Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida

Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida

Mr bigi anapopewa lifti na kikaushi chake cheus.

Jirani nishushe hicho kinjia cha kwenye korongo we endelea na safari.


Photo by MR BIGI BIGI on April 19, 2022..jpg
 
Yule Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida - Usiku wa mateso.



Usiku ule sitakuja kuusahau maana yale nloshuhudia yalikuwa nje kabisa ya ulimwengu huu wa nyama na damu, sijui niseme ni ulimwengu gani ule lakini itoshe kusema ni ulimwengu wa ajabu mno nilioonyeshwa na bwana yule ...

Nilikurupuka usiku baada ya kusikia mtu anagonga hodi mlangoni nikadhani nipo ndotoni lakini kumbe haikuwa hivyo, ilikuwa ni kweli mtu anagonga mlangoni, wala sio kwamba masikio yangu yalisikia vibaya, lah, ilikuwa ni uhalisia.

Kabla ya kunyanyuka kitandani nikatazama nje dirishani, huko palikuwa shwari, kumetulia tuli-tuli, hata nilipoangaza mlangoni niliona mlango wa grill umefungwa, basi nikatulia kidogo nikijiuliza yanayoendelea, bado hapo mlango wangu ukiwa unaendelea kugongwa na kugongwa.

Mwishowe wa kufikiri niliamua kupiga moyo konde nikaenda sebuleni, nikawasha taa kisha nikaufuata mlango na kuufungua, kutazama simwoni mtu! Nilitazama korido nzima nisiambulie kitu wala mdudu yoyote anayetembea ukutani, nikatazama milangoni, nikaona kila mlango kwa chini yake ukiwa ni kiza totoro, taa zimezimwa huko ndani, ni kimya cha mwituni! Moyo wangu unapiga kana kwamba unataka kutoka kifuani.

Kabla sijaufunga mlango, yaani nikiwa hapohapo bado naangaza, mara nilisikia sauti ya kikombe kikidondoka - puuh!- alafu ikafuatia na kilio kikali cha mtoto kule chumbani! Basi haraka nikaurejesha mlango wangu pasipo hata kuufunga na funguo, nikakimbilia kule chumbani kama mwendawazimu, kufika huko nikawasha taa upesi, kurusha macho kitandani namwona mtoto ameegamia ukuta, uso wake ameufinyaga kwa kilio na hofu. Chini kuna maji yaloyomwagika pamoja nayo kikombe cha plastiki ambacho huwa tunatumia kunywea maji.

Mtoto aliponiona alinikimbilia akanikumbatia kwanguvu akinambia baba kuna mtu baba kuna mtu ... Nikamuuliza mtu gani? Yuko wapi? Hakusema cha kueleweka.

Alikuwa anatetemeka mwili mzima, macho yake hayakomi kumwaga machozi, hapo amening'ang'ania kana kwamba nilimuahidi nitamrushia korongoni.

Nilitazama kila kona ya chumba lakini sikuona chochote kilichomtisha, kidogo nilipotazama dirishani, ndo' nikaona kivuli cha mtu akiwa anachungulia, kivuli kipana katika kingo ya dirisha langu la kaskazini, lakini kivuli hicho -kufumba na kufumbua - kilitokomea kwa kushuka chini! Nikastaajabu kuona.

Nilitulia hapo kidogo nikitazama, kila kitu mbele ya macho nikiona kama miujiza ama ndoto hivi, yaani muujiza mbele ya mboni zangu, niliporadhi ndipo nikasogea taratibu dirishani kutazama nje. Huko palikuwa pametulia tuli, hamna mtu wala kiumbe ninayemwona, lakini niliporusha macho kule kwenye mlango wa grill, nikaona mlango huo uko wazi! Sikujua nani nani aliufungua na ni muda gani alifanya hivyo maana sikusikia mlango huo ukipiga kelele zake za siku zote, nikabaki tu nikiutazama kwa kama dakika moja, sikuona kitu wala mtu hapo, kidogo nikasikia tena mtu akiugonga mlango wangu kwa mtindo uleule --- ngo ngo ngo ngo! "Nataka tuongee, nina shida na wewe!"

