Lee
JF-Expert Member
- Jul 31, 2013
- 43,973
- 150,463
Yule jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida - 12
ILE ndo siku niliyoona vema makazi ya BIGI kwa ndani, hapakuwa kama sehemu zingine za kwawaida kwamba utakuta kochi, meza na samani zingine, hapana, yeye ndani kwake kulikuwa na mkeka mmoja, jaba moja kubwa la maji, viroba vitupu, mifuko kadhaa ya plastiki, ile ilopigwa marufuku, nguo kadha wa kadha zilizochoka na kuchacha, pia na takataka zingine ambazo sikuzielewa ama sikuzitilia mkazo kuzielewa.
Ukitazama kwa haraka haraka mahali hapo unaweza dhania dampo, sio makazi ya watu wa kawaida, kumbe ni mahali pa familia ya watu watatu, nikajiuliza kama sebuleni palikuwa vile je, muhali gani chumbani?
Kwa mikono nane, yaani wanaume wanne, tulibeba mwili wa BIGI tukaelekea kwenye geti kubwa, hapo tukapita kisha tukatembea kukatiza njia ilopita kama nyumba tatu hivi mpaka kufika mahali ambapo gari lilipakiwa, tukamweka humo bwana BIGI kwenye viti vya nyuma kisha kila mtu akahema kwanza maana haikuwa kazi nyepesi, bwana yule alikuwa na kilo za kutosha.
Na muda wote huo tulokuwa tumembeba kumpeleka kwenye gari lile alikuwa ametulia tuli kana kwamba kiroba cha taka, hakuuchezesha mwili wake zaidi ya kuguguma kwa mbali na mdomo wake ulokuwa wazi, nililijua anaguguma wakati tunamtengenezea aketi vema kwenye ule usafiri, hapo kwa bahati nzuri au mbaya nikajikuta nikiusogelea uso wake ... Ushawahi kusikia sauti ya mtu aliyebanwa kifua na kitu kizito? Ndivyo ilikuwa kwa BIGI.
Tulimbeba pia mke wake, wanaume wawili, tukampeleka kwenye lile gari, bado amefunga macho lakini anahema, haikujalisha kumtembeza barabara nzima mpaka kwenye gari, mwanamke yule hakujigusa wala kufumbua macho yake.
Lakini,
Bwana yule nilokuwa nikisaidia naye kumbeba yule mwanamke, yaani jamaa wa ulinzi shirikishi, kuna kitu alibaini kumhusu mwili wa mwanamke yule, kitu ambacho mimi kwangu hakikuwa kigeni, alistaajabu namna mwili ule ulivyokuwa wa baridi kana kwamba umetokea kwenye jokofu, akaniuliza ni namna gani mtu mzima anaweza akawa katika hali ile? ... Kweli hata mimi sikuwa na majibu.
Tulimfikisha mwanamke yule kwenye gari, tukamtengenezea vema, kurudi tukamkuta Mwenye Nyumba akiwa amesimama kibarazani pamoja na Mjumbe, mabwana hao walikuwa kwenye mazungumzo, kidogo Mwenye nyumba aliponiona aliniita akaniambia zoezi lililomleta hapo itabidi alisitishe kwa muda mfupi, alikuwa amekuja kwaajili ya kutoa vitu vya BIGI akidhania bwama huyo yupo ama hata kama hayupo basi ni mkamilifu wa mwili lakini haikuwa hivyo, kwahiyo ameona, kwasababu za ubinadamu, atazame kwanza swala lile linakuaje kisha atakuja kuendeleza alipoishia.
Lakini,
Kwa mdomo wake, alikiri familia ile haikuwa ya kawaida, ni aibu tu kuwatupia vitu vyao nje ilhali wapo katika hali ile, la sivyo ...
Aliniuliza: "unamjua mtu yoyote wa karibu na huyu bwana?"
Nikamwambia hapana, hata namba yake ya simu tu sina sembuse kufahamu watu wake? Akaniuliza sikupata kuwaona katika msiba? Nikamwambia sikuwepo kabisa katika msiba, labda majirani wengine, tena mbali na Bembela na yule shoga yake maana nao hawakuwapo, ikawa kheri bwana yule aliyeungana na mimi kutoa msaada tulipoitwa mwanzoni, yeye alikuwapo msibani, akamuuliza, lakini naye hakuwa anajua kitu, alichosema aliwaona watu watatu tu katika ule msiba na watu hao hakupata kuwatambua kiasi hiko mpaka kuongea na kupeana namba za simu.
Lakini katika alichosema kuna jambo nilimsikia likanigusa, aliuita msiba ule msiba wa ajabu na mimi sikufahamu kwanini alisema hivyo, nikatamani kumuuliza lakini haukuwa muda mzuri, nikavunga, nikidhamiria pale nitakapopata muda mzuri basi ntafanya hivyo.
