Kagera war

Kagera war

Comred Mbwana Allyamtu

JF-Expert Member
Joined
Jun 28, 2016
Posts
351
Reaction score
887
VITA YA KAGERA ILIMNYANYUA YOWERI KAGUTA MUSEVENI NA KUWAANGUSHA YUSUPH LULE, GODFREY BINAISA NA TITO OKELLO.

Na.Comred Mbwana Allyamtu
Thursday -18/10/2018

Nimeshawishika kuandika makala hii baada ya leo kukutana na rafiki yangu Akampa Bosco. Leo nimekutana na rafiki yangu huyu hapa kwenye hoteli ya Kilimanjaro Resort iliyopo hapa Marangu kilomita 12 kutoka hifadhi ya mlima Kilimanjaro, nikiwa hapa kwenye hoteli hii nikipata mapumziko ya honeymoon mara baada ya ndoa yangu mapema wiki hii . Nikiwa Nimejipumzisha katika eneo la mapumziko katika garden ndipo tunaonana na rafiki yangu na yeye akiwa honeymoon yake aliyochagua ifanyike mahali hapa.

Mimi na Bosco tulikutana kwa mara ya kwanza nchini Uganda mwaka 2015 mtaa wa kyandondo jijini Kampala, yeye alikuwa mwenyeji wangu kwa kipindi chote cha miezi mitano nilipokuwa nchini Uganda, nilipo rudi nchini humo mwaka 2016 yeye ndie alinikutanisha na Sandra aliyekuwa katibu wa shirika la Oxfam ambapo Winnie Byanyima ni mkurugenzi. Kupitia Sandra alinifanya nimfahamu Winnie Byanyima mke wa Kiza Besigye ambae huko zamani alikuwa ni mchumba wa Museveni, kupitia urudufu huo nimejikuta nikishawishika kuandika juu ya Museveni, Yusuph lule, Binaisa, Tito Okello na vita ya Kagera.

Yoweri Kaguta Museveni ambae ni rais wa Nane (8) wa Uganda alichukua kiapo cha kuwa raisi tarehe 29/1/1986 mjini Kampala, ya kuongoza Uganda taifa lilo kuwa limetokea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe na mapigano na jirani yake Tanzania vita ambavyo vilijulikana kama Vita ya Kagera.

Alichukua madaraka baada ya kushinda vita vya msituni chini ya kundi la National Resistance Movement (NRM). Kwa muda mrefu, kabla ya kuwa rais wa Uganda, Museveni aliongoza vita vya msituni dhidi ya serikali za Idd Amin aliyetawala toka mwaka 1971-79, na serikali ya Milton Obote aliyekuwa madarakani mwaka 1980-85.

Museveni aliibuka kuwa mpiganaji wa msutuni baada ya utawala wa Idd Amini kushika hatamu kwenye serikali ya Kampala, kufatia mtafaruku wa kisiasa hatimae kukazuka vikosi vya ukombozi vilivyotaka kuondosha utawala wa Amin madarakani, ni kipindi hicho hicho kulipozuka vita vya Kagera na kuipa nafasi vikosi vya uasi kujitanua na hatimae kuibuka kwa Museveni.

Katika vita hiyo serikali ya Idd Amini iliyokuwa na makazi yake katika ikulu ya Enttebe iliondolewa madarakani kwenye mapigano yaliyotekelezwa pakubwa na serikali ya Tanzania iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere, Idd Amini aliye lengwa kwenye vita hivyo aliingia madarakani tarehe 25/1/1971 kwa njia ya mapinduzi yaliyo muondoa madarakani Dr Milton Obote rais wa pili wa Uganda na waziri mkuu wa kwanza wa nchi hiyo ambae alipinduliwa tarehe 25/1/1971 wakati wa mapinduzi haya Obote alikuwa nchini Singapore kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za jumuiya ya madola.

Kufatia utawala wa Idd Amini nchini humo hatimae kulizuka mivutano ya kidiplomasia baina ya Tanzania na Uganda hali iliyo pelekea kuzuka vita vya Kagera mwaka 1978. Je chanzo cha vita ilikuwa ni nini?

VITA VYA KAGERA NA KISA CHA VITA YENYEWE.

Uhusiano wa Tanzania na Uganda ulidorora tangu Januari 25, 1971, Idd Amin Dada alipoipundua serikali halali ya Rais Milton Obote aliyekuwa nchini Singapore kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Madola, kufatia mapinduzi hayo Obote akakimbilia nchini Tanzania kutafuta hifadhi ya kisiasa.

