Date::10/30/2008
Kashfa ya EPA: Macho ya Watanzania kuelekezwa kwa Rais Kikwete
Na Ramadhan Semtawa
Mwananchi
RAIS Jakaya Kikwete leo atahutubia taifa katika siku aliyoiweka kuwa ya mwisho kwa wote waliochota fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kuwa wamesharejesha fedha, huku joto kwa waliochota fedha hizo likiwa limepita kiwango cha kawaida.
Mafisadi hao waliiba Sh133 bilioni kutoka kwenye akaunti hiyo na ni kiasi cha Sh61 bilioni zilizokuwa zimeelezwa kuwa zimesharejeshwa wakati Rais Kikwete aliagiza kuwa yule ambaye atakuwa hajarejesha ifikapo leo, apandishwe kizimbani ifikapo Novemba mosi.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana haielezi kuwa Rais Kikwete atazungumzia masuala gani hasa kwenye hotuba yake ya leo, lakini kuna uwezekano mkubwa akazungumzia suala hilo ambalo limeifanya serikali yake irushiwe maneno machafu, kukosolewa, na kukebehiwa kuwa haijachukua hatua madhubuti kukabiliana na wezi hao.
"Katika hotuba hiyo, mheshimiwa Rais atazungumzia masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya kijamii na kiuchumi kama yalivyojitokeza katika kipindi kilichopita hapa nchini na nje ya nchi," inasema taarifa ya iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais.
Duru za kiserikali zilidokeza kwamba, timu ya rais ya kuchunguza ufisadi huo, inayoundwa na vigogo, jana ilijichimbia katika moja ya maeneo nyeti jijini Dar es Salaam ikihitimisha kazi yao, huku baadhi ya akaunti za vigogo waliotumia mgongo wa vibarua wao kuiba mabilioni hayo, zikiwa zimefilisiwa.
Ufisadi wa EPA unahusu wizi wa Sh90.3 bilioni ambazo zilichotwa na makampuni 13 kwa kutumia nyaraka za kughushi na Sh42.6 bilioni zililipwa kwa makampuni tisa, ambayo uhalali wa malipo ndiyo umejaa utata huku taarifa nyingine zikiwa nje ya nchi, hali iliyomfanya Rais Kikwete kuongeza muda wa uchunguzi kutoka Agosti hadi leo Oktoba 31.
Wakati akihutubia kwa njia ya televisheni na redio, Watanzania watakuwa wakisubiri kwa kujua mbivu na mbichi katika sakata hilo na fedha zilizorejeshwa kutoka kinywani mwa mkuu huyo wa nchi kuhusu utekelezaji wa agizo lake la Agosti wakati akihutubia bunge, mjini Dodoma.
Hata hivyo, taarifa ya aya mbili ya Ikulu iliyotolewa jana jioni na Kurugenzi ya Mawasiliano haikueleza kama Rais Kikwete atazungumzia EPA.
Wakati taarifa ya Ikulu ikiweka fumbo katika hotuba ya rais, Watanzania wangependa kusikia na kuona mkuu huyo wa nchi akieleza utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa bungeni baada ya kusema mafisadi wa EPA wana hali mbaya ingawa wanavaa makoti na tai.
Katika hotuba hiyo rais pamoja na kuzungumzia mambo mbalimbali pia alitoa muda wa miezi mitatu kutoka Agosti hadi leo Oktoba 31 kwa watuhumiwa wote walioba fedha hizo wawe wamezirejesha, vinginevyo kesho Novemba mosi wawe mahakamani.
Rais katika kauli yake ambayo ni nzito kutokana na madaraka yake makubwa aliyonayo kikatiba kuweza kushughulikia mtu yeyote ipasavyo, ndiyo inafanya Watanzania kuwa na shauku ya kujua utekelezaji wake.
Maswali mawili makubwa yanayojitokeza siku ya leo ni kuona kama kiasi chote cha fedha ambazo zilibaki baada ya kukusanywa Sh53.9 bilioni katika awamu ya kwanza, zitakuwa zimepatikana na pili, hatua zitakazochukuliwa kwa watu ambao watakuwa hawajarejesha fedha.
Hata hivyo, siku ya leo pia inaangaliwa kwa upana zaidi kuona kama serikali ni kweli ilikuwa imeweka mtego kwa watuhumiwa ili warejeshe fedha kisha kiwe kidhibiti cha kuwaburuza mahakamani ama la.
Ingawa Rais anaweza kuzungumzia mambo mbalimbali ikiwemo mjadala wa Tanzania kujiunga au kutojiunga na Jumuiya ya nchi za Kiislam Duniani (OIC), bado suala la EPA ndilo kubwa zaidi katika kipindi hiki na hasa siku ya leo ambayo Rais Kikwete aliagiza kuwa ndio iwe mwisho ya huruma yake kwa wezi hao.
Wakati macho na masikio yakiwa kwa Rais, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora Sophia Simba, aliwataka Watanzania kuwa na subira, huku mwanasiasa mkongwe nchini na Naibu Gavana wa zamani wa BoT, Bob Nyanga Makani, akisema kuwa leo ndio ukweli au usanii wa serikali utajulikana.
Akizungumzia zaidi uchunguzi huo, Waziri Simba alisema muda umekwisha hivyo iachwe timu imalize kazi kisha ikabdhi ripoti kwa Rais ambaye ataeleza umma kwani hakuna cha kufikisha.
"Ipo timu ya rais ilikuwa inafanya kazi, hebu watu wavute subira, kwani siku si zimekwisha... sasa kuna nini tena na wakati Rais ataeleza," alihoji Waziri Simba na kuongeza kuwa akiwa ni waziri mwenye dhamana ya utawala bora, anaheshimu timu ya rais na kwamba kila kitu kitaiabinika katika muda mfupi ujao.
