Yule Jirani yangu wa Goba, hakuwa mtu wa kawaida - MWISHO.
Siku mbili baada ya kumwona Bembela akiwa na shangazi yake usiku ule wamebebela mfuko nisijue wapi walipotokea na nini walibebelea, nilipigiwa simu na Mwenye nyumba majira ya mchana nikiwa kazini.
Bwana huyo baada ya kunisalimu na kuniuliza mambo ya nyumbani, aliniuliza kama kuna watu wamefika pale nyumbani kumuulizia bwana BIGI, nikamwambia sifahamu, binafsi sikuona mtu labda wapangaji wengine, baada ya hapo nikamuuliza hali za wale wagonjwa, akanieleza hali zao ni bora ya jana yake, siku hiyo alipitia asubuhi hospitali kabla ya kwenda kwenye shughuli zake akakutana na hali mbaya sana ya bwana BIGI.
Alinambia, "yule bwana sijui sasa kama kuna kupona. Amepooza mwili wake mzima, ni wa kugeuza na kumfuta tu, sasa wanataka kumpatia rufaa!"
Aliniambia hofu yake endapo bwana huyo akifa maana hamjui mtu wake hata mmoja na wala hana mawasiliano nao, achilia mbali hata mkataba naye hana, sijui ataeleza kitu gani akaeleweka mbele ya vyombo vya usalama, lakini pia hata mkewe ambaye alikuwa anategemea atapoa ili amhudumie mumewe na kutoa taarifa kwa watu wao wa karibu naye hali yake haikuwa inaeleweka, tangu amefikishwa hapo hospitali hajapata kuonekana akifungua macho wala kutoa ishara yoyote ya mawasiliano, amepimwa kila kitu, hamna kinachosoma na hitilafu ila fahamu hazimo, ajabu gani?
Aliniaga akiniambia alimwacha yule bwana, mpangaji aloongozana naye siku ile kwenda naye hospitali, baadae atampigia kumuuliza maendeleo, baada ya hapo akakata simu nikaendelea na shughuli zangu.
Kesho yake majira ya jioni nikiwa natoka kazini, nikakutana na huyo mpangaji mwenzangu kwenye geti dogo akiwa anarejea nyumbani, bwana huyo alikuwa ametoka kwenye mihangaiko yake ya hapa na pale, tulisalimiana kisha akanieleza ya kule hospitali.
Bwana yule akaniambia mambo ambayo Mwenye Nyumba hakupata kusema au pengine hakuwa anayajua.
Alisema: "Baada ya leo asubuhi kutoka kule, mimi sitokaa nirudi tena kule hospitali hata mwenye nyumba akiniomba na kunilamba miguu."
Nikastaajabu kweli na maamuzi hayo ambayo niliyaona ya ghafla, kabla sijamuuliza kulikoni, akaniambia mwanamke yule alokuwapo hospitali hakuwa mgonjwa, mwanamke yule ni mzima kila ifikapo usiku, maneno hayo yakanifanya nimuulize: "ushawahi kuwa kule hospitali majira ya usiku?"
Akanijibu "lah!" na kusema kamwe hajawahi lakini alionana, asubuhi ya siku hiyo, na nesi alokuwa anaingia zamu usiku, nesi huyo alimwita kando akamuuliza mwanaume yule yaani BIGI ni ndugu yake? Akamwambia ndio na yule mwanamke ni shemeji yake, basi akamwambia mwanamke yule huenda ndo' amemuadhiri ndugu yake mpaka kufikia vile.
Bwana yule alisema: "nilimuuliza nesi kwanini anawaza hivyo akaniambia yeye ana uzoefu na hayo mambo ya hospitali, anajua mambo ya kutibiwa hospitali na mambo ya kutafuta njia zingine mbadala, na hili la kwetu ni la njia mbadala, tena tufanye upesi kabla hatujampoteza ndugu yetu."
Bwana yule akaniambia nesi huyo alishawahi kumshuhudia mwanamke yule,kama kivuli, akiwa anatembea wodi ya watoto na wazazi nyakati za usiku, na anaamini ni kweli alichoona sio mauzauza ama kiini macho, lakini alipoenda kutazama kitanda chake bado akamkuta mwanamke huyo hapo, mwili wake umetulia kitandani, na jambo hilo si mara moja bali mara mbili.
Ajabu kule kote mwanamke huyo alikokatiza, kesho yake paliongokea msiba ya watoto kwenye vitanda viwiliviwili, kwa siku mbili wakapoteza watoto wachanga wanne!
"Ndugu yangu," bwana yule aliita kisha akasema, "kuanzia leo mimi sitahusika kwa namna yoyote na wale mabwana, hata iweje, yote nimewaachia wale ndugu zao walokuja hapa kuhani msiba."
