Mbunge wa Urambo Magharibi Juma
Kapuya (CCM), anayetuhumiwa
kutishia kumuua binti anayedaiwa
kumbaka, amerejea nchini jana
akitokea nchini Sweden, huku Jeshi la
Polisi likikwama kumtia mbaroni kama
lilivyokuwa likitamba.
Wakati mbunge huyo akiwasili nchini
na kupokewa na kusindikizwa na
wapambe wake, Bunge limeridhia
kukamatwa kwake kwani tuhuma
zinazomkabili ni za jinai na
zinamhusu yeye binafsi.
Mbunge huyo ambaye amepata kuwa
waziri, amerejea nchini jana majira ya
saa tano asubuhi kwa ndege ya
Shirika la Qatar na kutua katika
uwanja huo wa ndege na kuondoka
kupitia mlango wa watu maarufu
(VIP).
Habari zinasema mbunge huyo
alipoondoka katika Uwanja wa Ndege
wa Mwalimu Julius Nyerere alikwenda
moja kwa moja kwenye moja ya hoteli
za jijini Dar es Salaam na kuacha
mizigo yake, kisha kuondoka na gari
namba T 104 AEZ Toyota, huku
wapambe wake wakiwa katika gari
namba T 170 BGY aina ya Benz.
Wakati Kapuya akitua katika uwanja
huo wa ndege, polisi ambao kwa
takriban wiki moja sasa wamekuwa
wakitamba kutaka kumtia mbaroni
mara baada ya kutua, baadhi yao
walionekana wakisalimiana naye kama
vile hawakuwa wanamuwinda.
Tangu Profesa Kapuya alipoondoka
nchini huku akizongwa na kashfa ya
kutishia kumuua binti anayedaiwa
kumbaka, polisi wamekuwa wakitamba
kutaka kumtia mbaroni na kuahidi
kuwa mara baada ya kurejea nchini
mbunge huyo angekuwa chini ya
ulinzi.
Gazeti hili juzi liliripoti mkakati wa
polisi kutaka kumtia mbaroni mbunge
huyo mara atakapotua kwenye Uwanja
wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere
jijini Dar es Salaam.
Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi
zilisema kuwa kumekuwa na shinikizo
kutoka ndani na nje ya jeshi hilo
kutaka waziri huyo wa zamani ahojiwe
kuhusiana na tuhuma zinazomkabili
za kutishia kumuua binti anayedaiwa
kumbaka.
Hatua ya polisi kutaka kumnasa
Kapuya akiwa uwanja wa ndege
inadaiwa kuchangiwa na taarifa ya
gazeti hili wiki iliyopita kwamba
baadhi ya vigogo wa jeshi hilo
walishiriki kufanikisha safari ya
mbunge huyo nje ya nchi huku
wakijua fika anatakiwa na polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kinondoni, Camilius Wambura,
alipoulizwa kuhusu ujio wa Kapuya na
kisha kuendelea kuachiwa huru,
alisema yuko nje ya Jiji la Dar es
Salaam na hakuwa na taarifa za
kurejea kwake.
Hata hivyo Kaimu Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Kinondoni, Yusuph Mrefu,
alipoulizwa kuhusu sakata la Kapuya,
alisema hakuwa na taarifa ya kile
kinachoendelea, kwa kuwa ndiyo
kwanza amekabidhiwa ofisi.
Mimi niambie jambo jipya, hapa
ofisini ndiyo leo nimeingia kukaimu,
sasa hayo mambo nitayajulia wapi, ni
vema ungeniambia jambo jipya
tuweze kutatua, alisema Mrefu.
Kwa upande wake, Bunge limesema
kuwa sakata la Profesa Kapuya
lilifikishwa bungeni na kubaini kuwa
ni la jinai, hivyo linapaswa kwenda
kwenye mkondo wa kisheria.
Akizungumza na gazeti hili jana,
Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila,
alithibitisha kulifahamu suala hili,
kwani binti aliyedai kubakwa na
kutishiwa kuuawa na mbunge huyo
alikwenda bungeni wakati Bunge la
13 lilipokuwa likiendelea mjini
Dodoma.
Suala la binti huyo lilifikishwa ofisini
kwangu kupitia kwa msaidizi wangu
ambaye alisikiliza hoja na rai yake na
kushauriwa kuwa hilo ni suala la jinai
na linapaswa liende katika mkondo
wa kisheria, hata hivyo binti huyo
alitambulishwa kwa Spika kama
kiongozi wa wabunge na kuelekeza
kuwa tumshauri alifikishe katika
mamlaka husika, alisema Kashilila.
Tayari binti anayedaiwa kubakwa na
kutishiwa kuuawa ameshafungua
jalada namba OB/RB/21124/13 katika
Kituo cha Polisi Oysterbay, jijini Dar
es Salaam na Jeshi la Polisi likaahidi
kumkamata Kapuya popote alipo ili
kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.
Tayari makachero wa polisi wameanza
kufuatilia namba ya simu inayodaiwa
kutumika kumtisha binti huyo na
wakati mwingine kutumika kurusha
pesa kwa njia ya mtandao,
zinazodaiwa kutoka kwa Profesa
Kapuya kwenda kwa binti huyo.
Nawasilisha.