Aisee nikahisi tumbo linakoroga, miguu yangu inapoteza nguvu, pumzi yangu mwenyewe inanikaba. Kwa muda huo nilitamani pakuche lakini wapi! Nilihisi muda umekwama kunikomoa na mateso ya usiku ule. Nilitazama saa ya simu yangu nikaona zimepita dakika tano tu tangu nikurupuke toka usingizini, nikaamini kabisa muda unashirikiana vema na mtesi wangu. Ule ulikuwa usiku wangu wa adhabu.

Nikajitahidi kutulia kadiri nilivyoweza lakini sikufua dafu abadan, mlango wangu uliendelea kugongwa pasipo kukoma huku mtu anayegonga akinitaka tukaongee tena akitumia sauti yangu, moyoni nikaapa siendi popote, nitabaki palepale kitandani na mtoto wangu mpaka nione nini kitakachojiri.

Baada ya dakika moja ya kuvumilia, nasikia kabisa mlango unagongwa lakini napuuzia, mara nilisikia kitasa cha mlango kikitenguka - 'klap!'- alafu ikafuatiwa na sauti za bawaba za mlango 'kkrrriiiiiiiiii!' ... sauti zilizoashiria mlango wangu unafunguka alafu sauti hizo zikakoma ghafla na kuwa kimya! Kimya cha kaburi. Kwa kama dakika tatu hivi ni kimya, sikusikia kitu chochote kile, nipo tu kitandani nimemkumbatia mwanangu.

Kwa kipindi chote hicho,sikuwa najua nifanye nini maana ubongo wangu uligeuka kuwa uwanja wa fujo, moyo nao unapiga mpaka nausikia masikioni kana kwamba ngoma za turufu! Jasho nalo linanichuruza nalisikia kabisa likishuka mgongoni chii-chii-chii kuangukia chini.

Sasa baada ya kimya hicho cha muda, nilisikia vishindo vya miguu vikipita sebuleni, vinakatiza hapa na pale, pale na hapa, alafu baada ya sekunde kumi na tano hivi, mlango wangu wa chumbani ukagongwa mara moja, "ngo!" ... Ile 'Ngo' ya kuashiria mgeni ameshafika ndani kisha kukarudi kuwa kimya tena, kimya cha awali.Sasa nikawaza,kama mtu huyu amengia ndani kwangu, je, mimi sina budi kujihami na kitu chochote nilichonacho?

Upesi nikatazama kwenye pembe ya kitanda changu, kule nilazapo miguu, hapo kulikuwa na fimbo moja ndefu nene, nikaichomoa na kuishika mkononi barabara kama lolote likitokea basi nipate kujihami, lakini nilishika fimbo hiyo mpaka nikachoka, hamna nilichokiona wala hamna kilichoingia ndani.

Nilimaliza sala zote ninazozijua, nilimuita Mungu wangu kwa majina yote niliyofunzwa kanisani na mtaani lakini bado nilijihisi niko mwenyewe, dunia imenipa mgongo.

Nilingoja hapo kwa muda ambao niliona unatosha, nikanyanyuka kwenda kuufungua mlango wa chumbani kutazama sebuleni kama kuna mtu niliyemuhisi,kufika huko na kuangaza sioni mtu, lakini nilipotazama mlango wa sebuleni nikauona uko wazi, tena wazi ya kuachama haswa, nikarusha macho huko nje ya mlango, yaani koridoni, napo sikuona kitu wala mtu, lakini kitambo kidogo nikaanza kuhisi naishiwa nguvu katika namna ya ajabu, kichwa kinakuwa kizito na macho yananielemea, sijakaa vema nikaanguka chini, hoi taabani, hata kuusogeza mkono wangu mwenyewe nashindwa, sijiwezi kabisa, kitu pekee nilichokuwa namudu ni kusikia na kuona tu!

Nikiwa hapo chini, nimelala kifudifudi,sijui nini kinaendelea, macho yangu yanatazama kule koridoni, mara nilisikia sauti ya mlango unafunguka, haukuwa mlango mwingine bali mlango wa BIGI, na kitambo kidogo nikamwona mwanaume huyo anatoka sasa akija mwelekeo wangu.

Bwana huyo alikuwa amevalia kaniki nyeusi kiunoni, mithili ya taulo la kwendea bafuni, na kichwa chake amekiveka kiremba kikubwa chekundu, kiremba ambacho baki yake aliilazia kwa nyuma kana kwamba mwanamke mwenye nywele ndefu.

