"Nimesimama dukani nichukue mzigo, Jiji wamebeba Pikipiki yangu, wanasema nilipe Sh 50,000
Mimi ni dereva wa Taksi Mtandao, leo (Oktoba 7, 2026) nilienda Kariakoo, kuchukua mzigo wa mteja karibu na Msimbazi pembeni kabisa mwa Barabara, sio kwenye barabara kuu wala katikati ya njia, nikaingia dukani nifunge mzigo kisha niondoke.
Cha kusikitisha na kushangaza, nilipotoka dukani nikakuta Maafisa wa Jiji wameibeba na kuipakia kwenye gari lao, nilipouliza kulikoni wakawa wananijibu kwa ukali kuwa "Tukutane ofisini".
Wakati huo kuna pikipiki na bajaji nyingi zimepaki n ahata magari tena mengine yameegeshwa vibaya lakini inakuwaje wanachagua pikipiki za baadhi ya watu na kuzichukua huku zingine wakiziacha?
Sisi Taksi Mtandao ukifika sehemu ukasimama hata kuzungumza na mtu kwenye simu kama ni Mteja wako umuulize alipo hapohapo wanakukamata.
Hali hii inatukatisha tamaa sana sisi vijana tunaojitafutia riziki kwa halali, ajira hakuna, tunapambana kujiajiri kwenye usafiri wa mtandao, lakini badala ya kututengenezea mazingira mazuri na rafiki ya kufanya kazi, Serikali hiyohiyo inatunyanyasa.
Mamlaka zinazohusika ziangalie kero hii ya Kariakoo na kutupatia mazingira stahiki ya kufanyia kazi."