Nikahamaki,
"Ndugu hao uliwaona?"
Akanambia hapana ila kama walikuja wakati wa msiba basi waje pia na kuwatazama huko hospitali, nikabaini bwana huyo amepandwa na jazba, niliagana naye akaondoka zake, kesho yake asubuhi ya mapema nikiwa najiandaa kwenda kazini mwenye nyumba akanipigia simu, akaniambia amepitia hospitali asubuhi ya siku hiyo akapata taarifa bwana BIGI amefariki dunia!
Alisema: "Kifo chake kimetokea usiku wa kuamkia leo kwahiyo hapa tunapoongea, mwili wake umehifadhiwa."
Kuhusu mkewe, alinambia bado hali yake iko vilevile, hamna afueni wala ahueni, namna alivyoletwa ndo' namna alivyo, lakini kabla hatujamaliza maongezi akaniomba ningoje mara moja atanirejea, akakata simu.
Yakapita masaa kama mawili, hakunipigia, nishafika kazini na ninaendelea na mambo yangu lakini kule nyumbani kabla sijaondoka nilishaacha taarifa ya msiba, baada ya masaa hayo nlosema, mwenye nyumba alinipigia akaniambia muda ule alokata simu, kuna watu walikuja hapo hospitali wakisema wao ni ndugu zake na BIGI, akaniuliza kuna mtu niliyempa taarifa kuwa BIGI yuko hospitalini hapo? Nikamjibu hapana, akasema;
"Basi itakuwa Muddy, nampigia hapokei simu yangu, sijui yuko wapi?"
Muddy ni yule jamaa jirani aloongozana na mwenye nyumba kwenda naye kule hospitali, mwenye nyumba aliponieleza anampigia bwana huyo hampati nikakumbuka moja kwa moja maneno alosema yule bwana jana yake usiku nilipokutana naye, pengine alihisi mwenye nyumba anamtafuta ili aende hospitali, kitu ambacho yeye hakukitaka tena abadani.
Lakini kama ndiye Muddy alisema kuhusu BIGI kuwa kule hospitali, je alikutana na hao majaa lini? Mimi sikuamini kabisa hilo jambo. Na kama kweli hao majamaa wamemjuaje mwenye nyumba ukizingatia mwenye nyumba hata kwenye msiba hakuwapo?
Sikukaa nikayajua.
Baadae jioni niliporejea nyumbani, nilimkuta baba mwenye nyumba akiwa pamoja na Mjumbe, vijana wawili wa ulinzi shirikishi na mabwana wawili ambao sikuwatambua. Tulisalimiana kisha mwenye nyumba akanieleza kinachoendelea hapo ya kwamba mabwana wale wawili ni ndugu zake na BIGI na wamekuja hapo kubeba vitu vyao.
Alinieleza mabwana wale ndo' waliofika kule hospitali kujumuika naye, kama haitoshi, walisimamia kila kitu kuhusu gharama za matibabu na kitanda alicholalia BIGI muda wote ule wa kuuguzwa.
Lakini mimi nikabaki na maswali, sawa mabwana hao wameibuka na kubeba majukumu, lakini tuna uhakika gani kama wao ni ndugu halisi wa BIGI? Nilijiulizia moyoni...
Vitu vyote vya BIGI vilitolewa nje, kweli hakukuwa na cha maana, yaani ungeweza kubeba vitu hivyo kichwani ukaondoka navyo kwa miguu, kulikuwa ni mifuko mifuko, viroba, nguo na mavitu mengine kadhaa ambayo kwakweli sikuona kama yana tija, ajabu ni kwamba mabwana wale hawakubakiza hata kitu, kila kilichochao walibeba, hata yale ambayo unaweza dhania ni taka, yote hayo walikuwa wanakusanyia katika kiroba chao kikubwa walichokuja nacho.
Wakiwa wanafanya hivyo mimi nikaona moja ya 'toy' la mwanangu, nikawaambia hiki ni changu hamna kwenda nacho, hapo ukaibuka mzozo, mabwana wale hawakuwa tayari kuacha kitu, nami kuona vile nikapata mashaka juu ya kwanini wanang'ang'ania vile vitu kiasi hiko, mpango wao ni nini?
Nikapambana mpaka nilipohakikisha 'toy' ile haiendi kokote, swala hilo likawafanya majirani wengine nao wasogee kuziangatia vitu vile vinavyobebwa, hamaki majirani watatu wakapata nguo zao humo, tena wawili kati yao walipata nguo zao za ndani!