Kumwona bwana huyo akinijia, nikajaribu kwa nguvu zangu zote ninyanyuke lakini sikuweza kabisa kabisa, nilikuwa kama mtu aliyepigwa nusu kaputi kwaajili ya upasuaji, kitu pekee nilichokuwa naweza kufanya ni kugeuza shingo yangu huku na kule, hata nilipojaribu kutoa sauti kupiga yowe nayo hakuna! Nilikuwa mithili ya samaki majini, naachama tu mdomo lakini hamna chochote kinachotoka.

Bwana yule, nikiwa namshuhudia kwa macho yangu, aliingia ndani akaelekea moja kwa moja chumbani, kule ambapo mwanangu alikuwamo, huko sijui akawa anafanya nini, hata mtoto alikuwa kimya, baada ya muda kidogo akatoka akiwa amembeba mtoto begani huyoo anajiendea zake.

Aliuruka mwili wangu akatoka mlangoni kisha moja kwa moja akaenda kwake ... Nimebaki tu namtazama, macho yanavuja machozi ... naona kabisa mwanangu akienda kuuawa na huku sina la kufanya.

Nilifurukuta nikafurukuta ... nilifurukuta tena na tena. Nilifurukuta kwanguvu zangu zote na za akiba, nikatahamaki niko kitandani nimeketi nahema kama mbwa wa mashindano, nikajaribu kuunyanyua mkono wangu wa kulia, mkono ukanyanyuka, nikausogeza mguu, nao ukasogea, nikajiuliza ina maana yale yote niliyoyaona nilikuwa ndotoni?

Nilijikuta nafsi yangu inakataa.

Nilitazama kando yangu nikastaajabu mtoto hayupo, kitanda cheupe pe, nikanyanyuka upesi kama nakimbizwa kwenda kuwasha taa, nikawasha na kuangaza sikuona kitu, chumba kizima nilikuwapo mwenyewe. Nikakimbilia sebuleni kutazama, napo sikuona kitu, hata mlango wake umefungwa na funguo! Sasa nikahisi kurukwa na akili, mtoto yuko wapi?

Hapana! Nilizungumza mwenyewe kama mwehu ... hapana haiwezekani! Nikaufungua mlango wangu nikaenda moja kwa moja mpaka mbele ya mlango wa BIGI, nikaugonga mlango huo kwanguvu BAM-BAM-BAM-BAM! Fungua, namtaka mwanangu! BAM-BAM-BAM!- niliubamiza mlango huo bila huruma na bila kukoma, nafoka na kuchonga, namtaka mtoto wangu!

Kelele hizo zikawaamsha watu walokuwamo kwenye makazi ya Tarimo. Niliona wamewasha taa ndani wakiwa wanazozazoza, bila shaka walikuwa wanajiuliza ni nini kinachoendelea, lakini mimi sikujali, nikaendelea kuubamiza mlango wa BIGI niking'aka, kidogo mlango huo ukafunguliwa akatoka mwanaume huyo mpana akiwa amevalia kaushi yake pana na bukta.

Kabla hajasema kitu nikamwambia, "brother, namwomba mwanangu! Tena namwomba upesi kabla hatujajaza umati wa watu hapa."

Akawa ananitazama, hasemi kitu. Mara nikasikia mlango wa makazi ya Tarimo unafunguka, kutazama ni Mama Tarimo, mama huyo anatoka huku akiwa anatengenezea khanga yake kifuani, nyuma yake yuko dada mmoja hivi ambaye sikuwa namfahamu wana mahusiano naye gani, wote hao wawili nyuso zao zimeparwa kwa maulizo.

Mama Tarimo aliuliza, "Shemeji, kuna nini?" Nami upesi nikamwambia yule bwana BIGI amemchukua mwanangu kimazingara na mimi nimekuja hapo kumfuata. Kwa jazba nilokuwa nayo sikuwa najali chochote kile, niliyamwaga maneno mengi na vitisho, nikiapa siondoki pale mpaka pale nitakapompata mwanangu.

BIGI aliuliza, "Una uhakika mwanao yumo humu ndani?" Nikamwambia ndio, nikamtaka asogee pembeni mimi niingie ndani kutazama. Katikati ya hayo, mara Mama Tarimo akaniita: baba fulani, nilipomgeukia akaniuliza,"yule pale si mtoto?"

