SoC01 John Pombe Magufuli, Rais aliyeacha alama kwenye mioyo ya wanyonge na kuacha kovu kwenye kidonda cha Katiba

SoC01 John Pombe Magufuli, Rais aliyeacha alama kwenye mioyo ya wanyonge na kuacha kovu kwenye kidonda cha Katiba

Stories of Change - 2021 Competition
Joined
Sep 6, 2021
Posts
24
Reaction score
111
Na Elivius Athanas.

Ni takribani miezi mitano na siku ishirini na nne (24) sasa, tangu hotuba ya dharura ya Rais Samia Suluhu Hassan itutoe machozi Watanzania, alipokuwa akitangaza kifo cha Rais wetu mpendwa Dr. John Pombe Magufuli aliyefariki Jumatano jioni tarehe 17.03.2021 kwa tatizo la moyo. Vilio, simanzi, butwaa na utulivu vilitamalaki maeneo yote ya nchi wasiamini kilichotokea. Nchi ilitulia tuli! Mioyo ilipasuka pa! Vituo vyote vya redio na runinga, vya ndani na nje, vilitangaza msiba huu wa Tanzania. Siyo BBC siyo TBC, siyo DW siyo Wasafi, wote walitupasha habari za kifo cha Dr. John Pombe Magufuli.

Baada ya utangulizi huo wenye hisia na mitindo ya uandishi, nijielekeze sasa katika kukifafanua na kukitolea hoja kichwa cha mnakasha (thread) hapo juu kinachosomeka "John Pombe Magufuli, Rais aliyeacha alama kwenye mioyo ya wanyonge na kuacha kovu kwenye kidonda cha Katiba.

Makala hii inayochochea uwajibikaji na utawala bora, inajikita zaidi katika kuonyesha mazuri (mafanikio) na mabaya (dosari) zilizojitokeza kipindi cha utawala wa Dr. John Pombe Magufuli, Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na nini tumejifunza kutoka kwake na kipi siyo cha kujifunza.

Msingi wa wazo la makala hii, unatokana na nukuu kadhaa alizonukuliwa Dr. John Pombe Magufuli akisema kuwa "Watanzania mtanikumbuka kwa mazuri na siyo kwa mabaya". Kauli hiyo ya "mtanikumbuka kwa mazuri na siyo kwa mabaya", ndiyo mdhamini mkuu aliyeipa nguvu kalamu yangu kuandika makala hii. Hakika, ninaenda kuyachambua mazuri yaliyofanywa na Dr. John Pombe Magufuli na mabaya (dosari) zilizojitokeza kipindi chake, na nini viongozi wanatakiwa kujifunza.

ALAMA ALIYOACHA MAGUFULI KWENYE MIOYO YA WANYONGE.
(VIONGOZI IGENI HAYA).

Watanzania tunamkumbuka Dr.John Pombe Magufuli kwa mazuri mengi aliyotufanyia Watanzania. Mazuri ambayo yaligusa mioyo ya wanyonge na kubadili sura ya Tanzania.

Moja, alifufua, alitengeneza na aliboresha miundombinu mbalimbali. Moja ya jambo muhimu ambalo Rais John Pombe Magufuli alifanikiwa kuacha alama kwa Watanzania ni ufufuaji, utengenezaji na uboreshaji wa miundombinu. Miundombinu ambayo imebadili sura na mwonekano wa mama Tanzania. Hakika, unakumbukwa kwa hili. Miundombinu na miradi kama vile mabasi yaendayo kasi (mwendokasi), barabara za juu, ufufuaji wa shirika la ndege, treni ya umeme na kadhalika, ni miongoni mwa mambo ambayo yameacha alama isiyofutika kwenye mioyo ya Watanzania.

Pamoja na vyuma kukaza kipindi kile, bado Watanzania walifurahi kuona pesa yao inafanya kazi inayoonekana. Vilio vya wananchi baada ya kifo chake ni tafsiri ya hili. Mambo hayo nyeti, yanasadifu dhana ya uthubutu na uwajibikaji wa Viongozi. Kitendo cha kuthubutu kufanya hayo ni hatua kubwa kwa Kiongozi. Ukithubutu ukafeli, siyo jambo baya bali inakuwa ni hatua moja muhimu katika kufanikiwa. Hakika umetufunza dhana ya uthubutu na uwajibikaji kwa Viongozi.
Viongozi igeni uthubutu huo wa Magufuli.

