Kauliza muulizaji nani Sheikh Yusuf Badi?

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
KAULIZA MUULIZAJI NANI SHEIKH BADI?

Sheikh Muhammad Yusuf Badi alikuwa sheikh maarufu Lindi na sehemu yote ya Jimbo la Kusini, yaani Southern Province.

TANU iliasisiwa Lindi mwaka wa 1955 tayari Nyerere kesharudi UNO safari ya kwanza na alifika Lindi kutia nguvu TANU.

Kisa kirefu.
Tuingie kwa Sheikh Badi:

''Nyerere aliporudi Lindi mwaka 1959, TANU ilikuwa ina nguvu sana na ilikuwa imekumba kila mtu.

Wale watumishi wa serikali wengi wao wakiwa Wakristo, walio kuwa wakiibeza TANU mwaka 1955 kwa sababu ilikuwa ikiongozwa na Waislam ‘’wasiokuwa na elimu,’’ ukweli ulikuwa umewadhihirikia na sasa walikuwa wakionyesha heshima kwa chama.

Hawakuwa na khiyari na ilibidi waonyeshe heshima kwa sababu bwana mwenyewe, yaani serikali ya kikoloni, ilikuwa na heshima kwa TANU.

Serikali ilikuwa imetambua kuwa dhamiri ya watu ya kukataa kutawaliwa haiwezi tena kupuuzwa. Nyerere alikuwa amelihutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa mara mbili, mara ya pili ikiwa mwaka 1956.

Ujumbe wa TANU ulikuwa wazi, watu wa Tanganyika walikuwa tayari kujitawala.

Kila siku zilivyopita ndivyo TANU ilivyopata nguvu.

Rashidi Salum Mpunga, dereva wa lori, aliweza kumshawishi na akafanikiwa kumuingiza TANU mmoja wa masheikh wenye kuheshimiwa sana mjini Lindi na mshairi maarufu, Sheikh Mohamed bin Yusuf Badi.

Sheikh Badi alipoingia TANU kwa ajili ya heshima yake na kukubalika na watu, idadi kubwa ya Waislam walimfuata na kukata kadi za TANU.

Nyerere alipokuja Lindi kujadili tatizo la kura tatu na uongozi wa Jimbo la Kusini, Sheikh Yusufu Badi alimpokea Nyerere na madras yake, wanafunzi wakimwimbia Nyerere kasda na kumpigia dufu.

Kuanzia hapo sasa kila mtu alijiunga na TANU.

Hapakuwa na yeyote aliyekuwa na uwezo wa kupambana na TANU kama ilivyokuwa mwaka wa 1955 pale watu walipotishwa kuwa TANU ni chama cha Waislam kitaleta vita nyingine ya Maji Maji.

Polepole lakini na kwa kwa uhakika, TANU ilingia ndani ya maeneo ya yaliyokuwa ya upinzani huko Songea, Masasi, Tunduru na Newala, nyumbani kwa Yustino Mponda aliyekuwa mpinzani mkubwa.

Lakini matukio mawili ya kumbukumbu kubwa yalikuwa katika safari ya pili ya Nyerere alipozuru tena Jimbo la Kusini.

Kumbukumbu ya kwanza ilikuwa tawaswil aliyosomewa Nyerere na Sheikh Yusuf Badi mwenyewe pamoja na Waislam aliowachagua yeye sheikh mwenyewe maalum kwa hafla hiyo, pamoja na waliochaguliwa na masheikh wengine.

Kumbukumbu ya pili ni karamu iliyoandaliwa kwa heshima ya Nyerere na Mussa Athumani Lukundu, kiongozi wa Dockworkersí Union.

Siku ya ukumbusho mkubwa sana mjini Lindi ilikuwa siku ya uhuru, tarehe 9 Desemba, 1961.

Sheikh Badi, bingwa wa mashairi, aliombwa na TANU kuandika hotuba ya uhuru itakayotolewa na Yusuf Chembera mbele ya DC akiwa kama mwakilishi wa utawala wa Kiingereza uliokuwa uking’oka.

Hotuba hiyo ya Sheikh Badi na iliandikwa kwa Kiarabu na Chembera.

Akiwa mtoto mdogo Chembera alipelekwa kwa Sheikh Yusuf Badi na baba yake kwenda kusoma elimu ya dini na aliendelea kuwapo hapo chuoni kwa Sheikh Badi hadi alipohitimu.

Sheikh Badi hakuona kama ipo hotuba yoyote iliyoandikwa na mwanadamu iliyostahiki hafla kama ile ya siku ya kujikomboa kutoka minyororo ya ukoloni.

Sheikh Badi alimsomea mwanafunzi wake Chembera, dua ya kunut ambayo husomwa na Waislam katika kila sala ya alfajir.

Usiku wa manane wa tarehe 9 Desemba, 1961 ulikuwa usiku adhim sana kwa wote wawili, mwalimu na mwanafunzi wake, pale watu walipokusanyika katika uwanja wa gofu wa Lindi na kumsikiliza Chembera akisoma kunut kupokea uhuru wa Tanganyika."

(Kutoka kitabu cha Abdul Sykes 1998)

Pengine kama si kwa Sheikh Muhammad Yusuf Badi kupewa mtaa mchango wake katika kupigania uhuru wa Tanganyika usingefahamika.

 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…