BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,591
- 8,826
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Ashatu Kijaji amesema kampuni za nje zilizoshiriki katika maonyesho ya 47 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) mwaka huu zimeongezeka ikilinganishwa na mwaka jana.
Mwaka huu jumla ya kampuni 266 kutoka nje zimeshiriki maonyesho hayo ukilinganisha na kampuni 225 zilizokuwapo mwaka jana.
Ameyasema hayo leo baada ya kutembelea mabanda ya washiriki katika maonyesho hayo yanayotarajiwa kufikia tamati Julai 13, mwaka huu.
“Mwaka jana tulikuwa na waonyeshaji 225 kutoka nje ikilinganishwa na mwaka huu 266 na juzi tu jumla ya waonyeshaji 150 kutoka China waliwasili nchini wakiwa na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL),” amesema.
Amesema Wachina hao watakuwapo nchini hadi pale maonyesho yatakapokamilika.
"Wamekuja kubadilishana teknolojia na uvumbuzi na waonyeshaji wetu katika kilimo, biashara na viwanda," amesema.
Kamouni hizo za kigeni zinazoshiriki katika maonyesho ya biashara ya mwaka huu zinatoka katika nchi 16 zinashiriki katika maonyesho zikiwemo China, India, na Iran ambazo pia zitashiriki mikutano ya biashara kwa biashara ya ana kwa ana na wafanyabiashara kutoka Tanzania.
“Tanzania iko salama tunawakaribisha wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza,” amesema Kijaji.
Katika hatua nyingine, alibainisha kuwa wamepata ugeni kutoka Rwanda ambao wamekuja kutafuta fursa za masoko nchini.
Wakati waziri akiyasema hayo mwitikio wa watu katika utembeleaji wa maonyesho hayo bado si mkubwa ukilinganisha na mwaka uliotangulia licha ya kuwa ni siku ya sita tangu kuanza kwa maonyesho hayo.
Wengi wanaofika katika viwanja hivi wamekuwa wakikimbilia zaidi katika banda la Wizara ya Maliasili na utalii kwa ajili ya kuona wanyama wa aina mbalimbali walioletwa.
Pia banda la Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo nalo limekuwa miongoni mwa yale yanayopendwa kutokana na kualiaka watu mbalimbali ikiwemo vikundi vya ngoma, mabondia na wachekeshaji.
MWANANCHI