Jonas Mkude ni Nahodha Sahihi Kwa Simba

Jonas Mkude ni Nahodha Sahihi Kwa Simba

Baba Kiki

JF-Expert Member
Joined
May 31, 2012
Posts
1,544
Reaction score
943
Mengi yamezungumzwa na wachambuzi wa soka kuhusiana na matukio na matokeo ya mchezo wa Simba na Yanga Jumamosi iliyopita. Mojawapo ya tukio lililovuta hisia ni utovu wa nidhamu aliouonyesha nahodha wa Simba Jonas Mkude dhidi ya mwamuzi Martin Saanya na kupelekea kuzawadiwa kadi nyekundu mapema kabisa mwa mchezo hivyo kuifanya Simba icheze ikiwa pungufu na ikiwa nyuma kwa goli moja.

Baadhi ya wachambuzi wakiongozwa na mchambuzi ninayemheshimu sana Edo Kumwembe , wamempachika jina Mkude kama nahodha wa mwendokasi wakimaanisha asiyestahili kutokana na haiba na hulka zake. Wamefikia mahali pa kuhoji hata aina ya manahodha ambao Simba wamekuwa wakituletea siku za hivi karibuni. Kiasi nakubaliana nao.

Wakati nakubaliana kwa sehemu kuwa Jonas Mkude alionyesha utovu wa nidhamu unaostahili adhabu yoyote kuanzia kadi ya njano hadi nyekundu kulingana na 'mood' ya mwamuzi lakini napingana na wote wanaosema kuwa Mkude hastahili kuwa nahodha wa Simba kwa sababu zifuatazo;

1. MKUDE SASA NI MCHEZAJI 'MWANDAMIZI' NDANI YA SIMBA.

Nahodha lazima awe ni mchezaji mwandamizi au mzoefu wa mchezo wa soka na wa klabu yake.
Jonas Mkude si mchezaji chipukizi tena, si mgeni wa derby za Simba na Yanga, si mgeni ktk timu ya Simba na sim mgeni na ligi ya VPL. Ukiangalia ndani ya kikosi cha Simba, unakuta Mkude ndiye mchezaji aliyekuwepo kikosini kwa zaidi ya misimu 4 tena ktk kikosi cha kwanza. Ni kweli Mwanjali, Bokungu na Angban ni wachezaji wazoefu zaidi wa soka la Afrika lakini nani anajua mwanzoni mwa msimu huu kuwa hawa wangeweza kuwa wachezaji tegemeo? Nani anajua wataendelea kuwepo ktk kikosi cha Simba baada ya msimu huu? Tumeona mchezaji kama Justice Majadvi aliyekuwa mhimili wa timu msimu uliopita akiwa leo hayupo. Ni ngumu kuwa na nahodha mgeni ambaye bado hajathibitisha ubora wake na asiyeijua timu

2. ANAJUA SIMBA ILIKOTOKA, ILIPO NA INAPOTAKA KWENDA

Jonas Mkude anaijua timu ya Simba pengine kuliko wachezaji wote wa kikosi cha kwanza, ukiacha Mwinyi Kazimoto. Anajua 'njaa' na 'kiu' waliyo nayo mashabiki na viongozi wa Simba kutokana na frustrations za misimu iliyopita. Anajua ubora wa Simba uliopotea. Ana uchungu yeye mwenyewe binafsi na mafanikio ya Simba. Huyu ndiye anaeweza kuwaambia wenzake nini wanatakiwa kufanya ili kukidhi kiu ya wadau wa Simba. Tunaona manahodha wa timu nyingine hata huko duniani ni wale wanaoijua klabu, na historia yake. Kwa hiyo walaumiwe viongozi wa Simba kwa kubadilisha vikosi mara kwa mara lakini aliyemchagua Mkude kuwa nahodha kwa mazingira ya sasaya Simba hakukosea.

3. KIWANGO SAFI, USHAWISHI MUJARABU KTK MCHEZO WENYEWE

Nahodha popote anapaswa kuwa mwenye ushawishi ndani katika mchezo wenyewe. Ndani ya uwanja. Yaani mwenye kiwango binafsi kinachoweza kusimama na kuonekana kiki-influence mchezo. Asiye na makosa mengi binafsi au kiwango cha kuchechemea. Mkude yuko vizuri ktk hili. Ni mpambanaji asiyechoka na anayejitolea karibu kila kitu kuifanikisha timu yake. Morali yake ya ushindi na upambanaji inajitosheleza kiasi hahitaji kusukumwa na mtu yeyote ndani ya uwanja. Ni matarajio nahodha wa namna hii anafaa zaidi kwa timu aina ya Simbayenye wachezaji wachanga pia ndani yake kama Mdhamiru, Kichuya, Ajibu, Tshabalala, nk. Naamini kiwango na morali yake ndivyo vilivyowashawishi waliomchagua wafanye hivyo licha ya mapungufu yake kibinadamu.

