John Mwakangale ni mzaliwa wa kwanza kati ya watoto tisa kwenye familia ya Jesaya Bupimba Mugogo na Jeni Malakalinga, walioishi Makandana, Tukuyu, Wilaya ya Rungwe wakati huo Mbeya ikiitwa Mkoa wa Southern Highland.
Mwakangale, ni mwanaharakati wa haki za binadamu, mwanasiasa, mkulima na Daktari wa Mifugo, ambaye kabla ya kujiunga na siasa na kuungana na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Kwanza wa Tanzania, kwenye harakati za kutafuta uhuru wa Tanganyika, alikuwa mtumishi wa umma, aliyehitimu mafunzo kwenye chuo cha Mpwapwa, mkoani Dodoma.
John Mwakangale, alipata elimu ya msingi shule ya Tukuyu kuanzia mwaka 1931, darasa la kwanza hadi nne. Kutokana na kufanya vyema darasani na kushika nafasi za juu alichaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari shule ya Malangali, kuanzia Septemba 1935 hadi Novemba 1941.
Kisha alijiunga darasa la tano hadi la 10 ikiwa ni mfumo wa elimu ambao ulitumiwa kwa wakati huo kabla ya uhuru, uliorithiwa kutoka kwa wakoloni.
Alipohitimu masomo, mwaka 1955 alikwenda nchini Uingereza kujiunga na mafunzo ya serikali za mitaa na utawala, kwenye chuo cha Riding County Council Yorkshire, na kisha baadaye akajiunga na chuo cha Balham and Tooting College, jijini London, akisomea sheria, kuanzia Januari 1956 hadi Juni mwaka huohuo.
HARAKATI ZA UKOMBOZI
Unapozungumzia uhuru wa Tanganyika, hukosi kumtaja John Mwakangale ambaye alikuwa begabega na Mwalimu Julius Nyerere, ambao ni wanaharakati wa ukombozi Afrika, waliomuunga mkono, hukosi kumtaja John Mwakangale.
John Mwakangale kama alivyozoea ama kuzoeleka kujiita JBM, alimaanisha ufupi wa jina lake na zaidi auliutumia ufupisho huo, kama alama hata kwenye saini yake.
Mtoto wa kwanza wa John Mwakangale, Stephen Mwakangale, akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nanenane mwaka huu, jijini Mbeya, alisema baba yake alikuwa mwanasiasa akiwa karibu na Mwalimu Nyerere, na kwamba alikutana na wanasiasa na wanaharakati maarufu barani Afrika, akiwamo Nelson Mandela, aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini.
"Lengo la kuonesha kumbukumbu za John Mwakangale, ni kuhamasisha na kuitithisha jamii mazuri ambayo yalifanywa na waasisi wa taifa letu, kwa kutambua mchango wao kabla na baada ya uhuru. Mchango wao kwenye kilimo, siasa na uchumi unapaswa kukumbukwa kizazi hiki a kijacho.
"Ametambuliwa na viongozi tofauti maarafu. Nelson Mandela, kwenye kitabu chake kiitwacho 'LONG WALK to FREEDOM' amemuelezea John Mwakangale, na namna alivyompokea mkoani Mbeya mwaka 1962, kabla ya Mandela kwenda Addis Ababa, Ethiopia kushiriki mkutano wa Muungano wa Ukombozi Kusini na Mashariki mwa Afrika (PAFMECA)," alisema Stephen.
Alisema kwamba kabla ya uhuru, baba yake alikuwa mwajiriwa na mwanataaluma katika mifugo yaani daktari wa mifugo ilikuwa fani yake na kisha baadae aliamua kujikita na siasa na mwaka 1956 na alijiunga na Tanganyika African National Union (TANU) akishika nafasi ya Katibu wa Mkoa.
"TANU ilipozaliwa kulikuwa na wakereketwa wengi kisiasa akiwamo baba, Nyerere, Joseph Kizurira Nyerere (mdogo wa mwalimu Nyerere), Kissoky na wengine wengi, ambao walijikita katika ukombozi hata kwa za Kusini barani Afrika," alisema Stephen.
