Wahariri waandamana Dar wakiwa wameziba midomo
Na Boniface Meena
KWA mara ya kwanza katika historia ya habari nchini, wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini jana waliandamana kuishinikiza serikali kuliondolea gazeti la Mwanahalisi kifungo cha miezi mitatu, huku wakiwa wamebandika plasta midomoni kuashiria kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari.
Gazeti hilo la kila wiki lilifungiwa kwa miezi mitatu baada ya kuandika habari inayoeleza mikakati inayoendelea ndani ya Chama cha Mapinduzi ya kumuondoa Rais Jakaya Kikwete kwenye mchakato wa kuwania urais kupitia chama hicho katika uchaguzi wa mwaka 2010.
Katika maandamano hayo yaliyoanzia Mtaa wa Lugoda na kuishia ofisi za Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, wahariri hao, ambao waliungwa mkono na taasisi nyingine za kijamii, walisema wanapinga kwa kauli moja uamuzi wa serikali kulifungia gazeti hilo na kudai kuwa kitendo hicho ni kuvinyima uhuru vyombo vya habari.
Wakiwa wamebeba mabango yaliyokuwa na ujumbe tofauti ukieleza athari za kuchezea uhuru wa vyombo vya habari, wahariri hao waliandamana kupitia Barabara ya Kilwa, Sokoine na kumalizia Samora, ambako kuna ofisi za wizara hiyo.
Mabango hayo yalikuwa na ujumbe kama "Uhuru wa habari ni chanzo cha demokrasia," "Sheria ya magazeti ya 1976 ni ya kikandamizaji- haifai" na ujumbe mwingine ukisema, "Kufungiwa MwanaHalisi ni njama za mafisadi" na "MwanaHalisi jela, mafisadi huru".
Baada ya kufika jengo hilo, wahariri walituma wawakilishi wao kwenda ndani ya ofisi kukabidhi barua iliyokuwa na ujumbe wao na ubarua hiyo ikakabidhi kwa kaimu mkurugenzi wa Idara ya Habari- Maelezo, Habib Nyundo ambaye badala ya kuzungumzia hoja zilizo kwenye barua hiyo alipinga maandamano hayo na kudai kuwa Jukwaa la Wahariri, ambalo liliandaa maandamano hayo, halijasajiliwa kisheria.
"Jukwaa la wahariri halijasajiliwa na msilitumie kwani halipo kisheria," alisema Nyundo.
Lakini akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhi ujumbe wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, ambaye ni kaimu mwenyekiti wa chombo hicho, alisema: "Nashangazwa na kauli ya serikali kwamba jukwaa hili la wahariri halijasajiliwa. Hilo lililosajiliwa wahariri wake wako wapi?
"Uhariri si kazi ya kudumu na hilo jukwaa la wahariri ambalo serikali inadai limesajiliwa liko wapi na wahariri wake wako wapi. Wahariri wote wa vyombo vyote vikubwa vya habari ndio sisi hapa. Hao hilo Jukwaa la Wahariri lililosajiliwa wako wapi.
"Serikali lazima ijue kuwa enzi za kuwadanganya wananchi zimepitwa na wakati."
Jukwaa la Wahariri ambalo liliandaa maandamano hayo liko kwenye mchakato wa kusajiliwa, lakini halitajisajili Wizara ya Mambo ya Ndani kama lilivyokuwa la awali. Jukwaa hilo lilitazamiwa kuwasilisha maombi yake Wizara ya Viwanda na Biashara, likitaka hadhi ya kampuni.
Kuhusu kitendo cha serikali kulifungia gazeti la MwanaHalisi, Kibanda alisema: "Walitakiwa kwenda mahakamani kulifungia gazeti hilo kama walivyozuia mgomo wa walimu. Kulifungia inatia shaka kwani serikali na CCM zina mkono katika vyombo vya habari.
"Inashangaza serikali haitaki kujifunza kutoka kwa vyombo vya habari na inashangaza jinsi gani wanavyojaribu kuvunja uhusiano na vyombo vya habari.
"Nia ya kuikosoa serikali ni kwa ajili ya mustakabali wa taifa na siyo wa mtu binafsi. Taifa kwanza, mambo mengine baadaye."
Mbali na hilo pia Kibanda alihoji kitendo cha mkurugenzi wa MwanaHalisi, Saed Kubenea kutakiwa kuripoti polisi makao makuu kila siku kwa ajili ya kuweka saini katika kitabu bila kupewa maelezo yoyote.
Kibanda alisema atawasiliana na taasisi za kisheria ambazo ni wadau wa habari kuangalia jinsi ya kupambana na amri hiyo, akiita kuwa ya unyanyasaji.
Mwenyekiti wa taasisi ya vyombo vya habari vya kusini mwa Afrika, Misa-TAN, Ayoub Rioba, ambaye alishiriki maandamano hayo, alisema tabia ya serikali kufungia vyombo vya habari si tabia ya nchi inayofuata demokrasia.
"Watanzania hatuko tayari kuangalia mienendo inayotetea maslahi binafsi kupitia vyombo vya habari," alisema Rioba.
Naye mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini (TAMWA), Ananilea Nkya alisema kitendo ilichofanya serikali ni kuwafunga mdomo wananchi.
Alisema ni muhimu serikali ikatafakari uamuzi huo upya kwani inatafuta ugomvi na vyombo vya habari.
"Serikali ilifungulie haraka sana gazeti la Mwanahalisi kwani kulifungia ni kuwafunga wananchi mdomo," alisema Nkya.
Mhariri wa gazeti la Kulikoni, Nyaronyo Kicheere alisema kila kunapotokea habari mbaya, lazima kuwepo na mlalamikaji ambaye ndiye huchukua hatua ya kufungua kesi.
"Katika suala hili, mlalamikaji ni nani... Ridhiwani Kikwete amelalamika? Hakuna aliyelalamika, lakini serikali imeamua kulalamika kwa niaba na kuchukua hatua kwa niaba ya mlalamikaji. Hii siyo sahihi," alisema mwandishi huyo mwandamizi.
Ridhiwani, mtoto wa Rais Kikwete, alihusishwa kwenye habari hiyo iliyochapishwa na gazeti la MwanaHalisi.
Alisema uamuzi wa serikali katika kulifungia Mwanahalisi ni kijichimbia shimo kwa kuwa haina hoja katika suala hilo.
"Serikali haiwezi kuwa kila kitu kwa kutoa maamuzi ambayo hayana hoja ya msingi," alisema Kicheere.
Alisema anashangazwa na serikali kufanya uamuzi huo wakati mtoto wa Rais Kikwete, Ridhiwani ambaye alihusishwa kwanye habari ile hajawahi kwenda mahakamani kulishitaki Mwanahalisi hivyo serikali imeingilia nafasi ya watu wengine.
Mwananchi Tanzania News Paper