Kuangalia kwangu, nikamwona mtoto akiwa amesimama mlangoni ananitolea macho. Nikastaajabu. Nini hiki? Nilimwendea mwanangu upesi nikamkagua na kumuuliza alipokuwapo,akasema ndani, ndani gani na mimi niliangaza kila kona ninayoijua?

Niligeuka kumtazama BIGI, nikamwona bwana huyo ananiangazia, kama kawaida macho yake hayakuwa hata na tone la hisia ndani yake, hakusema kitu, ameegamia tu kingo ya mlango wake, nikaurejesha uso wangu kwa mtoto, nikamwona akiwa amejibana kwangu, amenishikilia nguo, anachungulia kwa woga.

Kidogo bwana BIGI akaingia ndani mwake, pia na Mama Tarimo, mimi nikawa wa mwisho kuufunga mlango.

Nilimpeleka mtoto kitandani nikamtaka alale lakini mimi nikiwa nasumbuka sana na mawazo kichwani, ina maana ni kweli mimi nilikuwa ndotoni? Ina maana yale yote ni mambo tu yaliyotungwa na ubongo wangu?

Sikuridhika...

Nilikagua mazingira ya mule chumbani, na hata sebuleni, nikaamini kabisa sikuwa ndotoni. Yale yote nloshuhudia yalikuwa halisia. Moja, kikombe kile cha maji bado kilikuwapo chini na maji yale bado sikuyadeki, lakini pili jasho nililomwaga nikiwa pale sakafuni sijiwezi kabisa, bado lilikuwapo, sasa halikuwa kimiminika bali limeganda pananata.

Sasa ilikuaje? Sijawahi kuelewa mpaka leo hii.

Baadae Jua lilipochomoza nikalishuhudia kama ukombozi, tena ukombozi nilioupambania kwa muda mrefu, mbali na kwamba nilihisi maumivu ya hapa na pale ya taya yangu ya chini, mimi sikujali sana na nilichofanya, pasipo kupoteza muda, nilidamka nikamwandaa mtoto na mimi pia kisha safari ikaanza kuelekea Massana hospitali, huko nilionana na mke wangu na pia mama yangu ambaye alifika muda si mrefu hapo, nikamwachia mtoto mama yangu nikimtaka aende naye kwake kule Mbezi Beach, Afrikana, mimi nitakuja kumpa habari vizuri nikitoka kazini, uzuri kumbe siku hiyo ndo' ilikuwa siku ambayo mke wangu alikuwa anategemea kutoka hospitali, hivyo basi wakaona ni vema wakienda huko Afrikana kwa pamoja. Mimi niliwaahidi nikitoka tu kazini nitaonana nao.

Baada ya kuachana nao, nilielekea kazini, huko niliweza kufanya kazi kwa kama masaa mawili ya mwanzoni lakini baada ya hapo nikaelemewa. Kichwa kilikuwa kizito kwa kukosa usingizi wa usiku ulopita kiasi nikawa naona kazi ni adhabu. Macho yananiwasha na niko 'slow' sana.

Nilitafuta 'kamuda' fulani, mbali na kubanwa hapa na pale, nikajipumzisha kidogo kwa kuegamia meza, usingizi ukanikomba bila huruma, kuja kuamka nimelala masaa mawili kama utani, na kama si kuamshwa sijui ningeamka saa ngapi? Kutazama simu yangu, naona 'missed call' na ujumbe mmoja, vyote vimetoka namba ngeni.

Ujumbe huo nilipoufungua ulikuwa unasomeka hivi: "Mimi Bembela nimesharudi nyumbani fanya tuongee." Nikapiga namba hiyo mara moja, simu ikaita kidogo na kupokelewa na sauti ya mwanamke, sauti ya Bembela, akanisalimu na kunijuza kuwa amefika nyumbani muda si mrefu, kila kitu amekiweka sawa lakini kuna jambo moja tu amekwama, anataka kuona kama naweza nikawa na msaada.

Alisema: "baba fulani, hapa sasa ili kila kitu kiende sawa, nahitaji nipate kitu kimoja ambacho ni mali ya yule bwana. Kitu kimoja tu, kama vile yeye achukuavyo vyetu na kuvitendea kazi, ndivyo na mimi pia. Je, unaweza nisaidia?"

Nikawaza vile viroba vya BIGI kule korongoni, je, mule hatuwezi kupata kitu? Nilipomweleza hayo akanielezea hofu lake ya kwamba vitu vile havina uhakika kama ni vyake au vya watu wengine, tusije tukawaingiza waso na makosa katika adhabu ya mtu mwingine, hivyo yatupasa kuwa na hakika asilimia zote.