Alisema kuwa PAFMECA, John Mwakangale, alishiriki harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika na TANU ilipoasisiwa alichaguliwa na kuonyesha mchango mkubwa kisiasa na harakati hizo ilimfanya kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO) mwaka 1957.
"Uhusiano wa baba yangu (John Mwakangale) na Mwalimu Nyerere, unakuwapo kwa sababu ya shughuli walizofanya ziliendana, siasa, kuwa mwana TANU pia Nyerere hivyo hivyo, na baada ya Uhuru wa Tanganyika, Nyerere akawa rais wa Tanzania, aliendelea kumteua kwenye nafasi za kitaifa na Mkoa mara kadhaa, akijua atamwakilisha vyema kwa wananchi," alisema.
Alisema kwamba, mwaka 1962, John Mwakangale, alikuwa Mkuu wa Mkoa Nyanda za Juu Kusini na mwaka uliofuata aliteuliwa na rais (Nyerere) kuwa Junior Minister of Local Government and Housing, pia akawa Mkuu wa Mkoa Dodoma mwaka 1964.
"Alishirikiana na Mohammed Kissoky, Fatma Mwashambwa, Binti Matola. Kwa ujumla Kusini mwa Afrika nchi kadhaa zilikuja Tanzania kabla na baada uhuru, na baba akiwa mwenyeji wao na baadhi walilala nyumbani mwetu Makandana, Tukuyu (Mbeya). Kulikuwa na cross borders, Malawi, Zambia, Afrika Kusini, kote huko.
"Nakumbuka waliishi vizuri hadi mwisho, marafiki wa kweli tangu ujana wao. Nakumbuka mwaka 1967 nikiwa likizo nikisoma chuoni Nairobi, baba ( John Mwakangale) akaniambia anatakiwa kuuza sehemu yake ya mali, nikamjibu ukiwa kutoka moyoni mwako unakubaliana na hilo na Azimio la Arusha, uza, na kweli akauza. Kwa hiyo alikuwa mzalendo mkweli."
"Kimsingi alikuwa muwazi, mkali na msimamo, alisimamia alichokiamini. Ndio maana walielewana na Nyerere na alimuamini," alisema Stephen na kuongeza:
"Mavazi yake (John Mwakangale) alikuwa anavaa mchanganyiko, suti ilikuwa vazi rasmi. Ila walivaa zaidi Kaunda Suti na zile kama za Mao (chuenlai), ni kama wote (na Nyerere) walikuwa na msimamo mmoja katika mavazi."
Pia, alisema kwamba mwaka 1990, wakati Nelson Mandela alipozuru Tanzania, mara baada ya kutoka kifungoni, alipowasili Dar es Salaam, John Mwakangale alikuwa miongoni mwa wageni wa kitaifa walioalikwa kumlaki Mandela, akiwa rais wa Afrika Kusini.
Kadhalika, alisema mwaka 1999 wakati Nelson Mandela alipofika kuwaaga Watanzania, mkoani Dar es Salaam, kati ya wageni waalikwa, Mandela alioomba awe na orodha ya wageni wake maalumu siku hiyo na kukutana nao kwenye hafla ya kumuaga, akiwamo John Mwakangale.
"Alipewa mwaliko huo na mwanaharakati huyo (Nelson Mandela), akifahamika zaidi kama 'Madiba' kutoka Afrika Kusini, aliyeacha historia na alama kubwa ya ukombozi barani Afrika na duniani," alisema Stephen.
KIFO CHAKE
Januari, mwaka 2002, John Mwakangale alifariki dunia nyumbani kwake Nditu, Wilaya ya Rungwe huku aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa, akituma salamu za rambirambi na kuandika barua kwa familia kuwafariji.
