Reli Dar - Kigali kumaliza tatizo la usafirishaji
THURSDAY, 17 MARCH 2011 18:52 NEWSROOM
Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amefungua mkutano wa wawekezaji wa mradi wa ujenzi wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Kigali, Rwanda ambapo amesema hatua hiyo itamaliza tatizo la usafiri na usafirishaji wa njia ya reli nchini. Alisema mpango huo utatekelezwa chini ya miaka minne na kwamba ni mwelekeo wa kumaliza kero ya usafiri katika mikoa inayotegemea reli hiyo kwa usafiri na usafirishaji.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, ujenzi wa reli hiyo utalazimisha serikali kupanua bandari ya Dar es Salaam na kuifanya kuwa ya kisasa na uwezo mkubwa wa kupokea mizigo.
"Hii sasa inaashiria kuwa hata bandari yetu ni lazima tuipanue ili iwe kubwa na ya kisasa itakayoweza kuhudumia mizigo mingi ambayo itaongezeka".
Awali, akifafanua kuhusu ujenzi huo, Waziri wa Uchukuzi Omar Nundu, alisema mkutano huo utapendekeza moja kati ya aina tatu za reli itakayotoka Dar es Salaam kwenda Burundi na Rwanda.
Nundu alizitaja aina zinazoshauriwa katika ujenzi huo kuwa ni kujenga nyingine mpya kwa kuweka tuta tofauti na lililopo sasa, litalogharimu dola za Marekani bilioni tano zaidi ya sh. trilioni 7.5 hadi kukamilika.
Nyingine ni kujenga reli pembeni mwa iliyopo itakayogharimu dola za Marekani bilioni 3.54 (zaidi ya sh. trilioni 4.7), na ya tatu ni kuiimarisha iliyopo kwa kujenga laini mbili pembeni mwake kwa gharama ya dola za Marekani bilioni 3.61 (zaidi ya sh. trilioni 4.6).
Kwa mujibu wa Nundu, aina hizo zinalenga kuifanya reli hiyo kuwa ya kisasa zaidi na kuwezesha kuruhusu kupita treni za kisasa zenye uwezo mkubwa zaidi.
"Ninachosema ni kwamba tukianza ujenzi, wananchi wategemee katika kipindi kisichozidi miaka minne reli itakuwa ya kisasa kabisa," alisema waziri Nundu.
Waziri huyo alisema mkutano huo wa jukwaa maalumu la wawekezaji wadau wa reli hiyo, utachagua moja ya aina tatu itakayokuwa rahisi katika utekelezaji ili ifanyiwe kazi.
Alisema tayari Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeshatoa fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa reli hiyo.
Miongoni mwa walioshiriki mkutano huo ni pamoja na Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Vicent Karega, Waziri wa Usafiri wa Burundi, Said Kibeya, mabalozi makatibu wakuu na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.