[h=2][/h] Ijumaa, Agosti 31, 2012 06:27 Na Eliya Mbonea, Arusha
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimekumbwa na tuhuma nzito baada ya kiongozi wake mmoja kukamatwa kwa kosa la utapeli wa Sh milioni 16.
Kiongozi huyo ambaye ni Katibu wa Kata ya Endulen wilayani Ngorongoro, Denia Paul (33), anadaiwa kuwatapeli wafanyakazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA) kiasi hicho cha fedha, kwa kujifanya kuwa yeye ni Katibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini wake mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas, alisema kuwa, mtuhumiwa huyo alikamatwa Agosti 27, mwaka huu.
Kabla ya kukamatwa, Paul aliwapigia simu wafanyakazi wa NCCA, akijitambulisha kuwa yeye ni Mwenyekiti wa Tume iliyoundwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.
Alidai anaitwa David Kagasheki, Katibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, ambaye amejumuishwa kwenye tume hii ambayo ina kazi ya kuchunguza tuhuma mbalimbali za wizara hii.
Aliwaambia wafanyakazi wa NCCA, kuwa atakuwapo Ngorongoro hadi Agosti 29, mwaka huu na siku ambayo ingefuata angekuwa Ngorongoro kwa ajili ya uchunguzi.
Inadaiwa katika mazungumzo hayo, alimwambia mfanyakazi mmoja aandae Sh milioni 10, wakati mwingine aliambiwa aandae Sh milioni 6, ili mambo yao yawe safi, alisema Kamanda Sabas.
Baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa hizo, liliweka mtego na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa eneo walilokubaliana kukutana.
Kwa upande wake, Katibu wa CHADEMA, Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, akizungumzia tukio hilo, alikiri kiongozi huyo kukamatwa.
Kweli kiongozi wetu amekamatwa, tunafanya utaratibu wa kumpata wakili atakayetusaidia na kujua ukweli wa tukio hili, ila ninachoweza kusema kwa kifupi ni kwamba taratibu zote zimekamilika, alisema Golugwa.
Alisema anasikitishwa na taarifa ya polisi kwani namba ya simu ya kiongozi huyo, inayodaiwa kutumika si ya kweli.
Paul alifika Mjini Arusha kwa ajili ya kulipia ada za shule za watoto wake, ndipo akapokea simu ya mtu asiyemfahamu ambaye alimtaka wakutane Hoteli ya Kibo Palace na kwa kuwa alitambua hana kosa, alilazimika kwenda.
Alipofika pale, aliona watu wakimuuliza wewe ndiye fulani?, wakampatia begi kushika, baada ya kukataa akajikuta akikamatwa kwa nguvu na kunyanganywa simu zake na baada ya kunyanganywa simu zake, aliwekewa laini ya simu ambayo imesajiliwa kwa jina la David Kagasheki, alisema Golugwa.
[h=4]Toa Maoni yako kwa habari hii[/h]