Nilipofikiria vema, nikaikumbuka ile sarafu ya hamsini katika mfuko wangu wa suruali. Nilikuwa na hakika kabisa ile ilikuwa ni mali ya BIGI lakini ubaya ni kwamba sarafu hiyo siku ile nilivyotoka hospitali baada ya kunisababishia majanga sikukumbuka niliiweka wapi haswa, sikuibakiza nguoni mwangu.

Ila kitu kilichonipa moyo ni kwamba mke wangu hakuwapo nyumbani, na mimi sikuwahi kufanya usafi mule ndani chumbani tangu siku ile, hivyo niliamini naweza nikaipata nikiitafuta.

Nikamwahidi Bembela na yeye akakata simu tulipomaliza maongezi.

Mbali na kwamba, nilikuwa nimeokoa salio langu la simu kwa simu ile kukatwa na Bembela, nilikuwa pia nimejipunguzia maumivu ya kinywa changu ambacho kilikuwa kinanivuta sana, haswa taya ya chini, kila nilipokuwa nazungumza neno.

Sikufahamu maumivu hayo yalisababishwa na nini na sikudhani kama yangeendelea kuwa makali vile, kipindi nayahisi pale asubuhi niliyachulia kiwepesi tu nikidhani labda nililala vibaya na hivyo yatakoma lakini kadiri muda ulivyoenda nilianza kuhisi hiyo kitu ni 'serious'.

Na kweli ilikuwa ni 'serious'.

Mpaka kufikia majira ya usiku, taya yangu ya chini ilianza kupinda ikielekea upande wangu wa kushoto wa mwili! Kila nilipoivuta kuiweka sawa, nilihisi maumivu makali yasokuwa na mfano!




***

Depal najua husomi ila ngoja nikutag dada kibungo
 
Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida - 03

Haikukaa muda mtoto akanyamaza kisha kukawa kimya sana, kimya cha usiku, nami nikakaa kitandani kubembeleza usingizi ambao baada ya muda ukanichukua.

Usiku huo, sikukumbuka ni nini ila nilikuja kushtuka majira ya saa kumi na moja ya alfajiri nisijue kilichonikurupusha ni kitu gani. Kidogo nikasikia sauti iliyonishtua sana, pengine kwasababu nilikua katika hali ile ya taharuki, ilikuwa ni sauti ya maji yakiichapa ndoo kwa presha kubwa, nilipotazama nikaona moja wa majirani akiwa anachota maji, baada ya hapo sikuupata usingizi tena mpaka majira yangu ya kwenda kazini yalipowadia.

Siku hiyo nilihangaika mno kazini, usingizi ulikuwa unanikaba narembua macho kama mjinga, kila nilipopata nafasi ya kuegemea kitu, hata kama sikudhamiria, nikawa napitiwa na usingizi. Nilikuwa mithili ya teja mwenye arosto.

Nilipochomoka kazini na kufika nyumbani majira ya jioni, sikuchukua muda nikajilaza kwa uchovu. Nililala majira ya saa kumi na mbili, kwasababu hiyo nilijikuta naamka majira ya usiku mnene usingizi umekata, nikatoka kwenda kuoga maana joto nalo lilikuwa jingi na tokea nilivyorudi nyumbani sikupata kuoga, nilijilaza tu kama ng'ombe.

Nje kulikuwa kumetulia sana, kelele zangu za kuchota maji ndo ziliharibu utulivu, bomba lilikuwa na presha kubwa sana kama ugomvi, nilipomaliza nikaingia bafuni lakini nikiwa navua taulo langu mara nikasika kaaa-kaaa-kaaa, sauti ya grill la nyumba kubwa, nikatulia kimya kuskiza, sikusikia kitu, nikahofu anaweza akawa mwizi anaingia ndani hivyo nikachungulia kwa mwanya wa mlango, sikuona kitu, nikafungua mlango ili nione vema, taulo langu kiunoni, nikarusha macho kule kibarazani, sikuona kitu.