Kufatia hatua hiyo Rais wa Tanzania, Julius Nyerere, akampa Obote na wenzake 2000 hifadhi ya kisiasa nchini Tanzania. Idd Amin hakufurahishwa na hilo kwani aliamini kwamba Nyerere alikuwa anamuandaa Obote aje kumpindua, kwa hiyo akapanga kumdhibiti kabla hajampindua hivyo Idd Amini akaanza chokochoko za kidiplomasia na Tanzania kisha akaivamia Tanzania.

Mikakati ya kivita ilianza kupangwa na Kanali, Abdu Kisuule, aliyekuwa mshirika wa karibu wa Idd Amin na kiongozi wa moja ya vikosi vya Uganda kwenye vita hiyo, kanali huyo alitumwa Ulaya kununua silaha, alikuwa na wenzake, Yekoko na meja Ndibowa. Walikwenda Bilbao Hispania. Walitumwa kununua vifaru, bomu aina ya Napalm ambalo ni maalumu kwa ajili ya kupambana na saba saba ya Tanzania(mtambo wa kurushia maroketi uliotengenezwa na Urusi uliokuwa ukiitwa BM Katyusha rocket launcher), na ndege 112 za kuangushia mabomu.

Kwa bahati mbaya, kila walipoenda, Tanzania iliwafuatilia na kuzima jaribio lao la kununua silaha.Endapo wangefanikiwa kununua bomu la Napalm, habari ingekuwa habari nyingine kwa sababu Napalm ni bomu la moto ambalo huunguza kila kitu, linapotua. Wakati bado wakiwa Hispania, Tanzania ikavamia Uganda na hatimaye Tanzania kuwahi mshindi wa vita ile.

Wakati wa vita yenyewe kwa upande wa Uganda ilianza mapema Januari 30, 1978, majeshi ya Idd Amin yalivamia Tanzania na kuvunja daraja la mto Kagera linalouunganisha mkoa wa Kagera na sehemu nyingine ya Tanzania. Amin akautangaza mkoa wa Kagera kama sehemu ya Uganda baada ya kufanikisha kusonga mbele na jeshi lake.

Kufatia hatua hiyo Rais wa Tanzania, Julius Nyerere akamsihi Amin kuondoa majeshi yake mkoani kagera lakini Amin akakataa na kukaidi amri ya Nyerere. Nyerere akaziomba jumuia za kimataifa kulaani uvamizi wa Idd Amin lakini dunia ikakaa kimya kufatia hatua hiyo Nyerere akatangaza vita vilivyoanza Oktoba 30, 1978.

Katika uwanja wa mapambano Nyerere alikusanya jeshi la wananchi lililoanza na askari pungufu ya 40,000 na kuongezeka mpaka 100,000 wakiwemo polisi, askari magereza, JKT na mgambo, Jeshi hilo likaungana na vikundi mbalimbali vya waganda vilivyokuwa vikimpinga Amin ambavyo vilikutana mjini Moshi kwenye mkutano wao waliouita Moshi liberation front.

Mkutano huo ndio ulioanzisha jeshi lililoitwa Uganda National Liberation Army (UNLA). Makundi haya ni pamoja na Kikosi Maalum kilichokuwa chini ya Tito Okello na David Oyite Ojok. Pia kulikuwa na kikundi cha FRONASA kilichokuwa chini ya Yoweri Museveni, pamoja na kikundi kingine cha Save Uganda Movement.

Majeshi ya Tanzania yalikuwa na mzinga kutoka Urusi ulioitwa BM Katyusha rocket launcher ambapo mizinga hiyo hapa nchini ilikuwa ikifahamika kama saba saba ambao ulivurumishwa moja kwa moja kwa majeshi Uganda. Majeshi ya Uganda yakaanza kurudi nyuma na kazidiwa nguvu na majeshi ya JWTZ ya Tanzania.

Kufatia kuzorota kwa majeshi ya Uganda hatimae Libya na Palestina wamsaidia Idd Amin, kufatia hatua hiyo Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi, alituma wanajeshi 2,500 kumsaidia Idd Amin. Wanajeshi hao walikuwa na silaha za kisasa kama vifaru vya T-54 na T-55, BTR APC, BM-21 Grad MRL, artillery, MiG-21, pamoja na kombora la Tu-22. Hata hivyo, walibya hao na wapalestina wakajikuta peke yao mstari wa mbele huku wanajeshi wa Uganda wakirudi nyuma. Askari wa Libya pamoja na Palestina wakatekwa.