Vifo kati ya Mwalimu Nyerere na John Mwakangale, havikupishana sana, vilipishana miaka mitatu tu, kwani Mwalimu Nyerere alifariki mwaka 1999 na John Mwakangale mwaka 2002.
Wakati Mwalimu Nyerere, akitimiza miaka 24, tangu kifo chake pia John Mwakangale, ametimiza miaka 21, tangu alipofariki nyumbani kwake Nditu wilayani Rungwe, mkoani Mbeya.
HISTORIA YA NANENANE
Uwanja wa Maonesho ya Nanenane uliopo Uyole jijini Mbeya, kupewa jina la John Mwakangale, ni kumuenzi kiongozi huyo.
Chama cha Kilimo Tanzania (TASO) kilichokuwa na jukumu la sekta ya kilimo, kiliandaa maonesho ya na Kikanda na kufanyika kwa Nyanda za Juu Kusini na ikaamuliwa kushirikisha mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Katavi, Rukwa, Songwe na Ruvuma, wakaamua kuyaweka hapa Mbeya kikanda. Ila ikawa mjadala ni suala kupata jina jipya.
Mkutano huo ulipendekeza majina mengi ila Mkuu wa Mkoa wa wakati huo (miaka ya 1990), alipendekeza jina la John Mwakangale, kwanza akisema alikuwa Mbunge wa Nyanda za Juu Kusini kwa muda mrefu na aliyekuzwa na harakati nyingi za kitaifa, kimataifa na mkoa, na ikaamuliwa apewe heshima hiyo.
Maonyesho ya Nanenane yalianza kabla ya nchi kupata Uhuru ambayo yalifanyika ngazi ya Wilaya na Mikoa. Mfano ‘Nyamwezi Agricultural Show’ yalifanyika miaka ya 1949 hadi miaka ya 1950 katika mikoa ya Kanda ya Ziwa; Mwanza, Tabora na Shinyanga, wakulima na wafugaji walionesha bidhaa zao.
Baada ya Uhuru mwaka 1961, shughuli ya Maonyesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima, ziliendelea kuwapo na baadae kujulikana kama Maonyesho ya Sabasaba.
Katika kipindi cha Maonesho ya Sabasaba (wakati huo) mapungufu mengi yaliyojitokeza ni pamoja na kushindwa kufikisha teknolojia mbalimbali za kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima na wadau wengine ipasavyo na pia yalikuwa na sura ya kutoa zawadi tu kwa washindi bora wa Vijiji, Wilaya, Taasisi na Mashirika ya umma.
Oktoba 20, mwaka 1992, Wizara ya Kilimo iliitisha Kikao mkoani Arusha na iliridhiwa kuanzishwa kwa Chama cha Kilimo Tanzania (Tanzania Agricultural Society Organisation -TASO) maalum kwa ajili ya kuratibu Maonyesho ya Kilimo.
Mwaka 1993 kwa mara ya kwanza, TASO iliratibu maonesho ya kilimo yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Mbeya kwenye uwanja wa Uyole ambao kwa sasa unaitwa Uwanja wa Maonesho ya Kilimo wa John Mwakangale.
Vilevile mwaka 1994, TASO iliratibu Maonesho ya Pili ya Kilimo yaliyofanyika Kitaifa yalifanyika Morogoro kwenye uwanja wa Tungi ambao kwa sasa unaitwa Uwanja wa Maonyesho ya Kilimo wa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
TASO kwa kushirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo, Mifugo na wadau wengine waliratibu Maonesho ya Kilimo Kitaifa katika viwanja vya Maonesho ya Kilimo vya Kikanda. Viwanja hivyo ni; Themi mkoani Arusha; Mwl. J.K.Nyerere-Morogoro; John Mwakangale-Mbeya; Nzuguni- Dodoma na Ngongo Mkoa wa Lindi.
NANENANE 2023
Maonesho ya Nanenane yanafanyika kitaifa jijini Mbeya, kwenye viwanja vya John Mwakangale na kauli mbiu ya mwaka huu ni; Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula.
Chanzo: Mwananchi