Nachelea kusema kwamba kumekua na shutuma kuu zinazoelekezwa kwa Serikali ya Tanzania kwamba imezigandamiza haki za binadamu haswa haki ya Uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.
Ni ukweli ulio wazi kwamba Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 katika Ibara ya 18 Ibara ndogo ya kwanza imetoa haki ya kila raia kuwa na uhuru wa kutoa maoni kwa maana ya kujieleza na kutoa nje mawazo kuhusu masuala mbalimbali na pia kupokea na kuto taarifa kutoka katika chombo chochote.
Hivyo basi sio kosa kisheria kwa raia yeyote kutoa maoni na mawazo kwa sababu tayari Katiba ambayo kimsingi ndio sheria mama imeshakikisha kwamba haki hiyo inapatikana kwa kila raia.
Nikiinukuu Ibara hiyo kama ilivyoandikwa inasema hivi;
"Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati."
Hapo mwanzo kabisa wa ibara hiyo ya 18 tunaona neno “BILA YA KUATHIRI SHERIA ZA NCHI” Sheria za nchi ni zipi? Sheria za nchi ni jumla ya ile miswada ambayo ilipitishwa na Bunge katika taratibu na kanuni zake za utungaji wa sheria kisha ikasianiwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano na kuwa sheria kamili.
Sawa, Katiba imetoa haki ya kutoa maoni na kujieleza lakini pia Katiba hiyo hiyo imetoa masharti kwamba unapotaka kutekeleza haki yako hiyo basi inakupasa usivunje sheria nyingine za nchi.
Ibara ya 30 ya Katiba yetu imeweka Mipaka kwa haki na uhuru na hifadhi kwa haki na wajibu.
Katiba inasema;
"Haki na uhuru wa binadamu ambavyo misingi yake imeorodheshwa katika Katiba hii havitatumiwa na mtu mmoja kwa maana ambayo itasababisha kuingiliwa kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma"
Maana yake ni kwamba haki na uhuru wa mtu binafsi haupaswi kuwa chanzo cha kukosa haki na uhuru kwa watu wengine au umma kwa ujumla. Hivyo hakuna haki au uhuru usio na mipaka. Mipaka au ukomo wa haki na uhuru ni kwa kiwango haki na uhuru wako unavyoweza kuathiri au kuingilia haki na uhuru wa wengine.
Kanuni kuu ya kufahamu juu ya dhana ya haki na uhuru wako ni ile kanuni ya kimaandiko inayosema ‘mpende jirani yako kama nafsi yako mwenyewe’ hii inaonesha kwamba kwa kiwango kile ambacho ungependa haki zako na uhuru wako uheshimiwe na kulindwa basi hakikisha nawe unafanya kwa kiasi hicho kwa jirani yako. Jirani yako ni mtu yeyote ambaye anaathirika kwa njia moja ama nyingine kutokana na kauli zako au matendo yako. Kama usingependa utu wako udhalilike, kwa matusi kebehi na fedheha basi jitahidi pia uulinde utu huo wa mwenzako.
Katiba inaendelea pia kuainisha juu ya mipaka ya haki na uhuru kwa kusababisha sheria kutungwa ili kulinda haki za watu wengine na maslahi mapana ya umma kwa ujumla, sawa na Ibara ya 30 (2) inasema;
"Ifahamike kwamba masharti yaliyomo katika Sehemu hii ya Katiba hii, yanayofafanua misingi ya haki, uhuru na wajibu wa binadamu, hayaharamishi sheria yoyote iliyotungwa wala kuzuia sheria yoyote kutungwa au jambo lolote halali kufanywa kwa mujibu wa sheria hiyo ."
Hapa maana yake ni kwamba mamlaka pamoja na kuzitambua na kuziheshimu haki na uhuru wa kila raia, zinaweza kutunga sheria kwa ajili ya kulinda na kutetea haki za watu wengine na makundi mengine ikiwepo serikali na mambo yote ya maslahi ya umma.
Mfano Sheria ya Kanuni ya adhabu,Sura ya 16 kifungu cha 89 kifungu kidogo cha kwanza kimeweka adhabu ya kifungo cha miezi 6 kwa mtu yeyote atakayetumia lugha ya matusi dhidi ya mtu mwingine.
Hivyo mtu kabla hujaamua kutekeleza haki yako yoyote lazima uifahamu mipaka yake na namna ambavyo sheria zinalinda watu wengine na mamlaka za nchi dhidi ya kuharibiwa sifa au udhalilishaji.
Eneo la mipaka ya haki na uhuru limekuwa na changamoto kubwa sana katika kufikia mwafaka, kwani wapo wanaoamini kuwa haki hizi za kibinadamu hazina mipaka lakini wapo wanaamini kuwa haki zina mipaka. Katiba imeweka wazi kuwa katika kutekeleza haki yako hakikisha upo ndani ya mipaka husika.
Hakikisha kwenye uhuru wako wa kujieleza au imani yako au faragha kwa namna yoyote hauingilii haki na uhuru wa watu wengine, shughuli za umma, mamlaka za nchi, hadhi za watu ikiwa ni viongozi au raia wa kawaida.
Ni rai yangu kwa wananchi wenzangu kuwa na taadhari katika maneno na vitendo tunavyofanya kwa kudhani kuwa tuna haki tu ya kufanya chochote, sheria zipo na mamlaka za kutekeleza sheria zipo, tuepuke kuwa na matumizi mabaya hasa ya mitandao kutuma na kupokea jumbe ambazo zinaweza kuingilia haki na uhuru wa watu wengine na mamlaka mbali mbali katika nchi yetu.
Hakuna Haki na Uhuru usio na mipaka, jua mipaka yako uepuke madhara kwa wengine na juu yako. Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote.
Tekeleza haki zako za kikatiba lakini zingatia usivuke mpaka wala kuvunja sheria nyingine za nchi .Usipofanya hivyo nyundo ya sheria itakugonga na hautakua na mtetezi wa kukusaidia pindi utakapofungwa gerezani.