Kila Jumamosi alasiri, Levin Chama mwenye umri wa miaka 11 huja kwenye Kituo cha Mtandao cha Konnect Hub kilicho kwenye mtaa wa 44 ya Githurai wa mji mkuu wa Kenya, Nairobi, ili kusikiliza masomo ya lugha, utamaduni, hisabadi yanayotolea na walimu wa nchi mbalimbali kupitia mtandao wa Internet.
“Napenda masomo haya, ambayo ni tofauti na yale ya shuleni. Nimejifunza lugha mpya na kujua utamaduni wa nchi nyingine” Alipoulizwa anapenda kujua zaidi mambo ya nchi gani, Levin alijibu ni China. “Kwa sababu China ni nchi yenye teknolojia nyingi za juu, naweza kujifunza mambo mengi ya kisasa."
Kituo cha Konnect Hub ni jukwaa la elimu ya mtandao lililotolewa na tawi la Kampuni ya Telecom ya China nchini Kenya kwa kushirikiana na Wachina binafsi nchini humo kwa watu wa kipato cha chini na cha kati. Katika miaka ya hivi karibuni, sekta ya mtandao wa Internet imekua haraka sana barani Afrika, lakini kiwango cha matumizi bado kiko nyuma sana ikilinganishwa na kanda nyingine duniani, kutokana na gharama kubwa. Takwimu zinaonesha kuwa, ada ya mtandao mjini Nairobi ni shilingi 3,000 kwa mwezi. Wakati huo huo asilimia 80 ya familia mjini humo zina kipato kati ya 20,000 na 50,000 tu.
Ili kusaidia watu wenye kipato cha chini na cha kati kuweza kutumia mtandao, tawi la kampuni ya Telecom ya China nchini Kenya kwa kushirikiana na Wachina binafsi walianzisha kampuni ya teknolojia ya mtandao ya Ahadi Wireless Limited, ambayo inatoa huduma ya mtandao ya bei nafuu ya shilingi 20 kwa saa, shilingi 70 kwa siku, shilingi 350 kwa wiki hadi shilingi 1,000 kwa mwezi, na kasi ya mtandao ni megabytes 8 kwa sekunde. Licha ya hayo, kampuni hoyo pia imeanzisha Vituo vya Konnect Hub, ambavyo vinatoa huduma bure ya masomo mtandaoni kwa watoto kati ya miaka 5 hadi 15. Hadi sasa, kampuni hiyo ina watumiaji 65,000 wa kusajiliwa.
Kufanikiwa kwa kampuni hiyo ni mfano mmoja tu wa ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika katika maendeleo ya shughuli za mtandao. Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC na pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, China imechangia sana ujenzi wa “Afrika ya Kidijitali”, na kuzisaidia nchi za bara hilo kutumia mtandao kama njia ya kukabiliana na changamoto, zikiwemo kuimarisha juhudi za kupambana na janga la COVID-19, kutoa mafunzo mtandaoni, na mawasiliano ya jamii mbalimbali.