa.
Hata hivyo, maafisa mauzo wengi hutumia maisha yao yote bila kuangalia mambo kwa mtazamao wa mteja. Kwa mfano, kwa miaka mingi niliishi Forest Hills, mtaa mdogo katikati ya jiji la New York. Siku moja, nilipokuwa nikiwahi kituo cha treni, nilionana na dalali wa makazi, kazi yake kuuza na kununua nyumba na viwanja kwenye eneo hilo. Alikuwa anaijua Forest Hills vilivyo, hivyo nikamfuata na kumuuliza iwapo ukuta wa nje wa nyumba yangu umewekewa wavu wa chuma au imejengwa kwa vigae vyenye uwazi katikati. Alisema hafahamu na kisha akaniambia mambo ambayo tayari niliyafahamu—kwamba niwapigie simu Forest hills Garden Association. Asubuhi iliyofuata nilipokea barua kutoka kwake. Je, alinipatia taarifa niliyohitaji? Angeweza kuipata ndani ya dakika moja tu kwa kupiga simu lakini hakufanya hivyo. Kwa mara nyingine tena akaniambia nitaweza kupata taarifa hizo kwa kupiga simu, kisha akaomba awe wakala wangu wa bima.
Hakuwa na nia ya kunisaidia. Alikuwa anataka kujisaidia mwenyewe tu.
Bwana J. Howard Lucas wa Birmingham, Alabama, anasimulia jinsi maafisa mauzo wawili kutoka kwenye kampuni moja walivyoshughulika na jambo kama hilo, alisema:
“Miaka kadhaa iliyopita nilikuwa katika sehemu ya uongozi wa kampuni moja ndogo. Jirani yetu kulikuwa na makao makuu ya wilaya ya kampuni kubwa ya bima. Mawakala wake walikuwa wamepewa maeneo, na kampuni yetu walipewa mawakala wawili ambao nitawaita Carl na John.
“Asubuhi moja Carl alifika ofisini kwetu na kusema kuwa kampuni yao imeanzisha sera mpya ya bima ya maisha kwa viongozi wa makampuni, na alifikiri labda tungeweza kupendezwa nayo hivyo atatutaarifu akipata taarifa zaidi.
Siku hiyohiyo, tulikutana na john njiani tulipokuwa tukitoka kwenye mapumziko ya kahawa, alisema kwa sauti kubwa: ‘Luke ngoja kidogo, nina habari nzuri kwenu.’ Alitukimbilia na kwa shauku akatuambia kuhusu huduma ya bima kwa viongozi ambayo kampuni yao imeianzisha siku hiyohiyo. (ulikuwa ni mpango uleule ambao Carl alikuwa ameugusia). Alitaka tuwe kwenye watu wa kwanza-kwanza kuingia kwenye mpango huo. Alitueleza kifupi jinsi bima hiyo ilivyo na akamalizia kwa kusema, ‘Huduma hii bado ni mpya kabisa, kesho nitamtuma mtu kutoka ofisini aje awaelezee vizuri. Kwa sasa, tujaze nakala za maombi yenu ili awe na taarifa za kutosha kuanza kufanyia kazi.’ Shauku yake iliamsha ari yetu ya kutaka huduma ile japokuwa hatukujua ipoje hasa, tulipopata taarifa zaidi, yalithibitisha yale yaliyosemwa na John jinsi alivyofikiri huduma itakuwa, na hakutuuzia tu huduma hiyo, bali aliongeza kiasi tulicholipia kwa ajili ya bima.
“Carl angeweza kuwa ndiye aliyetuuzia huduma ile, lakini hakufanya bidii yoyote kuamsha ari yetu ya kutaka huduma ile.”