4. NIDHAMU YAKE SIO MBAYA KIHIVYO

Mkude hana nidhamu mbaya kihivyo ndani ya uwanja kama tunavyotaka kuaminishwa! Sikumbuki lini Mkude aliwahi kupigana au kutaka kupigana na mchezaji mwenzake ndani ya uwanja! Sikumbuki lini alipewa kadi nyekundu kwenye mechi ya Simba na Yanga, ukiacha hii ya juzi. Kinachoonekana zaidi kumhusu ni tabia yake ya upambanaji ambao huku akitumia nguvu na akili na wakati mwingine kuonekana anatumia nguvu zaidi. Si vizuri kumvuruga zaidi kwa makosa ya mechi moja kati ya 15 alizocheza za watani wa jadi.

Hata huko duniani tunajua manahodha wana sifa tofuati tofauti sana. Tunakumbuka watu kama Roy Keane wa Manchester United na Patrick Vieira wa Arsenal walivyokuwa wabishi na wakati mwingine wakionekana wakorofi zaidi kuliko wachezaji wengine. Huko Hispania wote tunamwona Sergio Ramos ndiye nahodha wa Real Madrid na tunajua alivyo mtukutu lakini bado kaaminiwa. Akina Pepe na Ureno yao ni yale yale. Na hapa Bongo, wote tunajua Nadir Haroub Cannavaro alivyoongoza kumpiga mwamuzi Israel Nkongo mwaka 2012 akiwa nahodha msaidizi lakini akawa nahodha mzuri tu wa Yanga baadae.

Mojawapo kati ya tabia za manahodha au viongozi popote duniani ni kuwa wanatofautiana, lakini pia na wao ni binadamu wanaokosea kama binadamu wengine. Nguvu (strengths) za Mkude ni nyingi zaidi kuliko udhaifu wake, kwa hiyo mechi ya juzi haiwezi kuwa kigezo pekee cha kuhoji unahodha wake, ila anaweza kukosolewa na kupewa nafasi zaidi.

5. ANA NAFASI YA KUJIFUNZA KUPITIA 'UBATIZO WA MOTO'

Watu wengi ikiwemo wachambuzi wetu hawataki kueleza kuwa mechi hii ya juzi ilikuwa imetanguliwa na 'pressure' kubwa kwa upande wa Simba kutokana na vipigo viwili mfululizo msimu uliopita. Dharau, kubezwa na mihemko ya utani wa jadi ilikuwa juu sana. Aidha ikumbukwe kumekuwa na dhana na hisia ya kwa wanazi wa Simba kuwa Yanga inafaidika na kubebwa na waamuzi na Simba wanaamini mechi ya mwisho mwamuzi aliharibu kwa kumtoa beki wa kati Abdi Banda ndani ya dkk chache tangu mchezo uanze na baada ya hapo Simba ikapoteana. Simba wengi wanaamini ktk siku za karibuni, ni rahisi mchezaji wao kupewa kadi yoyote kwa kosa lilelile ambalo mchezaji wa Yanga anaweza kulifanya bila kuonywa kwa kadi. Hii ni hisia, na naamini hisia hizi zinawafikia wachezaji ambao kwa bahati mbaya nao huwa zianwaathiri. Ktk mchezo wa juzi hisia hizi zilikuwepo na ikaonekana zinaendelea kukua kadri mchezo unavyoendelea hasa kwa Tshabalala aliyeonekana akilalamikia mwamuzi kila mara baada ya kuangushwa mara 3 na wachezaji wa Yanga ndani ya dkk 15 bila mwamuzi kutoa angalau onyo la mdomo.

Ndio maana unaweza kuona baada ya bao la Tambwe hata wachezaji wapole kama Kichuya walionekana kupaniki sana na nusura mchezo uharibike zaidi kama si busara ya benchi la ufundi la Simba. Hizi ni hisia zinazoanzia nje ya uwanja na watu wanahitaji matukio machache sana 'kuthibitisha'. Hapa ndio Mkude alipoonekana kuzidiwa zaidi na hisia hizi kiasi cha kufanya alichofanya.

Hata hivyo Mkude anaweza kutumia tukio hili kama ubatizo wa kuelekea kukomaa katika majukum yake ya unahodha. Makocha wake watumie matukio ya mechi ya juzi kumwonyesha makosa yake na kwa hakika anaweza kuibuka kuwa nahodha bora sana kwa siku zijazo. Potential yake ni kubwa sana kuliko mapungufu yake.
 
Umeongea vzr ndugu,kuna kitu watu hawaelewi yakua mwanadamu anaendelea kukua kwa kadiri anavyojifunza siku kwa siku kutoka na makosa na kuzidi kuwa bora zaidi ila makosa yake hayamfanyi kumuondolea ubora na sifa zake zote,ni kweli yakuwa nahodha anatakiwa ajifunze kuzuia jazba na kua kiongozi kwa wenzake,lakini haiondoi picha ya ubora na upiganaji wa mkude uwanjani,anahitaji kuelekezwa,kuonywa ili asirudie makosa na aendelee kuwa bora zaidi
 
Umeandika vyema sana Mkuu.. nadhani Edo na 'nduguze' watakua wamejifunza kitu.
Heshima kwako.
 
Back
Top Bottom