NANI ATASHINDA TUZO YA MO IBRAHIM?
Imeandikwa na BBC London.21.10.07
Hii ni mara ya kwanza kwa tuzo ya Mo Ibrahim kutolewa.
Sikiliza Leo Afrika
Siku ya Jumatatu, mfuko wa Mo Ibrahim [Mo Ibrahim Foundation], utatangaza jina la mshindi wa tuzo ijulikanayo kama Mo Ibrahim Prize for Achievement in African Leadership, inayotolewa kwa mara ya kwanza kwa kiongozi bora mstaafu barani Afrika.
Aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, mwenyekiti wa kamati ya tuzo hiyo, atatoa tangazo mbele ya vyombo vya habari vya kimataifa, wawakilishi maswala ya kijamii na wanabalozi kwenye ukumbi wa City jijini London.
Kamati hiyo imefanya tathmini na kutafakari kwa sifa walizonazo viongozi wastaafu wa mataifa 13 ya mataifa ya Afrika, wengi wao wakiwa wameondoka madarakani katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Je unadhani tuzo hiyo ina manufaa yoyote kwa nchi za Afrika?
Tuzo hiyo ni wazo la Mo Ibrahim, mfanyabiashara milionea wa kampuni za simu za mkononi, ambaye anadhamini mradi huo kwa matumaini kwamba utatoa changamoto kwa viongozi wa serikali za Afrika; ili siku moja wananchi wao waishi bila kutegemea misaada.
Washindani:
Miongoni mwao ni wale ambao jopo lolote makini halitawazingatia, kwa kufanya hivyo watalichafulia jina bara la Afrika.
Sita kati yao walikuwa wameingia madarakani kwa njia ya mapinduzi; na baadhi yao walingolewa katika utawala kwa nguvu.Abdiqasim Salad Hassam wa Somalia, hakuwa na taifa rasmi la kuongoza.
Lakini wapo viongozi makini miongoni mwao, Benjamin Mkapa wa Tanzania anayesifika kwa kujenga uchumi wa taifa lake.
Lakini mfano unaong'ara zaidi ni Joachim Chissano aliyeitoa Msumbiji katika vita vya wenyewe vya wenyewe na kuimarisha amani na uchumi.
Mwingine ni Domitien Ndayizeye wa Burundi aliyefanya kazi ya kuisuluhisha nchi yake kati ya wahutu na watutsi
Malengo;
Tuzo ya Mo Ibrahim ilianzishwa kutambua ufanisi wa uongozi wa mataifa ya Afrika.
Viongozi wote wastaafu kutoka nchi za kusini mwa Afrika walioondoka madarakani miaka mitatu awali wanakuwa na sifa ya kuzingatiwa na kamati hiyo.
Tuzo hiyo itakuwa na thamani ya dola 500,000 kila mwaka kwa kipindi cha miaka 10, na dola 200,000 kila mwaka baada ya hapo.
Je unadhani tuzo hiyo ina manufaa yoyote kwa nchi za Afrika?
Tuandikie maoni yako ambayo tutayasoma katika mojawapo ya matangazo yetu.
www.bbc.co.uk/swahili