SoC03 Kanuni za utawala bora

SoC03 Kanuni za utawala bora

Stories of Change - 2023 Competition

tpaul

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2008
Posts
24,225
Reaction score
22,632
Utangulizi
Kila kitu kina kanuni ambazo zisipofuatwa au kuzingatiwa kitu hicho hakiwezi kufanikiwa au kuwepo. Kwa mfano, mwili wa binadamu una kanuni ambazo zikikiukwa inazweza kupelekea mwili kudhoofika au kusababisha kifo kabisa.

Utawala bora nao una kanuni mbalimbali. Kanuni za utawala bora zinahakikisha uwepo wa mambo kadhaa, ambayo ni pamoja na kupiga vita ufisadi, kuzingatia maoni ya wachache, na kuhakikisha maoni ya makundi maalumu katika jamii yanazingatiwa wakati wa kufanya na kutekeleza maamuzi.

Aidha, utawala bora lazima uzingatie mahitaji ya jamii ya sasa na ya baadaye. Kwa mfano, serikali inapoanzisha mradi wa maendeleo sharti izingatie kuwa mahitaji yataenda yakiongezeka kadri ya muda, hivyo ni muhimu kufanya makadirio mapana zaidi kuliko kuzingatia tu mahitaji ya wakati uliopo.

Zifutazo ni kamuni za utawala bora ambazo zikikiukwa kunakuwa hakuna utawala bora bali utawala msonge:

Ushirikishwaji
Ushirikiswaji wa wananchi wote, wake kwa waume, ndio msingi mkubwa wa utawala bora. Kushirikisha watu katika kufanya maamuzi ni kuhakikisha kuwa hawaburuzwi na kwamba uamuzi wowote utakaofikiwa unamnufaisha kila mmoja katika jamii. Ushirikishwaji unaweza kuwa ama wa moja kwa moja au kupitia uwakilishi. Ushirikishwaji ni nguzo muhimu kwa sababu demokrasia ya uwakilishi lazima ihakikishe maamuzi yanazingatia maslahi ya makundi maalumu.

Mara nyingi tumeshuhudia viongozi wakifanya maamuzi pasipo kuwashirikisha wananchi. Utamaduni huu yafaa ufe kwani kufanya maamuzi ya kibabe bila kuwashirikisha wananchi, ni tabia isiyokubalika.

Utawala wa sheria
Kwa ujumla, utawala wa sheria unahitaji mifumo ya sheria inayofanya kazi kikamilifu. Pia unahitaji ulinzi wa haki, hasa za wachache. Matumizi sahihi ya sheria yanahitaji mahakama zilizo huru na vyombo vya kusimamia sheria ambavyo havinuki rushwa.

Wakati mwingine maamuzi yanatolewa na mahakama yana walakini mkubwa. Na pia wasismamizi wa sheria sio wakamilifu kwa kiasi cha kutosha. Utawala wa sheria lazima uhakikishe kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria – kwmba watu wote ni sawa mbele ya sheria.

Uwazi
Uwepo wa uwazi unaamisha kwamba maamuzi na utekelezaji vinafuata sheria na taratibu zilizopo. Pia inaamisha kuwa taarifa zinatolewa kwa uwazi na zinapatikana kwa urahisi kwa wale watakaoathirika na maamuzi na utekelezaji huo Aidha ina maana taarifa za kutosha zinatolewa na kwamba zinzatolewa kwa lugha nyepesi inayoeleweka hata kwa watu wa kawaida.

Taarifa ikitolewa kwa lugha ngumu isiyoeleweka ina italeta wasiwasi kuwa kuenda kuna jambo linafichwa. Kwa mfano, unapotoa taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi wa kawaida unapaswa kuirahisisha ili zielewke vizuri. Ukizitoa kwa lugha ngumu kutakuwa hakuna uwazi, hivyo misingi ya utawala bora itakuwa imekiukwa.

Maamuzi ya pamoja
Mbali na wananchi kushirikishwa kwenye maamuzi ni muhimu kufikia maamuzi ya pamoja (consensus). Utawala bora unahitaji uwepo wa majadiliano ya pamoja kabla ya kufikia maafikiano yenye tija kwaj jamii nzima. Pia kunahitajika kuwepo mienendo chanya kwa ajili ya maendeleo endelevu ya watu na jinsi ya kufikia malengo hayo ya maendeleo.

Kwa ujumla, utawala wa kidemokrasia na maamuzi ya pamoja vinahitaji uwepo wa uongozi bora. Bila uongozi bora ni vigumu kuwa na utawala bora.

Mwitikio
Utawala bora unahitaji taasisi zijaribu kutumikia wadau wote ndani ya muda muafaka. Serikali ipo kutumikia wananchi, na kwa sababu hiyo serikali inapaswa kuhakikisha wanakuwa na mwitikio chanya kwa mahitaji na matakwa ya wananchi.

Kwa mfano, inapotokea baa la njaa au mafuriko, lazima serikali ifanye jitihada za haraka kuwasaidia wananchi kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kufuatia majanga hayo.

