BAADA YA KUCHAGULIWA MWENYEKITI AU
MWENYEKITI wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete amekiri kuwa anakabiliwa na kazi nzito ya kusuluhulisha migogoro katika nchi kadhaa barani Afrika.
Akizungumza na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Dar es Salaam, juzi usiku kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa J.K Nyerere, Dar es Salaam, mara baada ya kuwasili akitokea Addis Ababa, Ethiopia, alisema migogoro imekuwa chanzo kikubwa cha kurudisha nyuma maendeleo ya bara hili.
Ninakabiliwa na kazi moja ngumu ya kushughulikia migogoro kwenye bara letu, imekuwa chanzo kikubwa cha kurudisha nyuma maendeleo yetu kila kunavyokucha, alisema Rais Kikwete.
Alisema kazi aliyopewa ni ngumu, haiwezi kufananishwa na kazi ya urais wa nchi, lakini kwa kushirikiana na kamati mbalimbali za AU, wanaweza kufikia malengo waliyojiwekea.
Kazi hii siyo kama kazi ya urais wa nchi, ni ngumu ambayo naamini kwa ushirikiano wa kamati zetu mbalimbali, ikiwemo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya AU tunaweza kufikia yale tuliyojipangia, alisema.
Alisema anakabiliwa na changamoto nyingi za kupambana na migogoro, ikiwemo ile ya Jimbo la Darfur nchini Sudan, mapigano ya waasi nchini Chad na mvutano wa suala la ushindi wa Rais Mwai Kibaki wa Kenya.
Migogoro yote hii ni mikubwa, imesababisha tumesahau shughuli za maendeleo, yakiwemo ya kukuza viwanda na mambo mengine, alisema Rais Kikwete.
Alisema AU inakabiliwa na kazi nyingine ngumu baada ya kundi la waasi kutaka kumuondoa madarakani rais wa Chad na kuwa jukumu hilo amekabidhiwa Rais wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi.
Alisema katika mkutano wa Addis Ababa, viongozi hao wamekubaliana kwa dhamira moja ya kuinua maisha ya wananchi wao na kuepukana na mapigano ya mara kwa mara.
Rais Kikwete alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa AU wiki iliyopita baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa umoja huo, Rais wa Ghana, John Kuffour kumaliza muda wake.