Vita hiyo ilianza Oktoba 30, 1978 na kumalizika Aprili 11, 1979. Baada ya vita hii, Gaddafi akamuomba Nyerere awaachie askari wake na yeye atampa pesa nyingi au mafuta. Nyerere akakataa akisema binadamu halinganishwi na chochote, akawaachia bure askari wale ambao walisifu sana jinsi walivyotendewa wakati walipokuwa mateka.

Hata hivyo kufatia serikali ya Kampala chini ya Idd Amin kushindwa vita hatimae siku ya Jumatano ya Aprili 11, 1979, Rais wa Uganda Idi Amin Dada Oumee aliikimbia nchi yake na kwenda Libya na baadaye Saudi Arabia, baada ya kushindwa vikali katika vita dhidi ya Tanzania.

Baada ya vita Ile kuisha kwa ushindi mkubwa wa majeshi ya Tanzania hatimae uchaguzi wa mwaka 1980 ulimrudisha madarakani Milton Obote aliyeanzisha upya udikteta na kuua watu ovyo Obote alitekeleza unyama huo akidai kudhibiti maadui wake ambao walikuwa ni wafuasi wa serikali ya Idd Amini,. Wapinzani wake wakiongozwa na Museveni walirudi porini wakashika silaha chini ya wanamgambo wa National Resistance Amry (NRA) ambayo baadae ilibadilishwa jina na kuitwa NATIONAL RESISTANCE MOVERMENT (NRM) waliokuwa wakiongozwa na Yoweri Kaguta Museveni.

Katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kundi la Museveni likashinda na kutwaa serikali mapema mwaka 1986. Museveni mwenyewe ambaye alitokea kwenye baraza la vijana la chama cha Obote cha UPC, alijijenga vyema kipindi chote cha vita vya kagera

Kupitia jeshi lake la waasi ambao kwa sehemu kubwa walikuwa wanatokea Magharibi mwa Uganda, alifanikiwa kulishinda jeshi la serikali lililokuwa linadhibitiwa kwa sehemu kubwa na maafisa kutoka kaskazini hasa Walango na Wacholi.Yoweri Kaguta Museveni, alikuwa kati ya wanamigambo waliosaidiana na Watanzania katika vita vya kumpiga Amin Dada.

Huyu Yoweri Kaguta Museveni amezaliwa mwaka 1944 huko katika Kijiji cha Ntungamo, Wilaya ya Ntungamo, nchini Uganda. Yoweri ni mtoto wa mzee Amos Kaguta kwa Esteri Kokundeka ambae ndie mama yake mzazi, kufatia mama yake Museven Esteri Kokundeka kutengana na Amos Kaguta kufatia ndoa yao kuvunjika na Mzee Amos Kaguta, hivyo Museveni alilelewa na mama yake kwa shida sana kutokana na ufukara aliokuwa nao mama yake huyo.

Kwa bahati Boniface Byanyima ,Alikuwa mkuu wa shule ya Mbarara High School. Mzee Byanyima alikuwa ni mzee mwenye kupenda kufundisha na mwenye mapenzi makubwa na wanafunzi wake, hivyo mwaka 1959 Mwalimu Byanyima alimpokea mwanafunzi aliyekuja kujiunga na masomo hapo Mbarara High school ,alikuwa hana nguo za shule wala hana ada wala hana mahali pa kukaa, kijana mwembaa mwenye uso wenye uzuni sana na kila wakati anaonekana mpweke.

Mwalimu Byanyima akaamua kumchukua na kumweka nyumbani kwake na kumlimpia ada kijana huyo mdogo aitwaye Yoweri Museveni, hakujua kuwa kijana huyu ndie angekuja kuwa rais wa Uganda baadae, Mwalimu Byanyima hakuishia hapo akaanza pia kumsaidia mama Esteri Kokundeka mama mzazi wa Yoweri Museveni ambaye kipindi hicho mama huyo alikuwa amaechana na mzee Amos Kaguta baba mzazi wa Museveni, Mwalimu Byanyima alimfundisha Museven kidato cha kwanza na kidato cha pili huku akiwa kama mtoto wake aliendelea kukaa kwake na kumuhudumia huduma zote kama mwanae mpaka akafanikiwa kujiunga na chuo kikuu cha Dar es salaam kwa ufadhili wa pesa zake mzee Byanyima.