Pili, nidhamu kwa wafanyakazi wa Serikali na Taasisi binafsi ilishamiri. Ukali wake, kutopenda mchezo na 'tumbuatumbua', viliwafanya wafanyakazi wa Serikali waliokuwa wavivu, kuanza kuhudhuria ofisini kwa wakati, kutimiza majukumu yao kwa wakati na kuheshimu waajiri wao (wananchi). Ziara zake za ghafla na kushtukiza, ziliwafanya wakae ofisini mda wote wa kazi.
Nidhamu ilishamiri kila eneo la kazi. Kwenye vituo vya afya, ofisi za serikali, bandari na kadhalika. Hakika, umetoa somo muhimu kuhusu namna gani Kiongozi anapaswa kushughulika na wafanyakazi wazembe, wajanjawajanja na wasio timiza wajibu wao. Viongozi igeni hizo mbinu za kushughulika na wafanyakazi wazembe, msiwachekee.

Tatu, falsafa yake ya "Hapa kazi tu" na hulka yake ya uchapakazi, imeogeza hamasa kwa viongozi na wananchi wa kawaida kufanya kazi kwa bidii. Falsafa hii ya "Hapa kazi tu" imetia hamasa kwa wananchi na viongozi wavivu, kupenda kufanya kazi kwa bidii.

Dr. John Pombe Magufuli, aliamini katika kazi tu. Starehe na sherehe ziso lazima, hazikuwa na nafasi kwake. Mbegu hiyo ya uchapakazi, imeota katika vichwa vya Viongozi na wananchi wa kawaida. Majina aliyobatizwa na Watanzania kama vile "jembe" na "tingatinga", yametokana na hulka yake ya uchapakazi. Hakika, umeitafsiri vizuri dhana ya uchapakazi kwa Viongozi. Viongozi igeni hilo, litawasaidia.

Sambamba na hilo, kitendo na maamuzi yake ya kutoka ofisini na kwenda kusikiliza kero za wananchi na kuzitolea majawabu, yanasadifu dhana ya ufuatiliaji na uwajibikaji kwa Viongozi. Viongozi katika maeneo mbalimbali, igeni huu mfano wa ufuatiliaji kwani unaleta ufanisi kazini.

KOVU ALILOACHA MAGUFULI KWENYE KIDONDA CHA KATIBA.
(DOSARI ZILIZOJITOKEZA).

Kovu aliloacha Dr. John Pombe Magufuli kwenye kidonda cha Katiba, ni mjumuisho wa dosari zilizojitokeza kwenye uongozi wa Dr. John Pombe Magufuli.

Zifuatazo ni dosari zilizojitokeza kipindi cha uongozi wa Dr. John Pombe Magufuli.

Matukio ya watu wasiojulikana na matukio ya watu kutekwa, yalitia dosari kubwa uongozi wa awamu ya tano. Matukio haya yaliyokuwa yanafanywa na wahuni wasiojulikana, yalitia doa kubwa uongozi wa awamu ya tano. Mfano, tukio la kushambuliwa kwa risasi aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Mheshimiwa Tundu Lissu, lililofanywa na wahuni wasiojulikana, lilitia dosari kubwa sana uongozi wa awamu ya tano. Matukio kama vile kutekwa kwa msanii Roma Mkatoriki, kupotea kwa watu na kutekwa kwa tajiri kijana Barani Afrika Bwana Mohammed Dewji, yaliendelea kutia doa jeusi uongozi wa awamu ya tano.

Msamiati "Uchochezi" ulitafsiriwa vibaya hivyo ukaminya wigo wa watu kukosoa, kuongea na kushauri. Wanasiasa waliogopa kutoa mawazo yao kwa sababu ya msamiati "uchochezi". Waandishi wa habari waliogopa kutapika ya rohoni wakihofia msamiati uchochezi. Msamiati uchochezi, uliminya uhuru wa watu kuongea na kukosoa mitandaoni.
Wanasiasa waliojaribu kutafsiri vizuri msamiati uchochezi, walichochewa moto. Mitandao ya jamii iliyojaribu kutoa tafsiri sahihi ya msamiati uchochezi, ilitandikwa vizingiti.

Hakika, matukio haya ya kinyama, kishamba na yaliyokiuka haki za binadamu, yalitia dosari kubwa sana uongozi wa awamu ya tano. Haya ni mambo ya kukemea.

Mwisho, Viongozi tuige uchapakazi, ufuatiliaji na uthubutu wa Dr.John Pombe Magufuli katika kufanya mambo muhimu ya Taifa.

WAZO LA JUMLA: Maendeleo ya Nchi yanahitaji Viongozi Wawajibikaji na Safari ya Utawala bora inahitaji dereva mwenye uvumilivu wa mitazamo tofauti.

Ahsanteni.
Naomba kuwasilisha.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom