Kidumba anasimulia akibainisha tofauti ya tija kati ya huko walikotoka na waliko sasa akisema: "Nilianza kulima kwenye skimu hiyo mwaka 1986, tulilima kienyeji, hatukuwa na utaalamu wowote, lakini baadaye skimu yetu iliboreshwa, tukapata utalaamu kupitia mabwana shamba, shamba darasa na mzungu mmoja aliyekuja hapa kijijini kwetu.
"Nimeongeza uzalishaji wa mpunga, sasa navuna gunia kati ya 25 hadi 30 za mpunga kwa ekari moja, huko nyuma nilivuna kati ya gunia saba hadi kumi. Mwaka jana nilivuna gunia 31 katika ekari yangu moja niliyolima, niliuza gunia 15 na kubakiza 16 kwa ajili ya chakula na mbegu.
"Hapa ni kulima mwaka mzima, tunaita hakuna kulala, mpunga nalima mara moja kwa mwaka, halafu kuna vitunguu nalima mara mbili kwa mwaka, mwaka jana nililima ekari mbili na kuvuna gunia 80 kila ekari, lakini nikienda vizuri navuna hadi gunia 100 kwa ekari.
"Kwa mfano Julai mwaka jana nilivuna gunia 100 kwa kila ekari, safari ya pili nilivuna gunia 107, na safari ya tatu nilivuna gunia 96, bei ya Januari huwa ni shilingi 50,000 kwa gunia la vitunguu, lakini baada ya Januari huongezeka hadi kufikia shilingi 70,000."