Baada ya Museveni kujiunga na elimu ya juu katika chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM) ndipo alipo jikuta akianzisha mahusiano ya kimapenzi na mtoto wa mzee Banyima aliyeitwa Winnie Byanyima jambo lilopelekea kuingia uadui na Mzee Bonifasi Byanyima.

Huyu Winnie Byanyima ndie mke wa sasa wa mpinzani mkubwa wa serikali ya Museveni Kiza Besigye huko mwanzo Winnie Byanyima na Museveni walikuwa wapenzi na ni kipindi hicho katika kipindi cha mapigano ya vita ya wenyewe kwa wenyewe Museven alimtorosha binti huyo msituni kwenye vita vya ukombozi, Museveni alifanya uamuzi huo wa kumtorosha Winnie Byanyima baada ya Baba yake kukataa kumuozesha mwanae Museveni.

Ni kipindi hicho Museveni alipokuwa mstuni alipo kutana na kijana mwingine aliyeitwa Dr Kiza Besigye ilikuwa ni mwaka 1982, Besigye alijiunga na vita vya msituni kufatia taaluma yake ya utabibu Museven akamfanya kuwa tabibu wake na akawa tabibu wake kwa muda wa miaka 10 hadi mwisho wa vita wakati wote huo Dr Kiza Besigye akiwa na mke wake Janette ambaye huyu Janette ndie mke wa sasa wa Museveni.

Hata hivyo Dr Besigye akiwa msituni alikuwa akiona ule ukaribu wa Museveni na Winnie, kufatia Winnie Byanyima kushindwa kuolewa na Museveni ndipo Museveni akamlubuni Jenette aliyekuwa mke wa Dr Besigye kisha akamuoa mama huku Dr Besigye akamchukua Winnie Byanyima na kufunga nae ndoa mwaka 1990.

Mitifuano baina ya Museveni na Dr Kiza Besigye ulianza kushika kasi mapema mwa miaka ya I990S kwani kipindi hichi ndio mwaka ambao waziri wa mambo ya ndani Dr Kiza Besigye alifukuzwa uwaziri na anakutana na Winnie wawili hawa wanaanzisha mahusiano na anaolewe na Dr Besigye na kufanikiwa kupata mtoto mmoja wa kiume. Huyu Winnie sasa ni executive director wa Oxfam.

Njee ya mambo mengine Inadaiwa kuwa Museveni aliamuru Ranch ya mzee Boniface itaifishwe hadi mzee Boniface anafariki dunia walikuwa hawaongei na Museven na walikuwa ni maadui wakubwa, mara zote Mzee Boniface Byanyima alikuwa akisema kuwa Mungu ndie atakaye mlipia fadhila zake kwa Museveni.

Baada ya kumtazama Museveni sasa tuludi mpaka Kampala mwaka 1979 baada ya majeshi ya Idd Amini kukimbia nchi Ikulu ilikabidhiwa kwa Yusuph lule.

Huyu Yusuph lule alizaliwa tarehe 10. 04. 1912 Kampala nchini Uganda.Tarehe 13-04-1979 aliteuliwa kuwa Rais wa mpito nchini Uganda mara baada ya kuangushwa kwa utawala wa Iddi Amini Dada na Jeshi la Tanzania chini ya Amir Jeshi Mkuu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Wananchi wa Uganda walioungana na jeshi la Tanzania walikutana Moshi na kuanza kuunda umoja na kufanya uteuzi wa Yusuph Lule. Siku ya pili,Mwalim Nyerere na wenzake wakafanya kikao cha baraza la mawaziri na kuamua kumtambua Yusuph Lule kama rais wa Uganda.

Yusuf Kironde Lule ndie Kiongozi wa juu wa Uganda aliyekaa madarakani kwa muda mchache kuliko viongozi wote wa nchi hiyo,Lule alitawala Uganda kwa Siku 68 tu kuanzia tarehe 12-04-1979 hadi 20-06-1979 na baadaye akafuatia Godfrey Binaisa.

