Jumatano ya majivu: Kupakwa majivu ni kukubali kwetu kuwa, tu wadhambi, tunahitaji kusafishwa 'Mwanadamu, u mavumbi na mavumbini utarudi'

The Watchman

JF-Expert Member
Joined
Nov 7, 2023
Posts
896
Reaction score
1,427

Jumatano ya Majivu, Mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima Cha Siku 40
Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini za kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kufanya matendo ya huruma. Ni kipindi kinachotualika kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo, kwa kufunga na kutenda matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni kipindi cha toba na kujipatanisha na Mungu, Kanisa, ndugu katika familia, marafiki zaidi sana ni kujipatanisha mtu na nafsi yake.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Siku ya Jumatano ya Majivu, siku ya kwanza ya kipidi cha Kwaresima.

Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini za kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kufanya matendo ya huruma. Ni kipindi kinachotualika kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo, kwa kufunga na kutenda matendo ya huruma, kama vile kuwasaidia wahitaji hasa maskini, kuwatembelea wagonjwa na hata wafungwa.

Ni kipindi cha toba, kipindi cha kujipatanisha na Mungu, kujipatanisha na Kanisa, ndugu katika familia, marafiki zaidi sana ni kujipatanisha mtu na nafsi yake.

Kwaresima ni safari ya maishaya kiroho ambayo kilele chake ni adhimisho la fumbo la ukombozi wetu - mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo tunaloliadhimisha katika juma kuu, kuanzia alhamisi kuu, ijumaa kuu na jumamosi kuu, kilele chake ni domenika ya Pasaka. Kusali, kujitoa sadaka kwa ukarimu kwa wahitaji na kufunga, ndizo nguzo kuu tatu za kipindi cha Kwaresima, kipindi cha toba.

Siku ya kwanza ya kipindi hiki cha Kwarema huitwa Jumatano ya Majivu kutokana na tendo la kupakwa majivu katika paji la uso na wakati huo mhudumu wa tendo hili takatifu la kiroho akisema; Mwanadamu kumbuka, u mavumbi wewe na mavumbini utarudi.

Jina hili la Jumatano ya majivu, lilianza kutumika rasmi mwaka 1099 na Papa Urbano II. Mwanzoni iliitwa “Mwanzo wa Mfungo”.

Majivu yanayotumika siku hii ya Jumatano ya majivu ni ya matawi ya mitende yaliyotumika Jumapili ya Matawi ya mwaka uliopita ambayo yanaashiria ushindi dhidi ya dhambi na mauti kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kwanini kupakwa majivu? Majivu ni alama au ishara tu ya nje inayoashiria toba ya ndani ya mioyo yetu kama ilivyo rangi ya kijivu ambayo ni rangi ya toba na matumaini.

Kupakwa majivu ni ishara ya toba yetu ya ndani ya nafsi zetu tunayoifanya ambayo inatutakasa na kutusafisha na uovu wote, kama Majivu yanavyotumika kusafisha vyombo.

Kumbe kupakwa majivu ni kukubali kwetu kuwa tu wachafu, tu wadhambi, tunahitaji kusafishwa, tunahitaji kutakaswa. Majivu ni mbolea na mbolea hutumika kukuza mimea na kuifanya izae matunda mema, mengi na bora. Toba ya kweli tunayoifanya ndani mwetu ikiashiriwa na alama ya majivu hutusaidia kukua na kuzaa matunda mema ya kiroho.

Majivu haya yanapakwa kwenye paji la uso, kama vile siku ya ubatizo tulipopakwa mafuta ya Krisma takatifu, tukaondolewa dhambi ya asili na adhabu zake zote, kwa ishara ya msalaba, alama ya ushindi tuliyokombolewa nayo.

Kumbe majivu yanatukumbusha kufanya toba na kuungama dhambi tulizotenda baada ya ubatizo. Kupakwa majivu katika paji la uso ni kukiri hadharani bila kujificha kuwa tu wadhambi na tunahitaji huruma ya Mungu Baba, tunahitaji msamaha, tunahitaji kutakaswa na kufanywa upya watoto wa Mungu na wa Kanisa.

Asili ya kujipaka majivu kama alama ya toba: Tendo hili la kiroho la kupakwa majivu katika paji la uso ni ishara ya toba ya kweli, ishara ambayo imekuwa ikitumika kwa maelfu ya miaka iliyopita hata kabla ya kuja Kristo.

Katika ulimwengu wa wayahudi majivu yalikuwa ni alama ya huzuni, masumbuko, uchungu au uduni (Ayubu 2:8, 30:19; Zab 102:10). Baadaye utamaduni huu wa kupakwa majivu ulitumiwa na wakristo wa kwanza kama alama ya toba.

Mwaka 600 hivi, Gregory Mkuu aliifanya siku ya Jumatano ya majivu kuwa siku ya kwanza ya Kwaresma na kufanya kipindi hiki cha toba kuwa ni cha siku arobaini. Miaka ya 800 hivi, baadhi ya makanisa yaliadhimisha ibada ya Jumatano ya majivu kwa ajili ya wadhambi waliokubuhu katika dhambi na waliojulikana.

Wadhambi hawa waliojulikana walipoamua kufanya toba na kubadili maisha yao walipakwa majivu. Hivi wakati huu si wote walipakwa majivu ila tu wale waliokuwa wadhambi waliojulikana wazi, kama vile makahaba, wauaji na waasi. Kuanzia karne ya 11, Kanisa kwa kutambua kuwa mbele za Mungu hakuna asiye na dhambi, liliamuru tendo hili liwe kwa waamini wote likiambatana na kufunga, kusali, kutoa sadaka na kufanya matendo ya huruma
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…