Godlove Kabati
Member
- Oct 4, 2023
- 74
- 86
Chimbuko la hadithi:
Ashukuriwe Mungu kwa kutupatia zawadi ya sanaa hapa duniani. Sanaa ni burudani ya muhimu mno katika maisha yetu ya kila siku. Hebu fikiria dunia ingekuwaje bila wasanii wa muziki, wachoraji, wafumaji, wafinyanzi, waandishi wa fasihi na wengine? Ni wazi dunia ingekuwa sehemu inayochukiza sana eeh?
Basi Mungu alimbariki sana bwana Bram Stoker na kumpatia kipaji cha ajabu mno cha kuandika hadithi. Na Bram akatutungia hadithi nzuri sana katika riwaya yake ya DRACULA iliyopendwa tangu miaka ya 1897 hadi leo hii .Huyu DRACULA ni vampire, jini mnywa damu za viumbe hai. Ambaye anajulikana kama mfalme wa vampire wote kutokana na dhambi na mabalaa yake.
Ni kupitia riwaya ya bwana Bram Stoker, filamu hii ya THE LAST VOYAGE OF THE DEMETER ( Safari ya mwisho ya Demeter) ikatengenezwa. Filamu hii ni kipande kimojawapo cha hadithi hiyo kikijulikana kama ‘The captain’s log ’ (shajara la nahodha). Ambapo huyu alikuwa ni nahodha wa meli iitwayo Demeter, iliyokuwa ikisafirisha mizigo kutoka Romania kwenda Uingereza. Sasa tuanze kuizungumzia filamu yetu ya siku hii ya leo: kaa vizuri futa screen yako ili usome vizuri maandiko.
Filamu:
THE LAST VOYAGE OF THE DEMETER;
Ni mwaka 1897.
Makasha makubwa ya mbao 50, ambayo hayakujulikana yana nini ndani yake kutoka kijiji cha mbali sana kisichojulikana; yalihitajika kusafirishwa kutoka Romania hadi Uingereza. Makasha haya yaliletwa na watu ambao hawakutaka kujulikana pia.
Na kwa bahati siku hiyo meli iliokuwa iking’oa nanga ilikuwa ni meli ya DEMETER ,iliomilikiwa na nahodha wa kiingereza bwana Eliot. Ajabu ilikuwa ni kwamba wamiliki wa makasha haya hawakutaka kubaki pale hadi jioni, waliomba waondoke kwa haraka sana na hawawezi kusaidia kupakiza makasha hayo juu ya merikebu. Kabla ya kuondoka kwao, kiongozi wao kikongwe akawatakia safari njema mabaharia wa DEMETER, akawaombea wauone mwisho wa safari yao.
Mizigo ya kupakia ilikuwa mingi na nguvu kazi ilikuwa kidogo. Ikambidi nahodha atafute mabaharia wa ziada kusaidia jukumu lile na kazi za melini. Wanaume wengi na wenye nguvu waligombea kupata mchongo huu wa ubaharia. Miongoni mwao alikuwemo kijana wa kiafrika aliyeonekana msomi kutokana na unadhifu wa mavazi yake kulinganisha na wale baharia wengine. Nahodha akahitaji kumfahamu zaidi, akajitambulisha kama Clemens; muhitimu wa tiba katika chuo kikuu cha Cambridge na anao ufahamu juu ya masuala ya unajimu na ushonaji. Hapa CV yake Clemens haikutosha kumshawishi nahodha. Kilichohitajika ni nguvu na ukomavu wa utendaji kazi na sio vyeti vya elimu, kwa sababu hiyo akatoswa. Jambo hili likamfadhaisha sana Clemens, maana licha ya kutaka kuhudumu kama baharia chomboni mle, alikuwa akisubiria nafasi ya kurudi kwao Uingereza, hivyo akakosa vyote. Yakachaguliwa madume mengine matatu yenye nguvu kwelikweli. Wakaanza kupakia mizigo na makasha yale 50 merikebuni.
Makasha ya mbao yalikuwa mazito kwelikweli. Na yote yalikuwa na alama zinazofanana. Alama ya mfalme wa majoka, Dragon. Mmoja kati ya baharia akaiona alama hii na akaitambua, akashtuka na kuogopa sana; hakutaka kuendelea kufanya kazi melini hapo,akasema kuwa alama hiyo ya joka ni ishara mbaya sana. Akaondoka na akawatakia safari njema…akawaombea sana Mungu awalinde. Badala yake nafasi hii akapewa Clemens. We! Bahati iliyoje, Clemens akafurahia sana, akajumuika na jopo la mabaharia chomboni. Lakini alibaguliwa akadharauliwa, hakuna aliyeiona faida yake. Na safari ya DEMETER kutoka Romania kuelekea Uingereza ikaanza.
Nahodha Eliot, alikuwa ameshaihaidi nafsi yake kuwa hii ndio safari yake ya mwisho. Aliapa kuwa hatayasogelea tena maji ya bahari akiwa na cheo cha unahodha. Kwa maana hio akawa na imani kuwa safari yake ya mwisho itakuwa yenye Baraka na neema tele. Moyo wake ulikuwa na amani.
Ilikuwa ni ghafla tu, kiumbe muovu akaanza kutembea ndani ya chombo. Wanyama na mifugo ndani ya merikebu wakawa wa kwanza kugundua kuwa kuna shida mule ndani, hawakuwa na utulivu. Hali hii iliwashangaza sana mabaharia hasa baada ya kugundua kuwa ndani ya merikebu ile hata panya na wadudu wote walipotea ghafla. Katika staajabu yao wakamkuta binti mgonjwa katika shehena yao ya mizigo. Hawakujua ametokea wapi, wakaumia vichwa. Clemens akatumia taaluma yake kumsaidia binti huyu ambaye alikuwa amedhoofu mno.
Baharia wengine wote wakamchukulia binti huyu kama mkosi. Wote isipokuwa Clemens, yeye aliiamini sayansi na kupinga imani ya ushirikina na uchawi: alimuhudumia na akamfahamu binti yule kwa jina la Anna. Akajenga naye ukaribu na wakawa marafiki.
Wingu kubwa la sintofahamu likawakumba tena hasa baada ya mifugo yote kukutwa imeuawa tena kwa kifo cha kustaajabisha mno. Hapa wakaanza kumtafuta mchawi ni nani. Wote hawakuwa na majibu. Hata sayansi ya Clemens haikuweza kuwasaidia hapa. Baada ya siku moja tena mwenzao mmoja akapotea. Safari yao ikaingiwa na doa, binti Anna akajaribu kuwaeleza alichokifahamu, wakayaziba masikio yao wakamuona kama kichaa. Ni Clemens pekee aliyempatia sikio lake na akaelezwa ukweli ulio nyuma ya visa na mabalaa yaliyowakumba.
Anna akamwambia Clemens kuwa; katika merikebu yao ameletwa kiumbe wa kutisha anayefanania na binadamu; sio mwanadamu kiuhalisia na ni kosa pia kumuita mnyama. Yeye anaitwa- DRACULA, huyu amewasumbua sana kijijini kwao tangu enzi na enzi hata kabla ya kuzaliwa kwake, alikuwepo akiishi juu ya milima tangu kale. Anajificha mchana na anatokea usiku kunywa damu za wasio na hatia. Kijijini kwao amepunguza idadi kubwa ya watu. Kwa usalama wao ,wazee wa kijiji wakafanya naye shauri kumpeleka mahali penye watu wengi zaidi ili waondokane na balaa lake. Yeye (Anna) aliwekwa mule miongoni mwa makasha mengine ili awe ananyonywa damu katika safari hii yote. Na walifanya kosa kubwa kumuokoa maana hivi sasa DRACULA alihitaji mlo wake wa kila siku!
Wote kwa pamoja Clemens na Anna wakaanza kufanya upekuzi ndani ya makasha yale 50 ya mbao yaliyotoka kijijini kwa Anna. Moja baada ya jingine, wakitafuta alikokuwa analala huyu shetani nyakati za mchana na kwenda out nyakati za usiku. Kwa mahangaiko makubwa wakafanikiwa kulipata kasha moja kubwa kama jeneza ndani yake kulikuwa na mafunza na wadudu kuonesha kuwa kile ndicho kitanda chake huyu jini mchafu, DRACULA. Lakini walikuwa wameshachelewa tayari, huyu jini alianza mapema kumtafuna mmoja baada ya mwingine akihakikisha kuwa kila mtu aliyemo ndani ya merikebu ile anaionja mauti.
Kwa mara ya kwanza Clemens akaiweka chini taaluma yake ya udaktari na sayansi, akaziamini imani na hadithi za kishirikina; akavaa silaha. Yeye na wenzie, wakashirikiana kumuwinda adui aliyewawinda katika merikebu yao wenyewe. Zile baraka walizoombewa na watu kule Romania zikawageukia na kuwa kama laana. Lengo lao likawa ni moja tu, kuhakikisha kuwa Dracula hafiki Uingereza. Waliogopa sana laana hii kufika katika ardhi ya nyumbani kwao. Haikuwa vita ya kutafuta uhuru kama kwenye vitabu vya historia. Hii ilikuwa vita ya kuokoa nafsi iliyopiganwa usiku, tena kwenye uwanja mgumu; bahari iliogadhibika kwa upepo mkali na mvua kubwa yenye radi. Na adui wao alikuwa na uwezo wa ajabu, hata silaha zao hazikutosha kumuumiza. Hakika ilikuwa ni safari ya mwisho ya DEMETER.
DEMETER Ilifika Uingereza ikiwa hovyohovyo, ilikuwa wazi kabisa kuwa vita kali ilipigwa pale. Askari wa doria bandarini walipoiona waliikimbilia. Walichokipata kiliwaogopesha zaidi ya kuwashtua; ni ujumbe ukioandikwa kwenye shajara la nahodha
:Hii ni tahadhari kwenu, kama ikitokea na nyinyi amewafikia, basi Mwenyezi Mungu awasaidie .Sisi tumejaribu kupambana naye na kama tukishindwa kumzuia…Basi Mungu aziokoe nafsi zenu.Ni bonge moja la filamu, ambayo huwezi kuacha hata sekunde ikupite. Inaitwa “THE LAST VOYAGE OF THE DEMETER”imetoka mwaka 2023. Genre ya thriller (kusisimua) na horror(kutisha).
GOdlove Kabati,
Morogoro, Tanzania.