Mwitikio, kama kanuni ya utawala bora, lazima uhakikishe unasaidia kushughulikia mahitaji na madai ya watu kwa njia ifaayo, yaani, kutetea maslahi yao haraka, uwazi na kwa njia muafaka.

Usawa
Ustawi wa wananchi unategemea hakikisho kuwa raia wote wana maslahi ndani yake na hawajisikii kutengwa na mkondo mkuu wa jamii. Hii inahitaji kujumuisha makundi yote, lakini hasa makundi maalumu pamoja na yale yaliyo katika mazingira hatarishi.

Usawa lazima uzingatie kuwa wananchi wote watendedewe sawa bila kujali jinsia, rangi, imani, dini au aina yoyote ya ubaguzi. Na pia wananchi wote wapewe fursa sawa ya kujiendeleza na kupata rasilimali za jamii na fursa nyinginezo,

Serikali lazima ichukue hatua za makusudi kuendeleza makundi maalumu katika jamii. Makundi hayo ni pamoja vijana, walemavu na wanawake, pamoja na hilo, wananchi wapewe fursa sawa ya kumiliki na kudhibiti rasilimali za jamii ikiwa ni pamoja na uongozi, maliasili na mengineyo.

Ufanisi
Utawala bora lazima uhakikishe kwamba taasisi za umma zinazalisha matokeo yanayokidhi mahitaji ya jamii huku wakitumia vyema rasilimali walizo nazo. Dhana ya ufanisi pia inahusisha matumizi endelevu ya rasilimaili na utunzaji wa mazingira,

Ufanisi lazima uwawezeshe wananchi kuwa na fursa sawa ya kumiliki na kudhibiti rasilimali za jamii na pia kufanya kazi kwa bidii na kufikia vigezo na malengo yaliyowekwa.

Dhima ya ufanisi ni kuhakikisha huduma za umma zinatolewa na watu wenye sifa na wanaojiamini. Na pale inapowezekana sekta binafsi ishirikiane na serikali (PPP) lakini kwa kufuta sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa.

Uwajibikaji
Uwajibikaji ni hali ya kiongozi na mtendaji kuwa tayari kujibu, kubeba dhamana na kutoa maelezo kwa wananchi juu yamaamuzi au matendo aliyoyafanya katika kutekeleza dhamanaaliyopewa. Kwa mujibu wa Ibara ya 8 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 Serikali (viongozi nawatendaji) itawajibika kwa wananchi.

Serikali inaendesha shughuli zake kwa niaba ya wananchi. Hivyo, serikali inapaswa kuwajibika kwa matendo yake (na kutotenda) kwa

watu. Pia ni kweli kwamba uhalali wa serikali yoyote unatoka kwa watu kwa kuwa ni watu wanaoipa mamlaka kupitia mchakato wa uchaguzi.

Uchaguzi huru na wa haki
Mfumo wa uchaguzi huru na haki ni mojawapo ya sifa kuu za demokrasia duniani zinazodhihirisha mamlaka ya wananchi katika kuamua namna wanavyotaka kujitawala na kuongozwa.

Taasisi imara na mifumo thabiti ya chaguzi huru na haki, vinaondoa uwezekano wa nchi kutumbukia katika machafuko kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa mchakato wa uchaguzi.

Uchaguzi huru na wa haki hudhibiti mianya ya kuchaguliwa na kuwekwa madarakani mamlaka za kidikteta zenye kujali na kusimamia maslahi ya wachache badala ya maslahi ya taifa na matakwa mapana ya wananchi.

Hitimisho
Utawala bora ni muhimu kwani unasaidia kuchochea matumizi mazuri ya rasilimali za nchi, kuleta maendeleo endelevu na kupunguza umasikini, ujinga na maradhi. Pia, husaidia kupunguza ulaji rushwa, kuboresha huduma za jamii, kuchochea amani na utulivu na kuheshimiwa kwa haki za binadamu. Aidha, utawala bora husaidia katika utatuzi wa migogoro kwa mujibu wa sheria na kuchagiza ustawi wa wananchi.

Nawasilisha.
 
Upvote 3
Ushirikiswaji wa wananchi wote, wake kwa waume, ndio msingi mkubwa wa utawala bora. Kushirikisha watu katika kufanya maamuzi ni kuhakikisha kuwa hawaburuzwi na kwamba uamuzi wowote utakaofikiwa unamnufaisha kila mmoja katika jamii. Ushirikishwaji unaweza kuwa ama wa moja kwa moja au kupitia uwakilishi. Ushirikishwaji ni nguzo muhimu kwa sababu demokrasia ya uwakilishi lazima ihakikishe maamuzi yanazingatia maslahi ya makundi maalumu.
Hapa kwenye ushirikishwaji ndipo penye tatizo kubwa. Rejea uingiwaji wa mkataba na DP World ambapo wananchi hawakushirikishwa hata kidogo kutoa maoni yao. Hili ni tatizo kubwa sana hapa nchini Tanzania.
 
Back
Top Bottom