Kiranja Mkuu
JF-Expert Member
- Feb 18, 2010
- 4,534
- 5,342
Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Mbeya, Joseph Mwasote maarufu ‘China’, amesimulia mkasa mzito uliomfika akieleza jinsi alivyotwaliwa katika mazingira ya kutekwa na kufichwa kituo cha polisi, huku familia yake ikipigwa kalenda na kuambiwa hajulikani aliko wakati yupo ndani ya kituo hicho.
Akizungumza jijini Mbeya mnamo Agosti 12, 2026, Mwasote amefichua kuwa alitwaliwa tarehe 25 Oktoba mwaka jana muda mfupi baada ya kutoka karakana (gereji) kufuata gari lake, lakini alipofikishwa polisi, mke wake, watoto na marafiki zake walipokwenda kumtafuta waliambiwa na maofisa wa jeshi hilo kuwa hawana taarifa zake.
Kiongozi huyo amebainisha kuwa mbinu hiyo ililenga kumtesa kisaikolojia yeye na familia yake, kwani hata siku alipopelekwa mahakamani, ndugu zake walipata mshtuko mkubwa kumwona akitolewa mikononi mwa polisi wale wale waliostahili kumpa hifadhi ya kisheria.
"Siku nimechukuliwa tarehe 25 Oktoba, mke wangu, watoto na rafiki zangu walikwenda polisi lakini wakaambiwa 'hatujui aliko'. Wakiwa wanatoka, ndio wananiona wananileta mahakamani! Mimi nimetolewa kama nilivyokwenda kutupwa. Huku ni kutaka kukandamiza watu na siyo utendaji wa kisheria," ameeleza Mwasote.
Ameongeza kuwa pamoja na kuachiwa huru, simu zake zote za mkononi zilizochukuliwa na maofisa wa polisi siku hiyo hazijarudishwa mpaka leo, huku akifichua kuwa kuna askari aliyemfuata na kumtaka atoe fedha ili amrejeshee vifaa vyake hivyo.
Mwasote amehitimisha kwa kutoa rai kwa Jeshi la Polisi kujitathmini na kurudi kwenye misingi ya mafunzo yao ya kuheshimu Katiba, utawala wa sheria na kulinda haki za msingi za raia badala ya kutumia nguvu na vitisho.