Nikatoka bafuni kusogelea nyumba kubwa, hamaki nikasikia kelele za mwizi mwizi, kufumba na kufumbua nikamwona mtu akitoka ndani ya nyumba kubwa kwa kasi kubwa, lengo lake lilikuwa ni kuufuata ukuta akwee lakini aliponiona nipo upande huu wa magharibi ya nyumba akabadili mwelekeo kukimbilia mashariki, kule kwenye geti kubwa, nami nikaongeza mwendo kumkimbiza, mkono wangu wa kuume umeshikilia fundo la taulo iliyomo kiunoni mwangu, kukata kona nikamwona mwizi yule akikwea ukuta, sikumuwahi akawa amesharukia huko nje, na mimi sikujaribu kuhangaika maana niko nusu uchi nisije nikaacha mazaga hadharani, kidogo akatokea jirani mmoja na kisha mwingine akiwa ameongozana na mkewe, mwanamke huyo akasema alimkuta mwizi akiwa anapekua viatu ambavyo vipo mwishoni kabisa wa korido wakati anatoka aende maliwatoni ndipo akapiga kelele za mwizi.

Basi kama ilivyo ada mjadala ukaanza tena wa mambo ya wezi, wakaongezeka na majirani wengine kadhaa haswa wa vile vyumba vya nje, nao wakasimuliwa yaliyotokea na wakatoa maoni yao, tukakubaliana kwa dhati kuwa mwenye nyumba anapaswa kuitwa kikao kuhusu hili maana akipigiwa tu simu na kuelezwa haitatosha, inabidi aje tumsihi atuongezee urefu wa ukuta na pia atuboreshee miundombinu ya usalama mathalani geti, kwani kodi si tunalipa bwana?

Tukiwa tunajadiliana hayo, nilitazama dirisha la chumba anamoishi BIGI maana dirisha hilo limetazama upande huu na halipo mbali sana na geti kubwa, bila shaka hata hapo tulipokuwa tusimama kuongea alikuwa anatusikia vema maana tupo karibu na dirisha hilo. Nilipotazama nikaona dirisha lenye kiza maana ndani hakukuwa kumewashwa taa lakini nilipotia umakini hapo nikabaini pazia la dirisha lilikuwa limefunguliwa kidogo, nikahisi kabisa kuna mtu yumo pale anachungulia nje.

Kitu kilichonifanya nikaamini hivyo ni pale nilipoendelea kulitazama lile dirisha, pazia liliachiwa likafunga, baada ya muda kidogo pazia likafunguliwa tena na nilipotazama nikaona limefungwa upesi. Sikujua ni nani alikuwa dirishani hapo sababu ya giza la chumbani lakini nilipatwa na maswali kama sio kustaajabu na watu wale.

Baada ya muda kidogo, kila mtu alirejea kwenye kiota chake na mimi nikarejea bafuni kuoga. Nilichokifanya sasa niliufunga ule mlango wa grill kwa ufunguo alafu nikaenda nao bafuni kwaajili ya usalama zaidi, lakini kabla sijamaliza kuoga nikasikia mtu akigonga mlango, mlango ule wa grill, hakika nikashtuka, nikasema na nafsi yangu pengine kuna mtu anataka kutoka kwenda maliwato na funguo ninayo mimi, basi nikajifunga taulo upesi pasipo kujikausha mwili ili nipate kutoka haraka, mara nikasikia tena mlango unagongwa, mara hii unagongwa kwanguvu sana bam-bam-bam-bam!

Nikatoka na kuyarusha macho yangu upesi kule kibarazani, nikamwona mtu mkubwa amesimama mlangoni. Mwanga wa kibarazani haukua ang'avu lakini nilimtambua mtu yule alikuwa ni BIGI, mkononi ameshikilia mkoba. Nilimsalimu na kumwambia ufunguo ninao mimi kisha nikamfungulia mlango akaingia ndani, nami nikaingia ndani kumfuatia, mkononi nina ndoo yangu ya kuogea, lakini nilipopiga hatua kadhaa kuufuata mlango wangu nikabaini nimeacha sabuni ya kuogea bafuni kwasababu ya ile haraka yangu, basi sikuwa na budi kurudi nje.

Nilipotoka nikasikia sauti ya pikipiki nje ya uzio, alikuwa ni yule jamaa bodaboda, yale yalikuwa ni moja ya majira yake ya kurejea nyumbani. Alifungua geti dogo akaingia ndani, kabla hajaenda kuegesha chombo chake alinisalimu na kuniuliza kama kuna mtu ameingia hapo nyumbani muda si mrefu, nikamjibu BIGI ndiye ameingia, akaniuliza;

"Yule jamaa mgeni enh?"