Huyu Godfrey Lukongwa Binaisa alizaliwa Mei 30, 1920,alikuwa mwanasheria wa kujitegemea kuanzia mwaka 1969. Aliwahi kuwa Rais wa Uganda kwa muda na mwansheria mkuu baada ya nchi hiyo kupata uhuru miaka ya 60.

Baada ya Idi Amin kuchukua madaraka mwaka 1971, alikwenda uhamishoni Marekani,ambapo alifanya kazi kama mwanasheria huko Mount Vernon,mjini New York. Wakati alipokuwa Marekani,alikuwa mwanachama wa Uganda Freedom Union,moja miongoni mwa makundi yaliyokuwa yakimpinga Amin uhamishoni.

Kufuatia kupinduliwa kwa Idi Amin mwaka 1979, Binaisa akarejea Uganda.Baada ya Idi Amin,Yusuf Lule ,ndiye alikuwa Rais wa mpito kwa siku 68. Juni 20, 1979,Godfrey Binaisa aliteuliwa kuwa Rais wa Uganda na baraza tawala la wakati huo la National Consultative Council- NCC,chombo kilichokuwa chini ya Uganda National Liberation Front (UNLF),muungano wa waliokuwa uhamishoni kutoka Uganda waliosaidia kumwondoa Idi Amin.

Binaisa alipinduliwa Mei 12, 1980 na tume ya jeshi,chombo chenye nguvu cha UNLF kilichokuwa kinaongozwa na Paulo Muwanga na ambapo naibu wake alikuwa Yoweri Museveni (wakati huo akiwa kiongozi wa Uganda Patriotic Movement) Nchi hiyo baada ya hapo ikawa inaongozwa na tume ya Rais ya Uganda (iliyoundwa siku chache baada ya mapinduzi hayo) wakiwemo Paulo Muwanga,Yoweri Museveni,Oyite Ojik na Tito Okello. Tume hiyo ya Rais iliiongoza Uganda mpaka uchaguzi mkuu wa Rais wa Desemba 1980.

Binaisa alijiunga na akateuliwa kuwa naibu waziri wa Uganda Patriotic Movement.Ushindi ulipatikana kupitia chama cha Millton Obote cha Uganda Peoples Congress,hata hivyo, matokeo hayo yalipingwa,na kusababisha Museveni kuanzisha uasi msituni,uliosababisha yeye kupata urais mwaka 1986.

Kufatia machafuko ya kisiasa hatimae Tito Okello aliteuliwa kuongoza nchi katika kipindi cha kutafuta utulivu wa kitaifa,

Huyu Tito Okello Lutwa alizaliwa katika kijiji cha Nam Okora wilaya ya Kitgum wakati wa vita vya kwanza vya Dunia mwaka 1914,alijiunga na Kings African Rifles (KAR) May 16,1940 kama ilivyokuwa kwa Idd Amin naye alipigana vita vya Mau-Mau huko Kenya wakiwa upande wa waingereza mwaka 1957.

Tito Okello Lutwa alijiunga na Jeshi la Uganda na alipanda cheo kufikia Lieutenant mwaka 1962 na alifikia kuwa Colonel mwaka 1968.Wakati Amin anampindua Obote mwaka 1971 Gen.Tito Okello Lutwa alikimbilia Tanzania na alikaa sana Dar-es-salaam lakini pia aliwahi kukaa Nachingwea,Morogoro na Masange Tabora.

Mwaka 1978 wakati wa vita vya kumng'oa Idd Amin Tito Okello aliongoza kikosi maalum (Special-Force) kikosi ambacho alipigana bega kwa bega na waganda hao mpaka kung`oa utawala wa Idd Amin madarakani mwaka 1979.

Mwaka huo huo 1979 baada ya Amin kuondolewa alikuwa sehemu ya Tume ya kijeshi,na baadaye 1980 alikuwa mkuu wa Majeshi wakati huo huo akiwa kwenye Tume ya kijeshi.Mwaka 1984 Alipandishwa cheo na kuwa Lieutenant General.

Tito Okello Lutwa alipitia magumu sana kipindi hicho, kulikuwa na mambo mabaya sana jeshini Ukabila ulikuwa umetawala sana kulikuwa na vita kati ya makabila ya Acholi na Langi ilimuwia vigumu sana hata katika uteuzi wa maafisa wa jeshi mfano alimteua Smith Opon toka kabila la Langi kuziba pengo la David Oyite,uteuzi huo ulipingwa sana na wanajeshi toka kabila la Acholi ambao wao walitaka mtu kutoka kabila lao Brig.Olara Okello ambaye alikuwa na uzoefu katika nafasi hiyo.

