BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,591
- 8,826
Akielezea kuhusu wagonjwa wa moyo wanao pokelewa katika taasisi hiyo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. Dk.Peter Kisenge, anasema kwa siku wanawaona wagonjwa wastani wa 400, wengi wao huwa tayari moyo umefikia hatua ya kutokutenda kazi vizuri au misuli imeshatanuka.
Anasema katika utendaji wao wa kazi, wamebaini uwepo wa watoto wenye matundu kwenye moyo, lakini wazazi hawana uelewa kuhusu ugonjwa huo, hivyo wanawaomba wazazi kupeleka watoto kufanyiwa uchunguzi, pindi wanapoona dalili kama za kuumwa kifua, kukohoa kila mara ,mtoto anashindwa kukua vizuri na anachoka sana anapocheza na wenzake.
Katika kusogeza huduma kwa wananchi, timu ya madaktari kutoka taasisi hiyo wameanza kutembelea mikoa mbalimbali kutoa huduma, ikiwa ni hatua ya kusaidia wananchi kupata huduma karibu, ikiwamo ushauri wa kiafya.
"Mfano tumeenda Geita tumegundua watoto 37 wenye matatizo ya matundu kwenye moyo na wazazi wao walikuwa hawajui, sisi tumewaambia wawalete Jakaya Kikwete, tunaweza kuyaziba na mtoto anapona kabisa,” anasema Dk.Kisenge.
Pia, anafafanua kuwa endapo watu wakifanya vipimo angalau mara moja kwa mwaka kujua afya zao, inasaidia kubaini matatizo mapema na kupunguza madhara makubwa pamoja na gharama za matibabu ambazo kwa wastani inafika Sh. milioni 25 hadi 45, pale mtu anapopelekwa kutibiwa nje ya nchi.
Anaeleza, kwa sasa serikali imeboresha kwa kiasi kikubwa huduma katika taasisi hiyo, hivyo imewezesha asilimia 96 ya wagonjwa wa moyo kutibiwa nchini na asilimia nne tu ndio hupelekwa nje ya nchi wakati wakitibiwa na inawagharimu wastani wa shilingi milioni 15.
Dk.Glory Manyangu wa Magonjwa ya Moyo, kutoka Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando, anasema jamii inatakiwa kuzingatia maisha ya kawaida, ambayo mtu akiyafuata inamsaidia kujikinga na magonjwa kama kiharusi, kupumua, moyo, kichwa,ubongo na figo.
Moja ya njia ni bora za kukabili anataja inajumuisha kula chakula bora, kuacha kutumia bidhaa za tumbaku, kufanyisha mwili kazi na kupima kila mara sukari, shinikizo la damu na wingi wa lehemu kwenye damu yake.
Vilevile anasistiza watu wanapaswa kutumia kiasi kidogo cha mafuta, ili kupunguza lehemu kwenye damu na kuzingatia aina ya mafuta anayotumia pamoja na kupunguza matumizi ya vyakula vyenye sukari, akisema theluthi ya wagonjwa wa kiharusi na magonjwa ya moyo, husababishwa na shida ya lehemu kwenye damu.
Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza, Varelia Milinga, anasema kutokana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza wanaendelea kuelimisha jamii kuachana na tabia zinazo changia magonjwa hayo pamoja na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya utakaoboresha utoaji huduma.
Pia, anasema mwaka ujao wanalenga kufanya utafiti utakaotambua idadi ya Watanzania wenye aina fulani ya ugonjwa pamoja na kubaini idadi ya wanaotumia tumbaku na vileo hatua itakayo wezesha kuchukua hatua za kudhibiti kulingana na ukubwa wa tatizo.
Anasema hadi sasa mpango huo wamefanikiwa kuandaa mtaala wa mafunzo kwa watoa huduma ngazi ya vituo vya afya na zahanati ambako huduma hizo zilikuwa hazitolewi moja kwa moja lakini kwa sasa huduma hizo zinatolewa kwani kuna watoa huduma wenye elimu ngazi ya shahada katika vituo vya afya na Zahanati.
Mratibu wa Utafiti na Machapisho Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, James Kengia, anasema mwaka 2022 /2023 wameratibu kwa nchi nzima afua zote muhimu za magonjwa yasiyo ambukiza zinazo pelekwa kwenye halmashauri zote.
Anaeleza takribani shilingi bilioni 3.3 zilitengwa kwenye bajeti hiyo, kwa kuzingatia hali halisi ya tatizo katika eneo husika ikiwa ni pamoja na kuratibu uwepo wa huduma zote muhimu kama huduma tiba na kinga kwenye vituo pamoja na utoaji elimu katika jamii ili kutoa uelewa utakao saidia kupunguza ongezeko la magonjwa yasiyo ambukiza.
NIPASHE