Huku ukibainisha vigezo muhimu vya majibu yako, Ni ipi kati ya picha hizi mbili, imetengenezwa kwa kutumia Akili Unde?
- Tunachokijua
- Akili Unde (AI) ni seti ya teknolojia zinazoiwezesha kompyuta kutekeleza majukumu mbalimbali ya kina na kwa uwezo mkubwa kadri ya maelekezo ya mtumiaji, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kuona, kuelewa na kutafsiri lugha inayozungumzwa na maandishi, kuchanganua data, kutengeneza picha na video na kutoa mapendekezo ya utatuzi wa matatizo mbalimbali.
Aidha teknolojia hii imekuwa muhimu katika kurahisisha ufanisi wa shughuli za kila siku na hii ni pindi tu inapotumika kwa nia iliyo njema, lakini inapotumiwa kwa nia ovu huweza kusababisha madhara makubwa kwa watu, mathalani uwepo wa taarifa potofu unachangiwa pia na teknolojia hii ambayo watu hutumia kutengeneza na kusambaza taarifa zisizo sahihi mfano picha, sauti, na video.
Katika kujenga uwezo wa kumuwezesha kila mmoja kutambua maudhui yaliyotengenezwa kwa teknolojia hiyo ili kuepuka upotoshaji, wadau wa JamiiCheck walishiriki kuthibitisha picha mbili kwa kubainisha iliyotengenezwa na sababu halisi zinavyodhihirisha uhalisia huo.
Uhalisia wa picha
Picha zote mbili zinavutia na kushawishi mtazamaji hata kufanya zote zionekane kuwa halisi jambo ambalo ni tofauti. Picha iliyopewa herufi 'A' licha ya kuwa na muonekano mzuri na wa kuvutia lakini ina mapungufu kadhaa ambayo yanatofautiana na uhalisia jambo linalodhihirisha kutengenezwa kwa Akili Unde.
Sehemu ya mapungufu hayo ni pamoja na uwepo wa nyumba zenye urefu usio wa kawaida, mashine zinazotumika kwenye ujenzi wa barabara (Bulldozer, excavator) ambazo hazina matairi yanayowezesha mashine hizo kutembea.
Gari ndogo nyeupe iliyopo upande wa mbele, tairi yake ya nyuma upande wa kulia haina uwiano sawia na tairi za mbele.
Aidha Picha B, ni picha halisi iliyotumika kutengeneza picha A kwa kutumia Akili Unde. Katika picha hii hakuna madhaifu kama ambavyo yanaonekana katika picha ya awali. Chanzo halisi cha picha B ni kutoka Wizara ya ujenzi pamoja na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) walioichapisha katika mtandao wa Instagram mnamo mwezi Mei 27, 2025 ikiwa ni ujenzi wa barabara unaoendelea mikoa ya kusini.