Karudi Baba Mmoja (Toleo Jipya)

Karudi Baba Mmoja (Toleo Jipya)

Ha ha ha haaa Ile ya sungura karuka ruka matunda hakufikia?


Hadithi inayokuja, ni ya sungura sikia
Hadithi uliyongoja, leo ninakuletea
Alitoka siku moja, njaa aliposikia
Njaa aliposikia, sungura nakuambia

Siku hiyo akaenda, mjini kutembelea
Akayaona matunda, mtini yameenea
Sungura akayapenda, mtini akasogea
Mtini akasogea sungura nakuambia

Endelea sasa.

 
Good staff ngoja nione kama nakumbuka
karuka tena karuka, mtini akarukia
......
naona nafanya kazi bila faida kujua
yakamtoka machozi sungura akagumia

mwengine aendelee
 
Karuka tena karuka,Matunda akarukia,
Mwisho wake akachoka, kachoka hata mkia
Penye mti akatoka, pembeni akasogea
Pembeni akasogea , Sungura nakuambia

Sizitaki mbichi hizi, Sungura akagumia,
Naona nafanya kazi, bila faida kujua,
Yakamtoka machozi, Matunda akalilia
Matunda akalilia,Sungura nakuambia


Zile zilikuwa ndiyo Shule . Za Juma na Roza
 
Ila kosa lilikuwa pale tulifundishwa eti Mzungu gani sijui akavumbua
mlima Kilimanjaro, wakati Wachaga wameishi na kulima kuuzunguka huo mlima
miaka elfu iliyopita.
Eti mzungu gani kavumbua ziwa Nyasa,Nyanza,Tanganyika. Sijui mto gani.
Duh !! hapa ukweli tulidanganywa:
 
Dah hyo kitu umenikumbusha mbali,then hapa nipo shop kwangu nasikiliza mtaa wa mangoma nyimbo za zamani dah full furaha.
 
Wadau tafadhali mwenye kumbukumbu niwekeeni Shairi hili;

Wakati titi la Nyati, hukamuliwa kwa shaka.
.....
Wakati Johari njema, hasa ule wa bahati.

Nawasilisha
 


Hadithi inayokuja, ni ya sungura sikia
Hadithi uliyongoja, leo ninakuletea
Alitoka siku moja, njaa aliposikia
Njaa aliposikia, sungura nakuambia

Siku hiyo akaenda, mjini kutembelea
Akayaona matunda, mtini yameenea
Sungura akayapenda, mtini akasogea
Mtini akasogea sungura nakuambia

Endelea sasa.


Dah mkuu malizia basi mbona umekatisha uhondo? Halafu kuna lile la fikiri sasa ashiba chakula kingi kwa baba.......
 
sikiri mimi maskini,uvivu wangu nyumbani
nikiwa uu njiani, nakufa hapa kwa nini
sadiki sasa ashiba chakula kingi kwa baba,
chakula kingi kwa baba nakufa hapa kwa nini?
nitalima kama sadiki, nitalima wala sichoki
na nyumbani tena sitoki, baba na mama nisamehe.

vipi kuhusu lile la "yai au kuku"?
 
Ninaye ndege mzuri, mrembo wa Kupendeza
Rangi zake mashuhuri, ni nne nawaeleza
Ndizo rangi za fahari, urembo kuutimiza
Ndege huyu ndege gani, hapa Kwetu Tanzania?
 
Tumeizika elimu, elimu ya kizamani
Elimu ile haramu, maana ya kikoloni
Imetuishia hamu, kuiga ya ugenini
Elimu yetu ya sasa yawafaa wananchi
 
Harudi baba mmoja, toka safari ya mbali
Harudi hata kiroja, bali kifo cha ambari
Harudi mbaba soja, na si sababu ya mali
Tanzania ya bazazi, arudi kufanya nini?

Baba alivyoondoka, katu hakutaka rudi
Alivyokwishachomoka, kurudi katu kwa budi
Nasema si kuropoka, kurudi hata kwa udi
Ufisadi wazi wazi, arudi kufanza kipi?