Baada ya maongezi hayo mafupi, Mwenye Nyumba alinitaka niongozane naye pamoja na Mjumbe twende sehemu ya huduma ya matibabu ya serikali kwaajili ya wale wahanga kisha pia tukatoe 'statement' polisi, mimi nikamwambia nimebanwa na shughuli, sitakuwa na huo muda, basi wakaondoka na yule jamaa mwingine mimi nikaendelea na mambo yangu, si kwamba sikuwa na muda kama nilivyosema ila tu sikutaka kujihangaisha na mambo yale kwa huo muda, basi nikatulia hapo nyumbani mpaka majira ya usiku nilipoonana na Mama Tarimo kumuulizia hali ya mumewe kwani ilipita kitambo kidogo sijaenda kumtazama bwana huyo.
Mama huyo akanikaribisha kwa ukarimu, tukaongea mambo mawili matatu kuhusu mgonjwa, nilifurahi kusikia anaendelea vizuri, kwa mujibu wake alisema haitoisha mwezi bwana Tarimo atakuwa amerejea nyumbani.
Mbali na hilo tuliteta kidogo kuhusu swala lile la msiba, jambo hilo lilikuja baada ya mwanamke huyo kugusia mambo ya pesa, hapo akayakumbuka mambo ya zile sarafu, nilimuuliza kama bado anazo akaniambia hajabakiwa nayo hata moja, baada ya mtoto yule kufariki, ile siku ya msiba, usiku wake hakupata tena kuziona zile pesa, na anaamini hamna aliyechukua maana mahali alipoziweka ni chumbani juu kabisa ya kabati.
Alisema, "jirani, yule mtoto naamini atakuwa kaenda na pesa zake. Si uliambiwa hata pale alipokutwa kulikuwa na sarafu za hamsini?"
Nikamjibu kisha nikamuuliza kuhusu siku hiyo maana yeye alikuwa miongoni mwa watu walokuwapo, vyote vilivyojiri hakuadithiwa bali alivishuhudia kwa macho yake.
Mwanamke huyo aliniambia mambo mapya kabisa, mambo ambayo sikukaa nikayadhania lakini mambo ambayo yalinifanya nikapatwa na maswali kadhaa.
Mwanamke huyo alisema, kwa macho yake mawili akiwa dirishani, saa kumi kasoro ya usiku, alimwona yule mwanamke mtu mzima anayekaa na Bembela, yaani yule shangazi, akiwa anazunguka nyumba yetu nzima kwa mbio. Mwanamke huyo alikuwa amevalia kitambaa kifuani, kitambaa kinachofunika kifua chake peke yake na kisha huku chini amevalia kitu kama sketi ama kaniki, hakuiona vema, chini alikuwa peku na mkononi ameshikilia kitu mithili ya kibuyu.
Akiwa anakimbia sasa akawa anapigapiga kile kibuyu huku akiongea mambo ambayo hakuwa anamsikia.
Alinambia: "nilikuwa nimeamka kwaajili ya kujiandaa kwenda hospitali lakini kwa tukio lile na kisha baadae kuona msiba ilibidi kwanza nighairishe mpaka mchana, kwanza niliogopa hata kutoka ndani mpaka nilipoona na kujiaminisha nje kuna watu."
Kwa maneno ya Mama Tarimo, baada ya mwanamke yule kuzunguka mara mbili yeye akiwa anamwona, alipotea mbele ya macho yake, ghafla hakumwona ... kukawa kimya, hata vishindo vya miguu hakuvisikia tena.
Kidogo, kama dakika nne hivi mbele, akamwona Bembela akitoka chumbani mwake na kusimama mbele ya mlango wake, mwanamke huyo alitazama huku na kule kisha kidogo uso wake ukasimama kuangazia kule kibarazani, kidogo tena akamwona yule shangazi akiwa anakuja kinyumenyume kuelekea pale alipokuwapo Bembela, alipomfikia mwanamke huyo, akiwa amesimama vilevile,akamwambia jambo, jambo ambalo yeye hakupata kulisikia,
Aliniambia: "nilimwona Bembela kama vile hakuridhia kile alichoambiwa, alitikisa kichwa chake lakini baada ya kuhimizwa na yule mwanamke mzee kwa muda, akaridhia, alitoka akielekea mwelekeo wa kule kibarazani, sijui alifanya nini huko, lakini punde nikamwona akirudi anakimbia, kabla hajaingia ndani aliangusha kitu pale mlangoni pake, nadhani ilikuwa ni sarafu ya hamsini, lakini hakuangaika nayo, aliishia kuitazama tu akaingia ndani upesi!"
Baada ya hapo, aliwashuhudia watu hao wakiondoka, walikua na haraka mno, na hakupata tena kuwaona mpaka siku ya kikao.
