Akizungumza Bungeni Oktoba 30, 2026, Mbunge wa Katavi, Thomas Maganga Kampala, ameitaka Serikali kuongeza nguvu na kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya kilimo, akisema kuwa sekta hiyo tayari inachangia asilimia 19 ya Pato la Taifa (GDP) licha ya kutokupewa msukumo wa kutosha.
Akichangia hoja hiyo, ameeleza kuwa kilimo kinaajiri takriban asilimia 65 hadi 70 ya Watanzania, na kwamba iwapo serikali itaweka kipaumbele cha dhati na kuboresha mazingira, sekta hiyo ina uwezo mkubwa wa kukuza uchumi na kuongeza mchango wake hadi kufikia asilimia 40.
Aidha, Mbunge Maganga amelalamikia ukosefu wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao katika maeneo yanayozalisha kwa wingi kama vile Katavi, Tabora, na Chunya, akitolea mfano wa zao la tumbaku ambalo wakulima wake wanakabiliwa na changamoto za kushuka na kupanda kwa bei kutokana na ukosefu wa uwekezaji wa karibu.
Ameitaka Serikali kuanzisha mkakati madhubuti wa kujenga viwanda vya kati na kuwekeza rasmi kwenye miradi ya umwagiliaji ili kuwaondoa wananchi kwenye utegemezi wa kilimo cha msimu na kufuata nyayo za nchi zilizopiga hatua kiuchumi kupitia kilimo.