Mimi nilifuatilia kwa karibu mjadala huu juu ya katiba; kuna msikilizaji mmoja alichangia kitu ambacho ni muhimu sana katika kufanikisha kupata katiba itakayotuletea maendeleo nacho ni kwamba utashi wa kisiasa wa kupata katiba huru ni muhimu sana hasa kwa Tanazania ambapo wananchi wengi hawana uelewa tosha wa masuala haya. Utashi huu wa wanasiasa usipokuwepo tunaweza kujikuta inafanyika referundum na majority wakasema wanaitaka hii iliyopo iendelee simply because hawana uelewa!! Tukumbuked tu referundum iliyofanyika juu ya kuwa na vyama vingi vya siasa au kuwa na kimoja , majority walisema hawakutaka multipartism; ilikuwa nguvu za hoja na vision ya Nyerere ndiyo iliyotufanya tukawa na vyama vingi vya siasa!! Unfortunately, na hiyo ndiyo hatari itakayoikabili referundum juu ya katiba kuwa hatuna viongozi wa aina ya mwalimu kwa wakati huu.
Ndinani
Wakati nakubaliana nawe kama nilivyokubaliana kwa kiasi aliyepiga simu kuhusu haja ya dhamira ya kisiasa, niweke angalizo kuwa hatupaswi kutumia kinachoitwa 'uelewa mdogo wa wananchi kuhusu masuala ya katiba' kuzima hoja ya mabadiliko makubwa ya katiba (katiba mpya).
Ripoti ya tume ya Nyalali isisomwe tu kwenye mstari mmoja kuwa asilimia 80 walikataa mfumo wa vyama vingi bali isingatiwe kuwa ripoti hiyo hiyo imeeleza kwamba asilimia kubwa kati ya hao 80 % walitaka mabadiliko makubwa ya kimfumo ambayo hayangewezekana kwenye mfumo wa chama kimoja.
Kwa hiyo Nyerere pamoja na kupata msukumo wa nje alisukumwa pia na mwamko mkubwa ambao wananchi walionyesha bayana kuhusu mfumo wa kisiasa. Nyerere alilifahamu hilo vizuri miaka hiyo ya 90 kwa kuwa alishalikabili vuguvugu la miaka ya 80 mwanzoni kabla ya kung'atuka kwake.
Hivyo, hata hili la katiba mpya- pamoja na kuwa wananchi wengi hawawezi kunukuu vifungu vya katiba vyenye mapungufu wanajua udhaifu wa katiba kwa kuonja madhara ya udhaifu wenyewe na wana matumaini ya kutaka kuandaa mkataba mpya kati ya wananchi na serikali (soma watawaliwa na watawala) ili kulinda haki zao za msingi za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa maendeleo ya taifa.
Tukiingia katika mtego wao, watasema kwamba kabla ya kudai mabadiliko ya katiba tuenze kwanza kuelimisha umma kuhusu katiba hivyo ajenda ya mabadiliko isubiri kwanza miaka kadhaa ya elimu kwa umma. Utakumbuka kwamba tume ya Kenya ya marekebisho ya katiba iliundwa kwa sheria ya bunge na sanjari na mchakato wa mabadiliko ya katiba ilipewa pia dhima ya kutoa elimu kwa umma; hawakusubiri kwanza elimu ndio mchakato uanze; walianza mchakato ukiambatana na elimu.
Ukisoma ripoti ya Kisanga, pamoja na kuwa serikali ilitumia mfumo wa White Paper badala ya Green Paper na kutanguliza msimamo wa serikali ili kuathiri maoni ya umma bado kuna maoni ya msingi ambayo wananchi waliyatoa yanayoonyesha ufahamu wa mahitaji kuhusu katiba ya namna gani wanaitaka.
Tuendelee kujadiliana
JJ