"Nilidhani nikirejea toka hospitali ile usiku ningewakuta lakini hawakuwapo na hawakurejea"
Mwanamke huyo akasema baadae sasa alipotoka kwenda huko nje ndo' akamkuta yule mtoto pale kibarazani, yuko uchi wa mnyama na sarafu zake ziko chini, akajaribu kumwita akiwa amesimama kwa mbali, mtoto yule hakujigusa, ameketi akiwa ameegemea nguzo, baada ya kuita sana bila mafanikio, akarejea ndani na hakutoka tena mpaka watu wengine walipokuja kupata ufahamu ... kumbe mtoto yule alikuwa amefariki.
Walijaribu kugonga mlango wa BIGI lakini hamna mtu aliyetoka wala kuitikia, wakamtafuta mwenye nyumba na kumweleza yaliyojiri, mwenye nyumba akawaambia yuko nje ya mji wafanye jitihada kuonana na Mjumbe, wakafanya hivyo, Mjumbe akafika hapo na baada ya masaa kupita isijulikane cha kufanya, waliuchukua mwili kwenda kuuhifadhi.
Alisema: "sijui kama yule bwana alikuwemo ndani au lah, yawezekana alikuwemo humo, lakini kama ndivyo kwanini hakutoka? Au ndo alikuwa tayari ameshapooza? Lakini mkewe je? Sijui!"
Nikajikuta namwelewa vema huyo mama, kweli hakuna mtu angeweza kuwaelewa wale watu isipokuwa wao wenyewe na Mungu alowaumba, zaidi ungejiumiza tu kichwa kwa mazigazi yao yasokoma.
Maongezi yangu na Mama Tarimo yaliendelea kidogo kwa mama huyo kuniuliza nilipokuwapo muda wote ambao sikuonekana pale nyumbani, na kuniuliza kuhusu zile sarafu ambazo alinipatia, baada ya hapo nikamuaga niende zangu kwangu lakini kabla sijatoka hapo, akaniuliza:
"Wamempeleka wapi yule bwana? ... Au ni kulekule walipoupeleka mwili wa yule mtoto ukapotea?"
Nikashangaa. Kumbe mambo hayakuwa yameisha? Nilimuuliza anamaanisha nini akaniambia habari mpya ya kwamba siku ya pili baada ya kifo cha mtoto yule, Mjumbe alikuja pale nyumbani kuwaambia mwili wake ulipotea kule ulipohifadhiwa, hamna anayekujua ulipokwenda, si mhudumu wa mochwari wala daktari!
Nikajiuliza hali hiyo inawezekanaje? Mwili kupotea mbele ya uangalizi wa mochwari? Mama Tarimo akaniambia mashaka yake na yale aloyoyaeleza Mjumbe.
Alinambia, "wanaume watatu wageni walifika hapa nyumbani kuhani msiba majira ya usiku, hakuna mtu wa hapa nyumbani aliyekuwa anawafahamu ... Wanaume hao walisema wamepata taarifa za msiba hivyo wamefika hapa kutoa pole, hatukujua wametokea wapi na nani aliwapa taarifa hizo, wakakaa kibarazani mpaka majira ya usiku mkubwa kisha wakaenda zao. Hamna aliyejua wapi walielekea na kipi walifanya, na mpaka sasa hatujawahi kuwaona tena! Huenda wanaume hao ndo' walienda kuuchukua ule mwili."
Hayo yalikuwa mawazo ya Mama Tarimo, vile alivyowaza na kudhania na mimi sikuwa na pingamizi juu yake wala lolote la kuongezea. Niliondoka hapo kwake nikiwa na mambo mawili kichwani: moja Bembela aliniongopea kuhusu kile kilichotokea usiku ule na pili waliondoka na zile sarafu za yule mtoto kwenda huko kusikojulikana.
Baadae, nikiwa kitandani nautafuta usingizi, nayatafakari mambo ya hapa na pale, nikapata wazo jingine la kunikosesha raha, hivi hospitali kule walikompeleka BIGI na yule mkewe kutakuwa salama kweli? ... Maana nilijikuta nakumbuka yale nloambiwa pale nilipompeleka mwanamke yule kule hospitali Kawe, Ukwamani, ya kwamba nilimsaidia kwenda kuchukua damu na uhai wa watu, je, vipi kuhusu kule? Nilijiuliza nisipate majibu.
Mara kidogo nikiwa hapo, bado napanga vitu kichwani, nikasikia geti dogo linafunguliwa, majira ni saa tisa usiku, nilikurupuka nikatazama dirishani kuona ni nani anayegusa mlango huo majira hayo, mara nikamwona Bembela na yule mwanamke alosema ni shangazi yake, wanawake hao wanatoka kwenda nje ya uzio.
Wanaenda kufanya nini? Sikujua. Baada ya dakika kumi hivi, wanawake hao walirejea Bembela akiwa amebebelea mfuko mweusi, sijui waliutolea wapi na ulikuwa una nini ndani yake lakini baada ya masiku na majuma kadhaa mbeleni, nilikuja kupata majibu mwenyewe, Bembela aliamua kuuvaa rasmi ushetani kwaajili ya biashara yake ...
Demi