Kwanza kutokake zengwe, hata pasi kuipata
Vichaa ka wa Mirembe, wajaliwa uambata
Waruka wabemba bembe, bila senti katakata
Nyumbani hakuna kazi, arudi kufanza kipi?

Miaka yake yapita, nadhiri bado akiri
Ughaibu kajikita, kama hanazo akili
Bi Mkubwa amuita, imani yamuajiri
Tanzania ya makadhi, arudi kufanya nini?

Tanzania ya makadhi, ustaadhi wenye mahadhi
Ya milioni makazi, kimarekani si nazi
Sembuse tuso jahazi, wala mtumbwi wa Chazi
Tanzania ya maPazi, arudi kufanya nini?

Umesomeka Kiranga, utenzi wako nimeupenda
japo siwezi kutunga,ila mtaalamu kuimba.
Nyote vizuri mmeimba, na mashahiri mmeyapanga.
 
Mama wa kambo ni mama hadithi nawaletea,mimi yalinitokea, kwenye yetu familia,mimi baba mama pia, Mungu alitujalia,maisha kufurahia, mama wa kambo ni mama,mimi naye twapendana
 
Wangapi wanakumbuka shairi hili?

Karudi Baba mmoja, toka safari ya mbali,
Kavimba yote mapaja, na kutetemeka mwili,
Watoto wake wakaja, ili kumtaka hali,
Wakataka na kauli, iwafae maishani.

Akatamka mgonjwa, ninaumwa kweli kweli
Hata kama nikichanjwa, haitoki homa kali
Roho naona yachinjwa, kifo kimenikabili,
kama mwataka kauli, semani niseme nini.

Yakawatoka kinywani,maneno yenye adili,
Baba yetu wa thamani,sisi tunataka mali,
Urithi tunatamani,mali yetu ya halali,
Sema iko wapi mali, itufae maishani.

Baba aliye kufani, akajibu lile swali,
Nina kufa maskini, baba yenu sina mali,
Neno moja lishikeni, kama mnataka mali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakazidi kumchimba, baba mwenye homa kali,
Baba yetu watufumba, hatujui fumbo hili,
Akili yetu nyembamba, haijajua methali,
Kama tunataka mali, tutapataje shambani.

Kwanza shirikianeni, nawapa hiyo kauli,
Fanyeni kazi shambani, mwisho mtapata mali,
Haya sasa buriani, kifo kimeniwasili,
Kama mnataka mali mtayapata shambani.

Alipokwisha kutaja, fumbo hili la akili,
Mauti nayo yakaja, roho ikaacha mwili,
Na watoto kwa umoja, wakakumbuka kauli,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Fumbo wakatafakari, watoto wale wawili,
Wakakata na shauri, baada ya siku mbili,
Wote wakawa tayari, pori nene kukabili,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakazipanda shambani, mbegu nyingi mbalimbali,
Tangu zile za mibuni, hata zitupazo wali,
Na mvua ikaja chini, wakaona na dalili,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Shamba wakapalilia, bila kupata ajali,
Mavuno yakawajia wakafaidi ugali,
Wote wakashangilia, usemi wakakubali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakawanunua ngómbe, majike kwa mafahali,
Wakapata na vikombe, mavazi na baskeli,
Hawakuitaka pombe, sababu pombe si mali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakaongeza mazao, na nyumba za matofali,
Pale penye shamba lao, wakaihubiri mali,
Walikiweka kibao, wakaandika kauli,
KAMA MNATAKA MALI, MTAYAPATA SHAMBANI.
 
Hili shairi umenikumbusha mbali sana,tulipigwa ndani ya wiki kila mtu alikuwa anachana mistari kama hana akili nzuri.Chezea kipigo weye!
 
ha ha ha ha ha sijui ilikuwa darasa la tano... kweli zamaniiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii
 
Aisee ngoja nimprintie mwanangu, atajifunza kitu hapo hata kama ni lugha tu. Hii imenikumbusha marehemu dada yangu alivyokuwa akiniimbia nilivyokuwa mdogo!
 
Back
Top Bottom