Nikamjibu ndio na kumuuliza, "kwani unamjua?" Akaniambia alishawahi mwona siku moja hapo nyumbani, mke wake akamwambia kuwa ni mpangaji mpya na amekuwa akikutana naye mara chache chache huko barabarani usiku mkubwa.

Alisema,

"Basi nilidhani nimemfananisha, nimemwona hapo kilimani akiwa anashuka na mdada fulani hivi, nadhani ni mkewe, nikajaribu kuwashtua ili nije nao lakini sikufanikiwa, nikasema nimeona vibaya nini?"

Pale nyumbani jografia yake ilikuwa hivi, kwa mtu anayetumia usafiri, aidha gari au pikipiki, kuna mahali fulani akifika hatoweza kutumia njia fupi zaidi (shortcut) ya kufika nyumbani kwasababu njia hiyo ni mbovu na nyembamba sana, hivyo atalazimika kuendelea kunyoosha na barabara mpaka mbele kabisa ambapo atakata kona na kuanza kurudi nyuma kwendea nyumbani, kwasababu hiyo ni kawaida kwa mtembea kwa miguu akafika mapema nyumbani kabla ya mwenye usafiri endapo wakiachania hapo.

Tukiachana na hilo, maelezo ya jamaa huyu kwamba alimwona BIGI na mwanamke aliyemdhania kwamba ni mkewe wakiwa wanatembea kuja nyumbani yalinitatiza kiasi kwasababu mimi nilimpokea BIGI akiwa peke yake mlangoni na mkoba wake mkononi, huyo mwanamke sikumwona machoni pangu.

Nikamuuliza kama kweli aliona vema, akasema ana uhakika na alichosema, nami sikutaka kusema zaidi mengine yakabaki ndani yangu, yeye akaenda kupaki chombo chake na kuingia zake ndani, na mimi pia nikaingia ndani na kujilaza kitandani ...

Nikawaza.

Nikajigeuza kitandani nikiwaza.

Hamna nilichoelewa.

Kama BIGI na mkewe hawakuwamo ndani, yule aliyekuwa anachungulia dirishani muda ule ni nani? Ni mtoto wao au? Na huyo mwanamke ambaye alikuwa na BIGI njiani lakini hakufika naye nyumbani, ni mkewe kweli? Kama ndiye mbona sasa ..... Aaagh ... Sikuelewa kitu! Hamna kilichokuwa kinaeleweka, nilikaa hapo mpaka kunakucha maana sikuwa na usingizi kabisa, ajabu wakati jua linawaka ndipo nikaanza kuona macho mazito, nashukuru ilikuwa ni weekend na siku hizo sikuwa naenda kazini basi nikajilalia zangu.

Kesho yake, siku ya jumapili, mwenye nyumba alifika pale nyumbani majira ya mchana kwaajili ya kuitikia wito wetu wa kikao. Kama kawaida yake alipofika alipita kila mlango akigonga na kusalimu na baada ya muda mchache karibia kila mtu akasogea kibarazani kwaajili ya kikao kile cha dharura, watu waliokosekana walikuwa wachache sana; yule jamaa bodaboda pamoja na BIGI ila wengine wote walikuwapo ikiwemo mke wa BIGI pia.

Mwanamke huyo alikuwa ameketi kwenye kona, amejitanda mtandio kichwani, ametulia tuli tofauti kabisa na wenzake, hata kikao kilipoanza karibia kila mtu alisema ya kwake lakini kwake hali ilikuwa tofauti, hakushiriki kwenye chochote, pengine sababu ni bubu hata angesema asingeeleweka, nikajiwazia mwenyewe moyoni, lakini cha ajabu ni kwamba kila niliporusha macho yangu kumtazama, aidha kiwiziwizi ama moja kwa moja, nilikutana na macho yake akinitazama.

Haikujalisha niliupoteza muda kiasi gani baada ya kumtazama ila kila nilipoyarejesha tena macho yangu kwake, nilimkuta mwanamke yule ananitazama. Macho yake hayakuwa ya urafiki.
**

Muendelezo soma Jirani yangu wa Kule Goba hakuwa mtu wa kawaida
Very interesting

Sent from my Infinix X665 using JamiiForums mobile app
 
Back
Top Bottom