Kardinali Protase Rugambwa, ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora ambapo Mnamo tarehe 13 Aprili 2023 aliteuliwa na Papa Francis kuwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora na tarehe 9 Julai 2023 akamteuwa kuwa ni Kardinali wa tatu kutoka nchini Tanzania na kusimikwa rasmi tarehe 30 Septemba 2023.
Mnamo tarehe 20 Aprili 2025 Kardinali Rugambwa aliongoza adhimisho la misa takatifu katika Parokia ya Theresia mtoto Yesu Jimbo kuu katoliki Tabora ambapo ilihudhuriwa na vijana waliokuwa wakipata Sakramenti takatifu ya Kipaimara pamoja na vijana wengine waliokuwa kwenye kongamano la Pasaka wapatao 792.
Madai
Kumekuwapo na Video inayosambazwa mtandaoni ikiwa ni sehemu ya mahubiri ya Kardinali Rugambwa siku ya pasaka ikidaiwa kuwa alikuwa akikemea vikali askofu aliyetoa tamko kinyume na msimamo wa kanisa.
Je ni upi uhalisia wa madai hayo?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia utafutaji wa maneno muhimu (Key Word Search) "Homilia ya Kardinali Rugambwa Pasaka" umebaini kuwa video hiyo imehaririwa na kupotosha uhalisia.
Video hiyo imehaririwa kwa kukata vipande vya video katika
mahubiri ya Kardinali huyo na kuviunganisha hatimaye kupoteza ujumbe halisi uliokusudiwa kwa waumini wa kanisa hiyo siku ya Pasaka.
Aidha kupitia mahubiri yake Kardinali Rugambwa alikuwa akiwasihi vijana waliokuwa wakipata Sakramenti takatifu ya Kipaimara pamoja na vijana wote waliokuwa kwenye kongamano la Pasaka wapatao 792 kudumu katika imani kwa kufuata mfano wa Mtume Petro huku akiwasisitiza kuitangaza imani kwa kusikia sauti ya Mungu inayosikika kupitia kanisa na kutoka katika maandiko.
"Basi bila uoga akaanza kuitangaza hiyo imani kitu ambacho na sisi inabidi kama kweli tumeimarika katika imani tusiwe na uoga tufuate mfano wa Petro kutangaza hiyo imani yetu bila uoga lakini msisahau tusiende tunasemasema tu, hapana tuwe na sababu kwanini tunafanya hivyo yawepo ya kweli kabisa tunayoenda kuyatangaza na ili tuyapate hayo kama nilivyosema lazima tusikie sauti ya Mungu, ambayo sauti ya Mungu hiyo kwetu sisi inasikika kupitia kanisa kutoka kwenye maandiko"
Kadhalika hii ni sehemu ya mahubiri hayo yaliyo na ujumbe wa kudumu katika imani bila uoga.
"Hawa ambao leo watapokea sakramenti ya kipaimara kuongozwa na nguvu hiyo ya roho mtakatifu mtaweza kuyafanya mengi, kwanza mtadumu katika hiyo imani na mtaweza kuyafanya yale ambayo ni mapenzi ya Mungu, katika maisha yenu, sikusema nampenda Mungu naamini katika Kristo aliyefufuka haitoshi, kwasababu huwezi kusema unampenda Mungu kama huoneshi katika matendo yako ambayo ndiyo yale aliyoyafunua Kristo kwa hao jirani zako. Ndugu zangu leo nisingependa kusema mengi napenda kusisitiza hilo moja la kudumu katika imani kufuata mfano wa hawa ambao wametutangulia."
"Tukianza na hao akina Petro mnafahamu kabisa kwamba tunayoyasikia katika juma hili kuu, Petro alipofikia wakati fulani alikuwa dhaifu akamkana huyo Kristo, lakini kwa sababu ya kuisikia hiyo sauti ya Mungu na akapenda aongozwe na huyo Mungu, alimuita alikubali na akabadilika na akawa imara."
"Basi bila uoga akaanza kuitangaza hiyo imani kitu ambacho na sisi inabidi kama kweli tumeimarika katika imani tusiwe na uoga tufuate mfano wa Petro kutangaza hiyo imani yetu bila uoga lakini msisahau tusiende tunasemasema tu, hapana tuwe na sababu kwanini tunafanya hivyo yawepo ya kweli kabisa tunayoenda kuyatangaza na ili tuyapate hayo kama nilivyosema lazima tusikie sauti ya Mungu, ambayo sauti ya Mungu hiyo kwetu sisi inasikika kupitia kanisa kutoka kwenye maandiko kama nilivyosema, kutoka katika mafundisho ya kanisa ndiyo tutaipata sauti ta Mungu.
Usiende na maneno yako tu na hasa kama ninyi vijana mtakutana na watu wengi sana wanaosema hili, wanasema lile wengine mnao hata madarasani kwenu huko, wanakuja na ya kwao tuwe waangalifu hapo tuangalie ni nani anatuambia na ni nini anatuambia kusudi badae na sisi tuweze kushuhudia kumshuhudia Kristu katika yale ambayo ni ya kweli"
View: https://youtu.be/bI2-kCWF2cw?si=-y_2UzZynrcastiQ