mkuu ... Tanzanian's zombies will arrive very soon...... the first victims will be the likes of C.Kombani.., F.Werema.., N.Mkono..., and MS
Kwa maoni yangu, habari fupi iliyotolewa juu kinachodaiwa kusemwa na Mh Mkono ni fupi sana kuweza kubaini ni nini hasa alichokusudia na hoja zipi alizokuwa anajenga. Ningemuomba mhariri kwa hisani yake atutolee habari hiyo kwa urefu ili tuwe na haki ya kumkosoa au kumuunga mkono Mkono kadili ya upeo wetu na misimamo yetu.
Kwa upande mwingine, sijaridhika na namna baadhi ya wachangiaji walivyokosa subira kuvumilia hoja tofauti na zao. Nionavyo mimi si lazima wanachama wote wa forum hii kuwa na msiomamo mmoja juu ya mabadiliko ya katiba. Wengine wanaweza kuona kwamba katiba iliyopo ina mapungufu mengi ambayo hayawezi kurekebishwa zaidi ya kuifuta na kuandika nyingine. Wengine wanaweza kuwa na mtizamo kama wa mh. Mkono kwamba kuifuta katiba mpya ni sawa na kupindua Constititional Order tuliyonayo na kuleta mfumo na utaratibu mwingine kabisa.
Kwa wale waliobahatika kukaa katika darasa za sheria watakuwa wamekutana na falsafa nyingi kinzani juu ya maana na nafasi ya katiba katika nchi. Wapo wanatizama katiba kama mama wa sheria na mamlaka zote za nchi. Kwamba kufutwa kwa katiba iliyopo huja tu pale panapokuwa mabadiliko ya msingi sana yanayofanya kanuni na miongozo iliyomo katika katiba na sheria pamoja na mfumo mzima wa kisiasa kupitwa na wakati. Katika sehemu kubwa ya kihistoria, baadhi ya wanafalsafa wa sheria na katiba wanasema, kufutwa kwa katiba na kuandikwa mpya hutokea pale dola iliyopo inang'olewa madarakani, kama ilivyokuwa wakati wa kuondolewa kwa dola za kikoloni. Kwa mitazamo yao, mapungufu mengine ya kikatiba yanaweza kuondolewa kwa marekebisho ambayo huendana na aidha kufutwa kwa baadhi ya vifungu katika katiba na kuandikwa vingine bora zaidi au kuongezwa vifungu vingine kadili vitakavyohitajika.
Jambo la kujiuliza hapa ni je kuna mabadiliko gani ya msingi yaliyotokea Tanzania yanayoifanya Katiba iliyopo kupitwa na wakati? Mmoja kati ya magwiji wakubwa wa sheria ya siasa na katiba Prof Issa Shivji analijibu suala hili kwa kuanisha mabadiliko mbalimbali kama vile kuondolewa azimio la Arusha na kuanzishwa mfumo vya uchumi huria na kuanzishwa mfumo wa vyama vingi badala ya mfumo wa chama kimoja. Maoni ya PROF Shivji pia yanajitokeza katika Repoti ya Utafiti wa Tume ya Nyalali kuhusiana na kuingia au kutoingia kwa Tanzania katika mfumo wa vyama vingi.
Ikumbukwe kwamba kabla Tanzania hatujaingia katika mfumo wa vyama vingi, katiba yetu ilifanyiwa marekebisho ya msingi kupitia Marekebisho ya 8 ya Katiba na baadae ya 9 hadi 12. Marekebisho hayo kwa kiasi fulani yalipunguza mapungufu ya kikatiba yaliyotokana na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi lakini mapungufu yangali yanaonekana. Ni kutokana na ukweli huo kwamba baadhi ya wanazuoni wanaona mapungufu yaliyomo katika Katiba hayawezi kuisha kwa marekebisho, katika lugha ya marehemu Prof Haroub 'viraka". Lakini bado mtu anweza kujenga hoja kwamba pengine hata Tanzania tungeandika Katiba mpya mapungufu yangeendelea kuwepo kutegemeana na namna tulivyoiunda hio katiba kama vile matatizo hayo yangeisha kama marekebisho ya 8 yangefanyika kwa umakini zaidi na kuwashirikisha watu zaidi. Nini ni kweli na nini si sahihi inategemeana na namna tunavyojenga hoja na kufanya utafiti wa kutosha. Pia inategemeana na matashi ya watu.
Dhana ya katiba na nafasi yake katika jamii ni kitu kinachoumiza akili na kinahitaji kuangaliwa kwa jicho pevu. Katiba sio maandishi tu yaliyomo katika kitabu kinachoitwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, 1977. Katiba ni zaidi ya hapo. Uganda ilikuwa ni nchi ya kwanza kuandika Katiba mpya wakati wa upepo wa vyama vingi. Lakini hatuwezi kusema kwamba Uganda ni ya kidemokrasia zaidi ya Tanzania au Kenya. Pia hatuwezi kusema kwamba matatizo ya kidemokrasia Uganda (kama yapo) yanasababishwa na Katiba yao mpya kutokuwa nzuri. Ninachomaanisha hapa ni kwamba tunapojadili katiba mpya tunapaswa kujadili kwa upana zaidi kwa kuingalia katiba iliyopo tukiihusisha na histria nzima ya siasa na uchumi wa nchi, maisha ya watanzania, mahusiano yetu ya kijamii na maadili kwa ujumla.
Kwa haya niliyosema sikuwa na lengo la kufanya hitimisho lolote bali kufanya madodoso ya hoja mbalimbali ili kupanuwa mawazo ya wachangiaji na uwigo wa mjadala kwa nia ya kuboresha zaidi. Kama kunasehemu nitakuwa nimewachanganya wbnaadhi ya wachangiaji hiyo itakuwa imetokana na mapungufu yangu katika lugha.