Dunia imejaa watu wanaotaka vitu wao tu, na wanaofuatilia maslahi binafsi pekee. Kwa hiyo, wale wachache ambao bila ubinafsi wanajaribu kuwahudumia wengine wanakuwa na fursa kubwa sana na ushindani mdogo sana. Owen D. Young, mwanasheria na mmoja ya viongozi wakubwa wa biashara katika Marekani amewahi kusema, “Watu ambayo wanaweza kujiweka mahali pa wengine, na wanaoweza kuelewa jinsi akili zao zinavyofanya kazi, hawana haja ya kujali kuhusu maisha yao yatakuwaje.”
Kama kwa kusoma kitabu hiki umepata kitu kimoja tu—yaani kujijengea tabia ya mara zote kufikiria kupitia mtazamo wa wengine, na kuona vitu kwa mtazamo wao—kama umepata kitu hicho kimoja tu kutoka kwenye kitabu hiki, basi hicho kinaweza kuthibitika kuwa moja ya nguzo za taaluma yako.
Kuangalia mambo kwa mtazamo wa mwingine, na kuamsha ndani yake ari ya kutaka kitu fulani, haitakiwi kueleweka kuwa ni kumlaghai mtu huyo ili afanye kitu ambacho kina faida kwako tu na hasara kwake. Kila mmoja anatakiwa kufaidika kwa makubaliano. Kwenye barua za bwana Vermylen, mtumaji na mpokeaji, wote walifaidika kwa kufanya kile kilichopendekezwa. Wote, benki na bibi Anderson walifaidika kwa barua yake, benki ilipata mfanyakazi muhimu na bibi Anderson kazi nzuri. Na kwenye mfano wa mauzo ya huduma ya bima ya John kwa bwana Lucas, wote walifaidika.
Mfano mwingine ambao kila mtu anafaidika kwa kanuni hii ya kuamsha ari ya kutaka kitu, unatoka kwa Michael E. Whidden wa Warwick huko Rhode Island. Bwana Whidden ni afisa mauzo wa eneo hilo wa kampuni ya mafuta ya Shell. Mike alitaka kuwa afisa mauzo namba moja kwenye wilaya yake, lakini kituo kimoja cha mafuta kilikuwa kinamuangusha. Kilikuwa kinasimamiwa na mwanaume mmoja mzee ambaye haikuwezekana kumshawishi asafishe kituo chake. Kilikuwa katika hali mbaya kiasi kwamba mauzo yalikuwa yanashuka kwa kasi.
Msimamizi huyu hakusikia chochote alichoambiwa na Mike juu ya kuboresha kituo chake. Baada ya vitisho vingi na kumsihi—njia ambazo hazikuzaa matunda—mike akaamua kumualika msimamizi huyo kutembelea kituo kipya cha Shell kwenye eneo lake.
Msimamizi yule alistaajabia sana ubora wa kituo kile kipya. Mike alipomtembelea safari iliyofuata, kituo chake kilikuwa kimesafishwa na mauzo yameongezeka. Hili lilimuwezesha Mike kuwa afisa mauzo namba moja kwenye wilaya yake. Kuongea kwake na kujadiliana kote hakukusaidia kitu, lakini kwa kuamsha ari ya kutaka ndani ya msimamizi, kwa kumuonyesha kituo cha kisasa, alikuwa amefanikiwa lengo lake, na wote, Mike na msimamizi walifaidika.
Watu wengi hupita chuo kikuu na kujifunza kusoma mashairi ya Virgil na kubobea katika masuala ya hesabu bila hata ya kufahamu ni jinsi gani akili zao wenyewe zinavyofanya kazi. Kwa mfano: wakati fulani niliwafundisha wanafunzi vijana wa chuo waliokuwa karibu kuanza kazi kwenye kampuni ya Carrier, watengenezaji wakubwa viyoyozi juu ya uzungumzaji wenye matokeo. Mmoja wa washiriki alitaka kuwashawishi wenzake wawe wakicheza mpira wa kikapu kwenye muda wao wa ziada, alisema: “Napenda kucheza mpira wa kikapu, lakini mara chache nilizoenda uwanjani hakukuwa na watu wa kutosha kucheza mechi. Jana usiku wawili au watatu kati yetu tukaamua tu kurushiana mpira—na nilidhurika jicho. Ningependa kesho usiku wote mje. Ninataka kucheza mpira wa kikapu.”