Mwaka 1984 vita na waasi wa NRA ulikuwa ameongeza mashambulizi yao kwa serikali pia iliwezesha jeshi la taifa kugawanyika vipande viwili upande mwingine ukiunga mkono Acholi na mwingine Langi kabila la Obote na Oyite Ojok. Baada ya migogoro isiyokwisha ndani ya Jeshi la taifa UNLA na mapigano makali yaliyokuwa yakiongozwa na NRA chini ya Museveni Gen.Tito Okello aliamua kumpindua Rais Milton Obote July 25-27,1985 na Obote kukimbilia Kenya na baadae alienda Zambia ambako alifariki October 2005.

Baada ya mapinduzi hayo Tito Okello alitangaza kuwa Uganda itatawaliwa na Baraza la kijeshi na yeye akiwemo kwa miezi 12 kabla ya Uchaguzi kufanyika.Okello alijaribu kuliunganisha jeshi ambalo tayari lilikua vipande vipande alijaribu kuunda serikali ya Mseto iliyojumlisha vyama vya Federal Democratic movement,Uganda National Rescue Front,Uganda Freedom Movement na NRA iliyokuwa inaongozwa na Yoweri Kaguta Museveni,Hata hivyo aligundua janja ya nyani aliyokuwa anataka kucheza.Tito Okello na akakataa serikali hiyo na kuendelea na mapambano dhidi ya majeshi ya serikali UNLA

Yoweri Kaguta Mseven aliweka masharti magumu ili kukwamisha mazungumzo ya Amani yaliyokuwa yanaendelea huko Nairobi chini ya Rais Daniel Arap Moi wakati huo vikosi vyake vya NRA vilizidi kusonga mbele katika miji ya karibu na Kampala Barabara ya Masaka,Mubende,Mbarara na Katonga zote zilifungwa na kusababisha usalama katika maeneo yote kuwa hatarini.Askari walianza uporaji na utekaji wa magari na vituo vya Mafuta,Maskini.Okello hata hakumaliza kipindi alichoweka ili uchaguzi ufanyika na akapinduliwa January 26,1986.

Baada ya kupinduliwa alikimbilia uhamishoni hatimaye June 3,1996 alifariki akiwa na umri wa miaka 82,na mabaki ya mwili wake yalirudishwa Uganda na kuzikwa nyumbani kwao huko wilaya ya Kitgum,katika mazishi yake Rais Yoweri Kaguta Mseven alimtaja Okello kuwa alikuwa mtu mkuu aliyelitumikia taifa lake na atakumbukwa kwa juhudi zake za kuleta Amani Uganda, January 2010 wakati wa kumbukumbu ya vita vya Kagera alitunukiwa nishani ya Kagera National Medal Kwa heshima yake kwa kupigana vita kwenye miaka ya 1970-1979 dhidi ya Nduli Idd Amin.

Yoweri Kaguta Museveni hatimae alichukua madaraka baada ya kushinda vita vya msituni chini ya kundi la National Resistance Movement (NRM). Kwa muda mrefu, kabla ya kuwa rais wa Uganda, Museveni aliongoza vita vya msituni dhidi ya serikali za Idd Amin aliyetawala toka mwaka 1971-79, na serikali ya Milton Obote aliyekuwa madarakani mwaka 1980-85, baada ya vita ya kagera kumalizika Uganda ilikumbwa na mtikisiko wa utawala kwa viongozi wao kushindwa kusalia madarakani.

Jambo hili lilimfanya Museveni kujiimalisha na hatimae kuchukua nchi tarehe 26/1/1986 , hakika Museveni ukili kama isingekuwa Vita ya Kagera asinge kuwa raisi wa Uganda. Maana vita vya Kagera imekuwa dalaja la Museveni kuukwaa uraisi, na daima Vita ya kagera ni historia mahususi kwa Yoweri Kaguta Museveni.


Email- mbwanaallyamtu990@gmail.com
IMG_20190507_101146_068.jpeg
 
First seat, asante mkuu, marehemu baba yangu kapigana vita hii ya kagera alikuwa ananipa story nyingi sana kaacha na nishani tatu home ila saiv sion hata moja sijui nani alikwiba . RIP father Mt 2589..
 
Back
Top Bottom