Hamna aliyejua ni namna gani nguo hizo zilifika humo, lakini kila mtu alikiri zilipotea kambani baada ya kuanikwa juani. Baada ya kila kitu kuwa sawa, mabwana wale walifunga kiroba chao kisha mmoja wao akasema, tena kwa sauti kuu:
"Kama kuna mtu yeyote mwenye kitu cha (akataja jina halisi la bwana BIGI) basi naomba akirejeshe hapa ... Kama vile mlivyodai vyenu, basi na vya kwake vyote virejeshwe, kama sivyo basi mwenye nacho atakuja kupata matatizo hapo baadae na sisi hatutabeba lawama."
Kimya,
Hakuna kilichorejeshwa, Bwana huyo akarudia tena maneno yake, kama kuna yeyote alowahi kubeba mali yoyote ya bwana BIGI basi airejeshe, la sivyo atakuja kujilaumu.
Kimya.
Mabwana wale walipoona kila kitu ni sawa, wakampatia mwenye nyumba mkono wa kheri na kisha Mjumbe, alafu wakasema msiba wa bwana BIGI utakuwapo maeneo ya Chanika eneo ambalo sikumbuki linaitwaje, baada ya hapo wakaenda zao na kile kiroba chao kikubwa, huo ukawa ndo' mwisho wa BIGI na mambo yake pale Goba. Baada ya hapo sikuwahi kumsikia wala kumwona tena bwana huyo. Sikumbuki kama kuna jirani yoyote aloenda kuhani msiba huo huko Chanika, laiti ingelikuwa hivyo basi ningelipata taarifa fulani.
Ikapita siku moja, siku ya pili, bila ya bwana BIGI, kila kitu kikiwa shwari, wiki moja na wiki ya pili, kila kitu kimetulia, hamna maisha ya usiku wala vimbwanga vyake, baada ya mwezi kukoma Bembela alihama pale nyumbani nisijue wapi alipoelekea, lakini sehemu yake ya biashara ilibakia kuwa ni ileile, nyuma ya kituo cha Goba Kontena.
Hapo mara kadhaa nilikuwa namkuta akiwa anahudumia watu, hata ameajiri wadada wawili wa kumsaidia maana wateja walikuwa wengi sana. Siku moja, nadhani ni baada ya kama mwezi kupita tangu amehama pale nyumbani, nilipita pale katika eneo lake la biashara kumsalimu, siku hiyo nilikuwa mwenyewe nyumbani maana mke wangu alikuwa ameenda huko Ugweno, Kilimanjaro, kwao kusalimu pamoja na mtoto, hivyo nilivyokuwa nikirejea nyumbani nilikuwa napitia hapo kupata chakula cha usiku kabla ya kwenda kulaza mazima ninaposhuka kule Mashuka.
Nilifanya hivyo mara kadhaa, kama majuma matatu hivi, nikikutana na Bembela kila siku na kila mara tukiongea naye mambo ya hapa na pale. Nilishawahi kumuuliza shangazi yuko wapi, akaniambia ameshakwenda zake Tanga lakini anashukuru kwani maisha si haba, kila kitu kinaenda sawa, sasa alikuwa anatazamia kumalizia nyumba yake aliyokuwa anajenga maeneo ya Kimara, Temboni.
Bembela, kwakweli, hakuwa yule Bembela wa zamani, kitendo cha kuajiri wasichana wawili na yeye akiwa wa tatu katika shughuli ile ya mama n'tilie ilionyesha namna gani alivyokua amepiga hatua kubwa kiuchumi.
Ilikuja kufikia pahali hata mimi nilokuwa naenda pale kupata chakula, zamani nikihudumiwa kama mfalme, sasa nikawa napanga foleni tena mpaka niwe nasisitiza mara mbili au tatu ndo' sahani ipate kuja mezani!
Nikatambua kweli maisha yanabadilika, na mengine, kama bahati, yanabadilika mbele ya macho yetu ya nyama, yaani tunapata kuyashuhudia yakiwa yanatokea tangu mwanzo wake mpaka mwisho wake.
Lakini mpaka leo, mimi binafsi, sijawahi kujua ni nini haswa kilichokuja kutokea katikati ya majuma na miezi kadhaa baina ya Bembela na yule shoga yake ... lakini mwanamke yule, yaani shoga yake na Bembela, ambaye tulikuwa tunaendelea kuishi naye pale nyumbani, ndiye baadae alikuja kugeuka kuwa mdomo wa kusema kuwa Bembela anamtumia yule mtoto na mke wa BIGI kwenye mafanikio ya biashara yake.
Sasa amepata mali na pesa, hakuna anayemjali na kumkumbuka, hata yeye alokuwa naye karibu katika yale yote alopitia ....
***