Aliongea chochote juu ya unachotaka? Bila shaka hautaki kwenda kwenye kiwanja ambacho hakuna mwingine anaenda sivyo? Haujali kuhusu anachotaka. Hautaki kudhurika jicho.
Je, angeweza kukuonyesha jinsi ya kupata vitu unavyotaka kwa kutumia uwanja? Bila shaka, angeweza kuzungumza juu ya burudani utakayopata ukihudhuria.
Nikirudia maneno ya busara ya Profesa Overstreet:
Kwanza, amsha ari ya kutaka ndani mtu. Anayeweza kufanya hivyo dunia yote ni yake. Asiyeweza hilo, anatembea katika njia ya upweke.
Mmoja wa wanafunzi katika kozi ya kujifunza uandishi alikuwa na wasiwasi juu ya mvulana wake mdogo. Mtoto wake alikuwa na uzito chini ya wastani na alikuwa akigoma kula impasavyo. Wazazi wake walitumia njia zilizozoeleka. Walimfokea na kumsema mara zote. “Mama anataka ule hiki na kile.” “Baba anataka ukue uwe mtu mkubwa.”
Je, mvulana huyo alijali maneno hayo? Kama tu ambavyo wewe unajali juu ya punje moja ya mchanga kwenye mchanga wa ufukweni.
Hakuna mtu, hata yule mwenye akili za farasi atategemea mtoto wa miaka mitatu aelewe mtazamo wa baba yake mwenye miaka thelathini. Lakini hichi ndicho baba yule alitarajia. Ilishangaza. Mwishowe aliona hilo. Hivyo akajiambia: “Mtoto wangu anataka nini? Nawezaje kuunganisha matakwa yangu na yake?”
Mara alivyoanza kufikiri kwa namna hiyo mambo yakawa rahisi. Kijana wake alikuwa na baiskeli ya miguu mitatu aliyopenda kuendesha mbele ya nyumba yao huko Brookyln. Nyumba kadhaa mbele, kulikuwa na mvulana mmoja mkubwa na mbabe ambaye alikuwa akimnyaganya kijana wake baiskeli na kuendesha yeye.
Kiasili, kijana yule mdogo angekimbia kwa mama yake akilia, naye angetoka na kumnyang’anya mbabe yule baiskeli na kumpandisha kijana wake tena, hili lilitokea karibu kila siku.
Je mtoto yule alitaka nini? Haikuhitaji Sherlock Holmes kujibu hilo. Heshima yake, hasira yake, tamaa yake ya kujiona wa thamani—hisia zote zenye nguvu ndani yake—zilimsukuma kutaka kisasi, kumpiga yule mbabe ngumi ya pua. Na baba yake alipomueleze kuwa siku moja ataweza kumpiga mbabe yule kama akila vitu ambavyo mama yake anamtaka ale—baba yake alivyomuahidi hilo—hakukuwa na tatizo tena kwenye suala la kula. Kijana yule aliweza kula kila kitu ili awe mkubwa—chochote ili kuwa na ukubwa wa kutosha kumpiga yule mbabe aliyekuwa akimdhalilisha kila mara.
Baada ya kutatua tatizo hilo, wazazi wake wakahamia kupambana na tatizo lingine. Mtoto alikuwa na tabia ya kukojoa kitandani.
Alikuwa akilala na bibi yake, bibi yake alipoamka asubuhi, alishika mashuka na kusema: “Johnny ona ulichofanya tena jana usiku!”
Mtoto alijibu: “Hapana siyo mimi. Ni wewe.”
Kumfokea, kumchapa, kumuabisha—na kusisitiza kuwa wazazi wake hawataki afanye hivyo—hakuna kati ya hayo yaliyofanya kitanda kiwe kikavu. Hivyo wazazi wake waliuliza: “Tunawezaje kumfanya kijana wetu atake kuacha kukojoa kitandani?”