Naye Makani, ambaye pia aliwahi kuwa naibu mwanasheria mkuu wa serikali katika awamu ya kwanza, alisema alishangaa, anashangaa na atashangaa zaidi iwapo tuhuma hizo za wizi wa fedha za EPA zitazidi kufanywa kuwa madai badala ya jinai.
Makani, ambaye ni mtu aliyewahi pia kushika nyadhifa mbalimbali za ujumbe na uenyekiti wa bodi mbalimbali za mashirika na taasisi za umma, alisema kilichofanyika BoT ni jinai na kwamba matumaini ya Watanzania ni kuona watu wanakamatwa.
"Si tuhuma za madai zile, ni makosa ya jinai, watu wameiba fedha huwezi kuwafanyia kesi ya madai," alisema Makani na kuongeza:
"Lakini siku si zimekwisha! Kuna kitu gani... hebu tumsubiri Kikwete tuone atafanya nini kama alivyosema mwenyewe, tusimhukumu kabla."
Duru za kiserikali zinasema baadhi ya akaunti za vigogo wa makampuni yaliyochota mabilioni hayo kwa mgongo wa wafanyakazi wadogo, zimeweza kuchunguzwa na fedha kuchukuliwa.
Taarifa hizo zinasema kukamatwa kwa akaunti za vigogo hao kunatokana na kuangalia mzunguuko mzima wa fedha kutoka malipo yaliyofanywa BoT hadi zilizoishia.
"Hawa watu walitumia wafanyakazi wao kusaini fedha, lakini uchunguzi uliona mwisho wa fedha ziliingia katika mikono ya vigogo kwa kuingia katika akaunti zao," kilidokeza chanzo huru kutoka duru za kiserikali."
Kwa mujibu wa duru hizo, iwapo rais ataamua kutumia mamlaka yake kufikisha wote waliohusika mahakamani, basi kuna vigogo ambao ni wafanyabiashara wakubwa, mawakili maarufu na baadhi ya maafisa wa serikali, watakumbwa na zahama hiyo.
Ufisadi wa EPA ulibainika katika hesabu za BoT za mwaka 2005/06, baada ya ukaguzi uliofanywa na kampuni ya Ernst& Young, ambayo ilipewa kazi iliyoachwa kiporo na Deloitte&Touche ya Afrika Kusini iliyositishwa ghafla kuendelea na ukaguzi huo.
Kampuni hiyo ya Afrika Kusini ilisitishwa baada ya kubaini ufisadi wa Sh40 bilioni zilizochotwa na Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.
Baada ya Deloitte &Touche kuzuiwa kuendelea na kazi, mwaka jana serikali mwaka jana ilimwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutafuta kampuni ya kimataifa, kufanya ukaguzi huo kubaini ukweli.
Ofisi ya CAG iliteua kampuni hiyo ya kimataifa ya Ernst&Young, ambayo ilibaini ufisadi wa fedha hizo zaidi ya sh 133 bilioni, ambazo zilichotwa na makampuni 22.
Makampuni 13 yalijichotea sh 90.3 bilioni, ni pamoja na Bencon International LTD of Tanzania, Vb & Associates LTD of Tanzania, Bina Resorts LTD of Tanzania, Venus Hotel LTD of Tanzania, Njake Hotel &Tours LTD, Maltan Mining LTD of Tanzania.
Mengine ni Money Planners & Consultants, Bora Hotels & Apartment LTD, B.V Holdings LTD, Ndovu Soaps LTD, Navy Cut Tobacco (T) LTD, Changanyikeni Residential Complex LTD na Kagoda Agriculture LTD.
Kwa upande wa makampuni tisa yaliyochota Sh42.6 bilioni ni pamoja na G&T International LTD, Excellent Services LTD, Mibale Farm, Liquidity Service LTD, Clayton Marketing LTD, M/S Rashtas (T) LTD, Malegesi Law Chambers (Advocates), Kiloma and Brothers na KARNEL LtD.
Makampuni mengine mawili ambayo ni Rashtas (T) na G&T International LTD, kumbukumbu zake ikiwemo nyaraka za usajili katika daftari la Msajili wa Majina ya Makampuni na Biashara (BRELA), hazikuweza kupatikana.
Kufikia mwaka 1999 deni katika EPA lilifikia dola 623 milioni, ambazo kati ya hizo dola 325 milioni zilikuwa ni deni la msingi na dola 298 ni riba na kisha baadaye deni likaongezeka hadi kufikia dola 677 milioni.
Hata hivyo, chini ya Mpango wa Kununua Madeni (Debt Buy Back Scheme) wa mwaka 1994 kati ya serikali na Benki ya Dunia (WB), waliokuwa wanaidai BoT waliombwa wakubali kulipwa sehemu tu ya fedha wanazodai, wapo waliokubali na wengine kukataa na kuongeza hadi mwaka 2004 taarifa zinaonyesha jumla ya dola 228 zililipwa chini ya mpango huo.
EPA ni akaunti ya madeni ambayo ilitumika wakati wa Mfumo wa Ujamaa, ambayo akaunti yake ilikuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) chini ya usimamizi wa BoT.
Mwaka 1985, EPA ilihamishiwa moja kwa moja BoT na ndipo mwaka juzi kulipoibuka utata wa tuhuma za ufisadi katika akaunti hiyo kwa mahesabu ya mwaka 2005/06, ambayo utata huo ulisababisha Ernst&Young kufanya ukaguzi kuanzia Septemba sita na kukabidhi ripoti yake kwa CAG mapema Desemba mwaka jana.