Matakwa yake yalikuwa ni nini? Kwanza, alitaka kuvaa nguo za kulalia kama baba yake na si gauni la kulalia kama bibi yake. Bibi yake alikuwa amechoshwa na tabia zake za usiku hivyo akajitolea kumnunulia nguo za kulalia iwapo ataacha kukojoa kitandani. Pili, alitaka kitanda chake peke yake. Bibi yake hakupinga.
Mama yake akamchukua hadi kwenye duka la samani huko Brookyln, alimkonyeza msichana wa mauzo na kusema: “Huyu bwana mdogo anataka kufanya manunuzi.”
Urefu ukiwa umemuongezeka kwa inchi kadhaa sababu ya kauli ile, alisema: “Nataka kujinunulia kitanda.”
Alipoonyeshwa kitanda ambacho mama yake alitaka akinunue, mama yake akamkonyeza tena yule muuzaji na mtoto wake akashawishiwa kukinunua.
Kitanda kililetwa siku iliyofuata; na usiku huo, baba yake aliporudi, mvulana alimkimbilia mlangoni akipiga kelele: “Baba! Baba! Njoo ghorofani uone kitanda changu nilichonunua!”
Baba yake, huku akiangalia kitanda, akatii kanuni ya Charles Schwab: “Alikuwa mwenye kuonyesha uthamini kutoka moyoni na mwingi katika kupongeza.”
“Hautakojoa kwenye kitanda hiki, siyo?” alisema baba.
“Hapana, hapana! Sitakojoa kwenye kitanda hiki.” Na mtoto alitunza ahadi yake, maana fahari yake ilihusika. Na hiyo ni kitanda chake. Ni yeye mwenyewe ndiye amekinunua. Na sasa alikuwa akivaa nguo za kulalia kama baba yake. Alitaka kutenda kama baba yake. Na alitenda.
Baba mwingine, K. T. Dutchmann, aliyekuwa ni mhandisi wa simu, ambaye naye alikuwa ni mwanafunzi wa kozi hii, alikuwa ameshindwa kumfanya binti yake wa miaka mitatu ale kifungua kinywa. Njia za kawaida kama kumfokea, kumtisha na kumbembeleza zote hazikufanikiwa. Kwa hiyo wazazi wake wakajiuliza: “Tunawezaje kumfanya binti yetu atake kula?”
Binti yule alipenda kumuiga mama yake, kujihisi mkubwa na mtu mzima; kwa hiyo siku moja walimsimamisha kwenye kiti na kumuacha atengeneze kifungua kinywa. Wakati huo huo, ili kucheza na saikolojia yake, baba yake aliingia jikoni binti alipokuwa akiandaa kifungua kinywa, binti akasema: “Ona baba, naandaa kifungua kinywa leo.”
Siku hiyo alikula mara mbili ya kiasi ch kawaida bila kulazimishwa, sababu alikuwa amependezwa nacho. Alikuwa amefanikiwa kupata hisia za kuthaminiwa; kwa kuandaa kifungua kinywa, alikuwa amepata uwanja wa kujieleza/kujionyesha.
William Winter amewahi kusema, “Kujieleza/kujionyesha ni hitaji muhimu la asili la mwanadamu.” Kwa nini hatutumii saikolojia hii kwenye masuala ya kibiashara? Tunapokuwa na wazo zuri, badala ya kuwafanya wengine wafikiri ni wazo letu, kwa nini tusiwaache wapike na kukoroga wazo hilo wenyewe. Hapo watalichukulia kama wazo lao; watalipenda na pengine watalila zaidi ya kawaida.
Kumbuka: “Kwanza, amsha ari ya kutaka ndani ya mtu. Anayeweza kufanya hili, dunia yote ni yake. Asiyeweza, anatembea katika njia ya upweke.”
KANUNI YA 3
Amsha ndani ya wengine ari ya kutaka